Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

TV

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

UDOM kama Ufaransa tu, kunguni tishio!

Hofu Ya Uvamizi Wa Kunguni Yaongezeka Kabla Ya Olimpiki Ya 2024 UDOM kama Ufaransa tu, kunguni tishio!

Wed, 18 Oct 2023 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Wakati wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM) wakilalamikia changamoto ya uwepo wa kunguni chuoni hapo, uongozi wa chuo hicho umewataka kuzingatia usafi kama njia ya kukabiliana na wadudu hao.

Kauli hiyo imekuja baada ya mitandao ya jamii kusambaza habari ya uwepo wa changamoto ya kunguni kwenye chuo hicho jambo ambalo limewafanya baadhi ya wanafunzi kulala chini.

Suala kama hilo limejitokeza pia nchini Ufaransa ambapo Serikali imelazimika kufunga shule ili kukabiliana na changamoto hiyo.

Mkurugenzi wa Mawasiliano na Masoko wa Udom, Rose Joseph ameiambia Mwananchi Digital jana Oktoba17, 2023 kuwa, kuwepo au kutokuwepo kwa wadudu hao chuoni hapo, si sababu ya kuwa mjadala mitandaoni.

“Ukweli ni kwamba kunguni ni mdudu ambaye yuko kwenye shule, vyuo na sio kwa Chuo Kikuu cha Dodoma (Udom). Itakuwa ni ajabu na kushangaza chuo kikubwa chenye karibia watoto 33,000 kikose kunguni,” amesema.

Rose amesema kwa kutambua kuwa kuna uwezekano wa kuwa na wadudu ikiwemo kunguni chuoni hapo, uongozi umekuwa na utaratibu wa kupulizia dawa, kila mara hasa wanafunzi wanapokuwa likizo.

Amesema wameanza zoezi la kupulizia dawa tangu Oktoba Mosi mwaka huu katika mabweni ya wanafunzi kama maandalizi ya kuwapokea wanafunzi wapya wa mwaka wa kwanza Oktoba 28 mwaka huu.

Amesema shughuli hiyo inafanyika kwa kuzingatia utaalamu wa upulizaji dawa kwenye maeneo yote ambayo ni maficho ya wadudu, masalia ya mayai ya kunguni na wanapohifadhi vitu mbalimbali ambako kunaweza kusababisha wadudu hao kuhama kutoka sehemu moja kwenda jingine.

“Suala la kujiuliza kitu gani kinasababisha kunguni kuwepo? Jibu ni uchafu. Na baadhi ya wanafunzi wanarudi na kunguni shuleni kwa hiyo matokeo yake baada ya muda mfupi linakuwa ni tatizo ambalo haliishi,” amesema.

Rose amesema changamoto kubwa inayokuja kutokana na suala la usafi wa vyumba vya wanafunzi kubakia mikononi mwao, tofauti na maeneo mengine ambako shughuli hiyo huwa mikononi mwa makampuni yaliyopewa zabuni ya kuendesha usafi chuoni hapo.

Amesema suala la usafi ni kati ya chuo, mwanafunzi na mlezi kwa kuona umuhimu wa suala la usafi na kwamba changamoto kubwa ya wadudu hao inaonekana kwenye mabweni ya watoto wa kiume.

Rose amesema shughuli ya kupulizia dawa ya kuuwa wadudu hufanywa na chuo mara mbili kwa mwaka ambapo hutumia zaidi ya Sh30 milioni.

Amesema kwa kawaida hatua zinazochukuliwa baada ya wanafunzi kuripoti uwepo wa wadudu hao kwenye vyumba vyao ni kuweka dawa ambazo hazina madhara, kuanika magodoro katika jua kali na kumwaga maji ya moto kwenye vyumba husika.

Wanafunzi wazungumza

Naye Mwanafunzi wa mwaka wa pili wa shahada ya Elimu kwenye chuo hicho, Janeth Bujeje amesema tatizo la kunguni haliko katika chuo hicho tu bali katika shule nyingi za mabweni nchini.

Amesema hatua wanazochukua ni kupambana nao kwa kupuliza dawa zisizo na madhara kwa binadamu, kufanya usafi kwasababu wadudu hao hukaa mahali pachafu.

“Suala la kunguni liko katika suala binafsi, kuhakikisha kuwa wanaishi katika mahali pasafi. Pengine wanafunzi wanachelea kufanya usafi na hivyo kunguni wanazaliana,” amesema.

Janeth amesema suala la kunguni limekuwa likiwakosesha kujiamini, likiwaboa kwasababu mara nyingine unakwenda kujisomea unaambiwa kuwa unakunguni katika nguo yako.

Amewataka wanafunzi wenzake kuamka na kuona kuwa uwepo wa kunguni katika mabweni yao si kitu cha kawaida na hivyo wajikite kwenye usafi wa binafsi ili kuepukana na tatizo hilo.

Naye Mwanafunzi mwaka wa pili wa shahada ya Elimu ya Watu Wazima na Jamii katika chuo hicho, Jairos Michael amesema jambo hilo amelikuta alipoingia kwenye chuo hicho na limeendelea kuwepo hadi hivi sasa.

“Tujitahidi kuendelea na jitihada za kukomesha tatizo hili lakini hata kwa chuo isiwe suala la kupuliza dawa ya kuwaua kunguni wakati wa likizo tu, bali hata wakati mwingine wapulize dawa ili kupunguza athari za wadudu hao ambao wamekuwa wakileta usumbufu,” amesema.

Amesema wadudu hao wamekuwa wakisababisha usumbufu wakati wa usiku na hivyo kutolala kutokana na maumivu wanayoyapata baada ya kuumwa na wadudu hao.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live