Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

UBISHI WA MZEE WA KALIUA: Yanga inakwenda au inarudi nyuma

Yangasc?fit=600%2C406&ssl=1 Kikosi cha Yanga kikijifua

Thu, 16 Sep 2021 Chanzo: www.mwanaspoti.co.tz

THE Return of Champions! Hii ndiyo ilikuwa kauli mbiu ya mabingwa mara 27 wa Ligi Kuu Bara kuelekea mchezo wa kwanza nyumbani wa Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Rivers United ya Nigeria.

The Return of Champions imegeuka na kuwa The Return of Aibu. Mabingwa mara 27 wa nchi wanafungwa nyumbani kirahisi na timu ndogo kutoka Nigeria. Hivi Yanga inakwenda kweli mbele au inarudi nyuma? Naomba maoni yako kupitia namba yangu ya simu hapo juu. Ukitazama ukuta wa Yanga unamuona Dikson Job na Bakari Mwamnyeto huku Yannick Bangala akiwa benchi. Inafikirisha kidogo. Nilidhani Yanga wamemsajili Bangala ili kuja kutatua changamoto ya upigaji vichwa pale nyuma.

Nilidhani Yanga wamemsajili ili kuleta ukomavu wa Ligi ya Mabingwa Afrika pale nyuma. Kumbe Kocha Nabi anafurahia tu kumuona Bangala akiwa benchi. Aisee! Hii ilinishangaza sana. Ukifa baharini kwa kiu Waswahili wanasema huo ni Uzembe.

Yanga wamekuwa na matatizo yaleyale ya kufungwa mipira ya juu lakini hakuna lolote linalofanyika kutatua changamoto hiyo.

Waliwahi kufungwa bao kama la juzi na Joash Onyango kwenye Kariakoo Derby. Waliwahi kufungwa tena bao kama la juzi na Tadeo Lwanga kwenye fainali ya FA Kigoma.

Mechi yao dhidi ya Zanaco ya Wiki ya Mwananchi walifungwa pia mipira ileile ya juu. Rivers United nao wanawafunga palepale Kwa Mkapa kwa staili ileile. Hivi ni kweli Yanga inakwenda mbele au inarudi nyuma? Naomba maoni yako kupitia namba yangu ya simu hapo juu. Moja kati ya sababu zitakazoifanya kuendelea kuwa timu kubwa ni kufanya vizuri kwenye ligi za kikubwa na kushinda mataji.

Yanga lazima warudi kwenye zama zao za kuitafuta hatua ya makundi kwenye michuano ya Afrika. Yanga lazima warudi kwenye zama za kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu Bara. Yanga haiwezi kuendelea kuwa timu kubwa nchini kwa kufungwa na timu kama Rivers United.

Yanga haiwezi kuendelea kuwa timu kubwa kwa kukosa ubingwa msimu wa tano mfululizo. Kuna kitu lazima kiwekwe sawa. Ukiwatazama uwanjani dhidi ya Rivers United unashangaa kwa nini Said Ntibazonkiza alichelewa kuingia uwanjani. Ile ilikuwa mechi yenye mipira mingi sana ya kutenga. Ukitazama kikosi cha Yanga unamuona mtu mmoja mzuri wa kupiga mipira hiyo, Ntibazonkiza.

Huyu walau amewahi kupiga mipira hiyo mara nyingi na kufunga. Alistahili kuingia mapema. Jesus Moloko huenda ni mchezaji mzuri, lakini mpira ukimkataa basi mapema tu amuachie nafasi Deus Kaseke. Kufungwa nyumbani dhidi ya timu ya kawaida tu kutoka Nigeria, sio dalili nzuri kwa Yanga. Hii sio namna sahihi ya The Return of Champions. Mabingwa huwa hawarudi kizembe namna hii ni The Return of Aibu!

Msimu wa 2020/21, Rivers United walimaliza nafasi ya sita ndani ya Ligi Kuu nchini Nigeria. Baada ya hapo timu moja inayojulikana kama Jigawa Golden Stars ilinyang’anywa alama tatu kwa kumtumia mchezaji mmoja kinyume na kanuni na alama hizo wakapewa Rivers United na mabao matatu mezani na kuwafanya wafuzu michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika.

Ukitazama njia yao ya kufika kwenye michuano hii unasikitika kuona Yanga inafungwa nyumbani. Rivers ni timu ndogo tu pale Nigeria. Hawana historia yoyote ya kutisha. Hawana mafanikio yoyote ya kuitisha Yanga. Bado nafasi ipo kwa Yanga, lakini inabidi akili kubwa kwenda kupindua matokeo ugenini. Kwa aina ya wachezaji waliopo Yanga wanatosha kabisa kwenda kuwapa matokeo.

Nabi anapaswa kuwa shujaa kwenye mechi hiyo. Watu wa kazi ni lazima waanze kikosini na wakapambane hasa. Mpira wa Afrika ni kila mtu ashinde nyumbani kwao. Kitendo cha Yanga kufungwa nyumbani ni kosa kubwa mno kwenye mpira wetu.

Huyu Djigui Diarra labda ana uwezo mkubwa wa kudaka RISASI kuliko mipira inayolenga lango. Naona kwa muda mfupi tu - mabao yanaingia.Bado hakuna chochote cha kumsifia, labda ni mapema sana. Labda atatuonyesha namna anavyoweza kudaka mishale hapo baadaye, lakini hadi sasa hana utofauti wowote na walioondoka.

Kama kuna mtu kiti kimeanza kuwaka moto, basi ni Nabi. Mechi mbili zilizopo mbele yake zinaweza kumgharimu - mechi ya marejeano na Rivers United ugenini na ile ya Ngao ya Jamii dhidi ya Simba. Akifungwa mechi zote sioni maisha yake pale Jangwani. Kama kuna jambo anapaswa kulipigania ni kutofungwa mechi hizo pamoja na kuwa Yanga bado wanajenga timu, lakini sio kwa kutolewa hatua za awali za michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika.

Pamoja na kuwa Yanga wanajenga timu lakini sio kwa kufungwa na Simba mfululizo. Kuna mitihani miwili kwa Nabi. Kuibakiza Yanga kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika au kuifunga Simba Septemba 25.

Tofauti na hapo, sioni kama mabosi wa Yanga watakuwa tayari kumvumilia. Kwa usajili walioufanya siwaoni kama watakuwa wavumilivu sana.

Wanataka kurejesha furaha ya Wanayanga. Wanataka kurejesha ufalme wao ambao kwa sasa uko Msimbazi. Bado naiona nafasi ya Yanga kushinda ugenini na kusonga mbele dhidi ya Rivers United, lakini kama Nabi ataamua.

Kwa nilichokiona wikendi iliyopita Kwa Mkapa haikuwa Return of Champions ilikuwa ni The Return of Aibu!

Chanzo: www.mwanaspoti.co.tz