Sidhani kama huu mjadala wa wachezaji wa kigeni na wale wazawa unaweza kuisha kutokana na utamaduni wetu wa kupenda kubishana bila kufikia muafaka hata kama jambo lina umuhimu na maana kubwa.
Naamini baada ya mijadala iliyopita juu ya namba ya wachezaji wa kigeni, msimu ujao itaibuka tena na hakutakuwa na suluhisho zaidi ya kila mmoja kuendelea kuvutia upande anaouona ni sahihi na una manufaa kwake.
Lakini pia sio mbaya kwa vile mchezo wa soka ni wa maoni na hiyo mijadala inaweza kutusaidia kujenga kwa namna fulani ingawa pia inaweza isitujenge.
Hata hivyo kinachotusikitisha kijiweni ni kwamba mijadala hii imekuwa ikigusa upande wa wachezaji tu lakini kwenye upande wa makocha wala huwa haifiki.
Tunaona kama hakuna haja ya kujadili namba ya makocha wa kigeni na kizawa labda kwa vile huko hatua maslahi nako lakini kiuhalisia ndiko kwenye hatari zaidi pengine kuliko hata upande huu ambako tunararuana kila ifikapo leo.
Kadri miaka inavyozidi kusonga mbele, namba ya makocha wetu wa kizawa inazidi kupungua kwenye ligi kuu na kwa bahati mbaya sasa hadi ligi ya Championship nayo, timu shiriki zimeanza kutazama makocha wa kigeni na kuwachukua ili wazifundishe.
Mfano katika msimu uliomalizika, kati ya timu 16, timu saba ambazo zinakaribia nusu ya zote zilizopo kwenye ligi, zilikuwa zinafundishwa na makocha wa kigeni wakati msimu unamalizika.
Na Kwa bahati mbaya, timu kubwa za Yanga, Simba na Azam ambazo ndio zimekuwa zikishiriki mara kwa mara mashindano ya kimataifa, hazikuwa zikiongozwa na makocha wazawa.
Hii ina athari kwa taifa kwani inapunguza wigo na uwezekano wa kupata kocha wa kufundisha timu zetu za taifa za soka lakini pia wanashindwa kuimarika kwa kukosa uzoefu wa michezo migumu ya kiushindani katika ngazi ya kimataifa.
Wale wazalendo mnaopigania idadi ya wachezaji wa kigeni ipungue tunategemea kuwaona mnapambana pia kulinda nafasi za makocha wetu wazawa kwani wana umuhimu