Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Twende kazi! ni mwendo wa hesabu za vidole huko Qatar

Uruguay Striker Darwin Nunez Mshambuliaji wa Uruguay, Darwin Nunez

Thu, 1 Dec 2022 Chanzo: Mwanaspoti

Ni mwendo wa hesabu za vidole, huyu afungwe na yule ashinde Mbili Bila. Hicho ndicho kinachoendelea kwa sasa kwenye mchakamchaka wa kusaka tiketi ya kutinga hatua ya 16 bora kwenye fainali za Kombe la Dunia 2022 kwa Kundi E na F.

Kundi E, kuna vita ya Hispania, Japan, Costa Rica na Ujerumani - kila moja inaomba mabaya kwa mwenzake.

Shughuli ni pevu. Kundi F kuna Canada, Morocco, Croatia na Ubelgiji, hapatoshi. Mwendo ni uleule, kupigiana hesabu za vidole; tushinde wafungwe. Hapo ndipo utamu wa fainali za Kombe la Dunia 2022 huko Qatar ulipofikia.

Kwenye Kundi E, msimamo unaosomeka; Hispania inaongoza kwa kuwa na pointi nne, ikifuatiwa na Japan yenye pointi tatu sawa na Costa Rica, huku Ujerumani ikishika mkia na pointi yao moja. Na mechi zao za mwisho kwenye kundi hilo zitakazopigwa leo Alhamisi, Costa Rica itakipiga na Ujerumani na Japan watacheza na Hispania.

Majaliwa ya Ujerumani kutinga hatua ya mtoano ni kuichapa Costa Rica, huku wakiombea Hispania iifunge Japan. Ugumu wa kundi hilo ni kwamba timu zote zina nafasi ya kusonga mbele. Hispania licha ya kuwa na pointi 4 bado haipo salama, kama itachapwa na Japan kisha Costa Rica ikaifunga Ujerumani. Sare kwenye mechi zote za kundi hilo zitatoa faida kwa Hispania na Japan kusonga mbele. Shida inayowakabili Ujerumani wao ni lazima washinde, wakati wenzao kwenye vita hiyo, Hispania, Costa Rica na Japan zinaweza kufuzu kwa matokeo ya sare tu. Nani atatoboa?

Rekodi zinaonyesha kwamba Costa Rica na Ujerumani zimewahi kukutana kwenye fainali za Kombe la Dunia, hiyo ilikuwa Ujerumani 2006, ambapo wenyeji walishinda kwa mabao 4-2 kwenye mechi ya Kundi A. Itakuwaje huko Qatar?

Hispania na Japan nazo zimeshakutana mara moja, kwenye mchezo wa kirafiki mwaka 2001, La Roja ilishinda 1-0.

Shughuli nyingine ipo kwenye Kundi F. Msimamo ulivyo, Croatia inaongoza kwa kuwa na pointi nne, sawa na Morocco kwenye nafasi ya pili na kufuatia Ubelgiji kwenye nafasi ya tatu na pointi zao tatu, huku Canada wao wameshatupwa nje baada ya kuwa na pointi 0, wakipoteza mechi zote mbili za kwanza kwenye hatua hiyo ya makundi. Kwa maana hiyo kuna timu tatu; Croatia, Morocco na Ubelgiji zikigombea nafasi mbili za kutinga hatua ya 16 bora.

Utamu unakuja kwamba Croatia na Ubelgiji watamalizana wenyewe, wakati Morocco wao watakipiga na Canada. Morocco inahitaji sare tu kusonga mbele bila ya kujali matokeo ya mechi nyingine. Ubelgiji wao kutinga hatua ya 16 bora hawahitaji matokeo mengine zaidi ya ushindi, kinyume cha hapo itakuwa na faida kubwa kwa Croatia. Matokeo ya sare kwa mechi zote yatakuwa na faida kwa Croatia na Morocco. Kipigo kwa Ubelgiji kitatoa fursa zaidi kwa Morocco hata kama watapoteza.

Ni mambo ya hesabu tu. Morocco na Canada zimeshawahi kukutana kwenye mechi ya kirafiki, 2016 - ambapo wawakilishi hao wa Afrika waliibuka na ushindi wa mabao 4-0. Croatia na Ubelgiji zimekutana mara nyingi, kwenye mechi za michuano tofauti - na mchezo wa mwisho ulikuwa wa kirafiki, 2021 ambapo chama la Ubelgiji lenye mastaa wa maana kama Kevin De Bruyne liliibuka na ushindi wa bao 1-0. Lakini, safari hii ni vita ya kubaki kwenye Kombe la Dunia, patachimbika.

Chanzo: Mwanaspoti