Miaka 13 ya Jonas Mkude ndani ya Simba ilikuwa ni ya mafanikio, changamoto, furaha na panda shuka za hapa na pale.
Mkude ni zao la Simba B na ndiye mchezaji wa mwisho tutoka ndani ya timu hiyo baada ya wachezaji wenzake waliopandishwa mwaka mmoja kusambaratika na kwenda kujaribu maisha mengine nje ya Simba.
Nyota hao wengine, Ibrahim Ajibu, Said Ndemla, Edward Christopher, Abdallah Seseme na wengine, lakini kiungo huyo hakujumuishwa moja kwa moja kama wenzake.
Mkude ameanza kucheza kwenye timu ya vijana ywa Simba 2010, kabla ya 2011 kupandishwa timu ya wakubwa na kuwa msimu wa kwanza kwake katika Ligi Kuu Bara.
Tangu alipoingia Simba, Mkude, ambaye ni maarufu kwa jina la utani la 'Nungunungu', hakuwahi kutoka, licha ya misukosuko kadhaa aliyokumbana nayo wakati mwingine kutokana na mambo ya utovu wa nidhamu.
Katika miaka hiyo 13, Mkude, kuna wakati alikuwa nahodha wa kikosi hicho kabla ya kuvuliwa kitambaa akiwa kambi ya maandalizi ya msimu nchini Afrika Kusini.
Kiungo huyu mkabaji ametwaa mataji ya kujivunia ambayo kuna baadhi ya wachezaji waliodumu kwa muda mrefu kwenye vikosi vyao hawajawahi kutwaa.
Mchezaji huyu wa kimataifa wa Tanzania amebeba kila kitu ukiondoa taji la mashindano ya kimataifa (CAF) kwa ngazi ya klabu, lakini kwa hapa ndani kakomba kila kitu kuanzia Ligi Kuu Tanzania Bara, Kombe la Shirikisho (ASFC), Ngao ya Jamii, Kombe la Mapinduzi na mengineyo yaliyoibuliwa na kufa.
Rekodi zinaonyesha kuwa msimu wa kwanza wa kuichezea Simba, Mkude alibeba taji la Ligi Kuu Tanzania Bara, tena kwa kishindo, kwani alikuwepo kwenye kikosi kilichoinyoa Yanga mabao 5-0.
Kwa waliosahau, Mkude aliingia kipindi cha pili kumpokea kaka yake, Mwinyi Kazimoto, wakati vijana wa Jangwani wakipigwa kama ngoma na Wekundu wa Msimbazi waliokuwa chini ya mwenyekiti, Ismail Aden Rage.
Kisha akatwaa mengine manne mfululizo kuanzia msimu wa 2017/18, 2018/19, 2019/20 na 2020/21, pia amebeba Ngao ya Jamii mara nne, kuanzia 2012, 2018, 2019 na 2020, kabla ya Yanga kutibua misimu miwili mfululizo iliyopita.
Mkude pia alibeba ASFC mataji matatu ya msimu wa 2016/17, 2019/20 na 2020/21, kabla ya mataji hayo kuhamia Jangwani alkikosajiliwa, wakati kwa Kombe la Mapinduzi, mwamba kabeba mara tatu kati ya mataji manne iliyotwaa Simba.
Mkude katwaa nao 2011, 2015 na 2022, taji alilolikosa ni lile la 2008, kwani wakati huo alikuwa yupo Mwanza na huenda hakufikiria kama angekuja kuichezea Simba kwa mafanikio hayo.
Msimu ujao, Mkude atakuwa anavaa jezi ya njano na kijani akiitumikia timu ya mabingwa watetezi wa Ligi Kuu, Yanga kwa mkataba wa mwaka mmoja.
Lakini katika kikosi cha Yanga, Mkude anakutana na upinzani mzito katika eneo la kiungo, ambalo limekuwa silaha kubwa kwa miamba hiyo misimu miwili mfululizo.
KHALID AUCHO
Kiungo huyu raia wa Uganda ni miongoni mwa sajili bora katika eneo hilo aliyeleta uhai ndani ya kikosi hicho tangu aliposajiliwa.
Aucho akiwa katika majukumu yake hana papara zaidi ya kutumia akili na utulivu mkubwa katika miguu yake. Ana uwezo wa kucheza kama namba sita (kiungo wa ulinzi) ama namba nane (kiungo wa kuchezesha).
Nyota huyu kumuona kwa haraka mambo yake ndani ya uwanja inahitaji akili zaidi, kwani ni mtaalamu wa kutuliza timu, kuachia mpira kwa haraka na pia kucheza pasi za mwisho.
Huyo ni Aucho ambaye Mkude anakwenda kupambana naye kupata namba, staa huyu ameiheshimisha vilivyo jezi namba nane iliyokuwa ikivaliwa na Haruna Ninyonzima, kiungo fundi wa Rwanda aliyeacha historia nchini kwa kuzitumikia timu za Simba na Yanga kwa nyakati tofauti.
SALUM ABUBAKAR 'SURE BOY'
Licha ya jina lake kuwa kubwa katika soka la Tanzania, alitumia muda mrefu kukipiga Azam FC, lakini alitamani kucheza Jangwani kama ambavyo viongozi walivyokuwa wakiitamani huduma yake, lakini wakikwama.
Sure Boy, mtoto wa winga wa zamani wa Yanga, Abubakar Salum aliacha alama Azam FC na kutua kwake Yanga wengi walidhani huenda akakosa namba kutokana na ubora wa viungo waliokuwepo.
Lakini ubora na juhudi zake zimemfanya kupata namba chini ya kocha Nasreddine Nabi aliyemuamini na kumfanya kuonyesha kipaji chake.
Umahiri wake unawaumiza vichwa wengi juu ya ujio wa Mkude, lakini itakuwa neema kwa benchi la ufundi kupanga kikosi.
MUDATHIR YAHYA
Ni moja ya usajili bora ulioonyesha matunda katika msimu uliopita, kwani licha ya kukosekana kwa Feisal Salum 'Feitoto', Wanayanga hawakuwa na wasiwasi kutokana na uwezo wa mwamba huyu.
Mudathir kwa kutazama huwezi moja kwa moja kukiona kipaji chake, lakini anajua nini anakifanya awapo ndani ya dimba kwa wakati sahihi.
Na yeye ni zao la Azam FC, kutua kwake Yanga kulizidi kunogesha timu kutokana na nyota wanaocheza eneo hilo wote kuwa katika ubora.
ZAWADI MAUYA
Kijana asiyekata tamaa ya mapambano katika majukumu yake, ukimtizama kwa haraka unaweza kujua ni mchezaji wa kigeni, kumbe ni mzaliwa wa Tanzania, umahiri wake na utulivu unakushutua.
Moja ya usajili ulioleta matunda msimu wa 2021/22 kwa timu hiyo ya Yanga hadi kulitwaa taji kutoka kwa watani zao, Simba waliotamba nalo misimu minne mfululizo.
Mkude anakwenda kupambana kupata namba na kiungo huyu mwenye utulivu wa hali ya juu.
YANICK BANGALA
Ni kiungo ambaye alikuwa mchezaji bora wa msimu (MVP), msimu uliopita, akiitumikia Yanga vyema kwenye eneo la kiungo mkabaji chini ya kocha Nabi, ambaye alimtumia katika maeneo mawili tofauti.
Msimu ulioisha, Bangala alitumika zaidi eneo la beki wa kati akicheza sambamba na Bakari Mwamnyeto na wakati mwingine Dickson Job, alimudu kucheza vyema pia kwenye nafasi hiyo pamoja na kupoteza tuzo yake aliyotwaa msimu wake wa kwanza kucheza Yanga.
Mchezaji wa zamani ambaye kwa sasa ni kocha, Kenny Mwaisabula anabainisha kuwa kila mchezaji anayesajiliwa katika timu fulani anakuwa na uhitaji na ndiyo sababu za uongozi kufanya hivyo.
Mwaisabula, ambaye ni maarufu kama 'Mzazi', ana imani kubwa na Mkude kutokana na uwezo wake lakini anachotakiwa ni kupambana ili kumshawishi kocha amuamini tofauti na aliowakuta licha na wao kuwa wazuri kama yeye.