Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Twiga Stars ilibugi hapa kwa Banyana Banyana

Twiga Vs Banyana Twiga Stars ilibugi hapa kwa Banyana Banyana

Thu, 29 Feb 2024 Chanzo: Mwanaspoti

Timu ya taifa ya wanawake ‘Twiga Stars’ imeondoshwa juzi na timu ya taifa ya Afrika Kusini 'Banyana Banyana' kwenye mashindano ya kufuzu ushiriki wa Michezo ya Olimpiki inayotarajiwa kufanyika mwakani nchini Ufaransa kwa jumla ya mabao 4-0.

Twiga ilianza kupoteza mchezo wa kwanza nyumbani kwa mabao 3-0 kisha kuruhusu bao 1-0 ugenini, mabao yaliyozima matumaini ya kikosi hicho kushiriki kwenye Michezo ya Olimpiki 2025.

Afrika Kusini sasa itakutana na Nigeria kwenye raundi ya nne na ikiitoa timu hiyo itakuwa kati ya timu mbili zitakazojikatia tiketi ya kushiriki mashindano hayo.

Mwanaspoti imekuchambulia baadhi ya mambo yaliyoiangusha Twiga Stars kutofuzu Olimpiki.

UBORA WA WASAUZI

Miaka ya hivi karibuni kikosi cha Twiga kimeleta ushindani kwa timu za Afrika hasa Mashariki kutokana na soka la Tanzania kukua siku hadi siku.

Kitendo cha Afrika Kusini kilichocheza Kombe la Dunia hatua ya 16 bora mwaka jana kuitoa Twiga kwa jumla ya mabao 4-0 ni maendeleo makubwa ya timu hiyo.

Ukiangalia njia iliyopita Twiga kuanzia hatua ya kwanza mpaka raundi ya tatu ilipoishia haikuwa na ugumu kutokana na raundi ya kwanza kupita kwa Congo Brazzaville kujitoa kisha raundi ya pili kuwatoa Botswana kwa mabao 3-0 na hii ambayo walianza na kichapo nyumbani.

Ubora walioonyesha Afrika Kusini kuanzia mechi ya kwanza ugenini Azam Complex, Chamazi uliipa ugumu Twiga Stars kusonga mbele kwani hawakuwaruhusu kufika golini kwao na kuimaliza mechi mapema kabla ya marudiano ambayo Twiga nayo ilionyesha ushindani ugenini kwa kuingia na mpango wa kuzuia.

WACHEZAJI WA NJE

Wachezaji 12 kati ya 24 (sawa na asilimia 50) ya walioitwa kwenye kikosi cha Banyana Banyana wanacheza nje ya nchi na wamekuwa wakifanya vizuri na kupata namba kwenye timu zao, Thembi Kgatlana aliyewasumbua mabeki wa Stars na kufunga mabao mawili anakipiga katika klabu ya Tigres UANL ya Mexico na Linda Motlhalo anakiwasha huko Racing Louisville, USA.

Wapo wengi ambao wanacheza nje na wamekuwa msaada kwenye timu ya Banyana kutokana na uzoefu wanaopata kutoka kwenye timu zao tofauti na Twiga ambao kuna upungufu.

Katika kikosi cha wachezaji 24 walioitwa kwenye kikosi cha Twiga Stars, wanne wanacheza soka la kulipwa nje ya nchi na hawakuwa wakipata nafasi mara kwa mara kutokana na ushindani uliopo.

Wachezaji wanne wanaocheza nje ni Enekia Lunyamila anayeichezea (Eastern Flames, Saudia) ndio amekuwa akipata nafasi ya kikosi cha kwanza na ni tegemeo tofauti na Opah Clement (Besiktas ya Uturuki), Julietha Singano (Juarez, Mexico) na Diana Msewa (Ama S.F.K, Uturuki) ambao wamekuwa wakipata mara moja.

KUTOJUANA

Mara ya mwisho timu hizo kukutana ilikuwa kwenye mashindano ya All Africa Games mwaka 2011 na timu hizo mbili zilizotoka sare ya 2-2.

Huenda kutofahamiana kimbinu kwa timu hizo kulisababisha Twiga kutolewa kwani katika mechi ya kwanza Stars ilifungwa nyumbani mabao 3-0 na juzi ugenini bao 1-0 lakini ilibadilika na kucheza kwa nidhamu ya juu.

Kipindi kirefu kimepita tangu Twiga icheze na Banyana na kama ingekutana nayo miaka ya hivi karibuni pengine isingefungwa idadi kubwa hivyo ya mabao kutokana na ubora wa wachezaji wa Stars na uzoefu walioupata kwenye mashindano mbalimbali.

Kuna wachezaji wa Afrika Kusini kama Jermaine Seoposenwe na Kgatlana ambao walikuwapo tangu kwenye mechi ya All Africa Games mwaka 2011 na mashindano haya wote walikuwepo kwenye kikosi hicho na ndio ambao kwa asilimia kubwa waliisumbua safu ya ulinzi ya Stars.

WASIKIE WENYEWE

Kocha wa Twiga, Bakari Shime anasema kuna tofauti kubwa ya kucheza kuanzia mchezo wa kwanza na wa pili ambao walicheza vizuri na wataangalia udhaifu wao na wataurekebisha ili kujiandaa na michezo mingine.

“Tuna nafasi ya kufanya vizuri kwenye mashindano mengine, tumetolewa lakini tumefaidika na inaweza kuwa chagizo kwetu kwa ajili ya mashindano ya WAFCON ambayo Twiga imeshiriki,” anasema Shime.

Kiungo wa Stars, Amina Ally anasema kama wachezaji walipambana ili kuhakikisha wanashinda na kufuzu lakini bahati haikuwa yao Afrika Kusini walifunga bao na kuwatoa.

“Watanzania wamekuja kwa wingi kutusapoti hasa wanaoishi hapa Afrika Kusini, wachezaji tulipambana vilivyo ili kushinda lakini bahati haikuwa yetu tumetolewa na tunaamini tutafanya vizuri kwenye michuano inayokuja,” alisema Amina.

Chanzo: Mwanaspoti