Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

USAJILI: Tambwe, Kamusoko wavunja ukimya Yanga

59919 Pic+tambwe

Tue, 28 May 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Wachezaji nyota wa kigeni wa Yanga, Amissi Tambwe na Thabani Kamusoko, wamezungumzia hatima zao ndani ya klabu hiyo kongwe nchini.

Akizungumza Dar es Salaam jana, Tambwe alisema ataikumbuka Yanga kwa namna ilivyompokea baada ya kutemwa na Simba msimu 2013/2014.

Nyota huyo alisema baada ya kuachwa na Simba alikuwa katika kipindi kigumu, lakini Yanga ilimuokoa kwa kuwa iliamini ana kiwango bora.

Tambwe alisema Yanga ilithamini mchango wake tangu siku ya kwanza na hawezi kuisahau hata kama ataachwa katika usajili na Kocha Mwinyi Zahera.

Kauli ya Tambwe na Kamusoko, zimekuja baada ya kuibuka taarifa kuwa hawataongezwa mkataba kwa ajili ya msimu ujao, baada ya mikataba yao kumalizika.

“Sijazungumza na uongozi kuongeza mkataba mpya, lakini nimepokea ofa nyingi hata nikiondoka Yanga popote nitakapokuwa nitaikumbuka timu hii.

Pia Soma

“Nilipotoka Simba, Yanga ilinipokea vizuri imenilea kisoka, mashabiki, wachezaji na viongozi walinipa ushirikiano mkubwa nitaikumbuka hata ikitokea nimeondoka Yanga,” alisisitiza Tambwe.

Kamusoko, nahodha wa zamani wa Platnum ya Zimbabwe, alisema ataendelea kuiheshimu Yanga kwa kuwa wasifu wake katika soka umechangiwa na Yanga.

“Nimejiunga na Yanga nikiwa sijawahi kupata taji hata moja la ligi japo nilikuwa na nafasi ya kucheza katika timu kubwa na nilikuwa na uwezo, hivyo kitu pekee ambacho nitakuwa nakikumbuka Tanzania ni historia niliyoweka na upendo wa mashabiki na viongozi,”alisema Kamusoko.

Kiungo huyo ambaye yuko Zimbabwe akiitumikia timu ya Taifa, alisema Yanga ni klabu kubwa ambayo imemtangaza katika soka.

Kamusoko alisema ingawa yuko Zimbabwe anawakumbuka marafiki zake aliowafahamu kupitia Yanga na mashabiki.

Akizungumza jana, Zahera alisema wachezaji wa kigeni walikuwa na msaada msimu huu akiwemo Tambwe na Kamusoko ambaye licha ya kuanzia benchi, alisema alikuwa akifanya vyema.

Kocha huyo alisema Tambwe na Kamusoko ni wachezaji wa Yanga na uamuzi wa kutangaza majina ya wachezaji watakaoachwa atatangaza baada ya kumalizika mechi yao na Azam kesho itakayochezwa kwenye Uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam.

Mchezaji wa kigeni raia wa DR Congo Papy Tshishimbi ndiye mchezaji pekee wa kigeni aliyetia saini mkataba mpya Yanga. Yanga ipo nafasi ya pili katika Ligi Kuu ikiwa na pointi 86.

Chanzo: mwananchi.co.tz