Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

TV

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Ubabe big six

Big Six Pic Ubabe big six

Thu, 6 Jul 2023 Chanzo: Mwanaspoti

Kocha mkuu mpya wa Chelsea, Mauricio Pochettino amedai amejiunga na timu bora kabisa England katika kipindi cha miaka 15 iliyopita.

Kocha huyo wa zamani wa Tottenham Hotspur na Paris Saint-Germain, Pochettino alisema: “Katika kipindi cha miaka 10, 12, 15 iliyopita, Chelsea imekuwa timu bora England.”

Hata hivyo, hilo halina ukweli. Kwa kuangalia mataji, Manchester City ndiyo timu iliyoonyesha ubora mkubwa na kubeba ubingwa mara nyingi kuwazidi Chelsea hasa baada ya kunyakua mataji matatu makubwa msimu uliopita, iliponyakua Ligi Kuu England, Kombe la FA na Ligi ya Mabingwa Ulaya.

Kauli hiyo ya Pochettino imewakera mashabiki wa timu yake ya zamani, Spurs - na walimshangaa Muargentina huyo kutoa maneno kama hayo wakati alipofanya mahojiano yake ya kwanza kama kocha wa Chelsea.

Mashabiki wa Spurs wamemshutumu Pochettino kwa kukosa heshima baada ya kuwaelezea mahasimu wao Chelsea kama timu bora zaidi katika kipindi cha miaka 15 iliyopita.

Muargentina huyo mwenye umri wa miaka 51 aliongoza Tottenham kucheza fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya mwaka 2019. Lakini, mwenyekiti wa Spurs, Daniel Levy aliwashtua mashabiki wa timu hiyo baada ya kumfuta kazi Pochettino miezi michache baadaye kutokana na kushindwa kuipa taji lolote timu hiyo katika kipindi chake cha miaka mitano aliyonoa timu hiyo.

Kwa nini maneno ya Pochettino hayana ukweli kwa kudai Chelsea ndio timu bora zaidi katika kipindi cha miaka 15 iliyopita? Majibu hayo hapo ikizingatiwa mataji yaliyobebwa ndani ya muda huo.

1. Man City - mataji 17

Kikosi hicho cha Kocha Pep Guardiola, Man City kiliichapa Inter Milan na kushinda taji la Ligi ya Mabingwa Ulaya kwa mara ya kwanza kwenye historia yao mwezi uliopita.

Msimu huo huo uliopita, waliweka jina lao kwenye kumbukumbu tamu kabisa kwa kubeba mataji matatu makubwa ndani ya msimu mmoja na hivyo kusisitiza Man City ndiyo timu iliyopata mafanikio makubwa na ubora mkubwa kwa miaka 15 iliyopita. Waliizidi ujanja Arsenal kwenye taji la Ligi Kuu England na waliichapa Manchester United kwenye fainali ya Kombe la FA, hivyo kufikisha mataji 17 katika kipindi hicho cha miaka 15 iliyopita.

2. Chelsea - mataji 14

Kabla ya makali yao ya msimu uliopita na kubeba mataji matatu, Man City ilikuwa imelingana na Chelsea kwa mafanikio yao ya miaka 15 iliyopita na kila timu ilikuwa imebeba mataji 14. Lakini sasa kwenye msimamo wa mataji katika muda huo, The Blues inashika namba mbili, lakini wao wakiwa wamebeba taji la Ligi ya Mabingwa Ulaya mara mbili ndani ya muda huo, hakuna timu nyingine ya England iliyofanya hivyo kwa miaka 15 iliyopita. Chelsea pia ndani ya muda huo imebeba Kombe la FA mara nne, Kombe la Ligi na Uefa Super Cup, huku wakishinda pia Klabu Bingwa Dunia na Europa League mara mbili.

3. Man United - mataji 12

Chelsea imeizidi Man United kwa mataji mawili na kuwafanya wababe hao wa Old Trafford kushika namba tatu kwa timu zilizopata mafanikio makubwa na bora kwa miaka 15 iliyopita. Man United ilibeba mataji manne katika miaka yake ya mwisho ya Kocha Sir Alex Ferguson, huku taji lao la mwisho la Ligi Kuu England lilikuwa 2013, pia ndani ya miaka hiyo 15, imebeba Ligi ya Mabingwa Ulaya na Klabu Bingwa Dunia. Man United ilibeba pia Kombe la Ligi mara nne na Europa League na Kombe la FA na hivyo kufikisha mataji 12 kwa miaka 15 iliyopita.

4. Liverpool - mataji 7

Ndani ya miaka 15 kwa maana ya hesabu za kuanzia 2008 hadi sasa, Liverpool imeshinda mataji saba, ikiwamo ya Ligi Kuu England, Ligi ya Mabingwa Ulaya, Klabu Bingwa Dunia, Uefa Super Cup na Kombe la FA. Ndani ya muda huo, imebeba pia mataji mawili ya Kombe la Ligi na hivyo kuwafanya kushika namba nne kwenye orodha ya wakali wa Big Six waliopata mafanikio makubwa na kuwa bora uwanjani kwa kipindi cha miaka 15 iliyopita.

5. Arsenal - mataji 4

Arsenal wanashukuru ubingwa wao mara nne wa Kombe la FA imewafanya kuwa na nafasi ya kupata cha kuzungumza kwenye orodha ya timu bora za England kwa miaka 15 iliyopita. Arsenal inaamini pengine inaweza kupata cha kuzungumza chini ya kocha Mikel Arteta, lakini kwa rekodi zao za miaka 15 iliyopita, hawana kitu kingine cha kujivunia zaidi ya mafanikio yao kwenye Kombe la FA pekee.

6. Tottenham - taji 1

Kama kuna timu ambayo mashabiki wake wanapaswa kukaa kimya wakati wenzao watakapozungumzia timu bora basi ni wa Tottenham Hotspur. Katika kipindi cha miaka 15 iliyopita, timu hiyo imeshinda taji moja tu, tena Kombe la Ligi. Kocha Pochettino aliwahi kuinoa timu hiyo na katika muda ambao amekuwa na timu hiyo hakuwa na maajabu yoyote ya kuleta ubingwa.

Mara ya mwisho, Spurs kubeba ubingwa ilikuwa 2008 walipobeba Kombe la Ligi na tangu wakati huo hakuna taji jingine jambo linalomfanya kocha mpya Ange Postecoglou kuwa na maswali mengi ya kujibu juu ya kumaliza ukame wa mataji kwenye kikosi hicho cha London.

Chanzo: Mwanaspoti