Kocha wa timu ya soka ya taifa, Taifa Stars, Kim Poulsen, amesema amefungwa na timu yenye uzoefu lakini ana matumaini ya kufanya vizuri katika mchezo wa marejeano nchini Benin kesho.
Stars ilifungwa bao 1-0 na Benin juzi katika mechi za Kundi J kuwania kufuzu kombe la dunia Qatar 2022.
Matokeo hayo yameifanya Stars kuporomoka mpaka nafasi ya tatu kwenye msimamo wa kundi lake ikiwa na pointi nne, ikiongozwa na Benin yenye pointi saba, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo ikiwa na pointi tano katika nafasi ya pili na Madagascar ikiwa mkiani bila pointi.
Akizungumza na waandishi wa habari juzi, Poulsen amesema unapocheza michezo ya kutafuta kufuzu fainali za kombe la dunia unakutana na timu kubwa hivyo kuna milima na mabonde unakutana nayo.
“Tumejisikia vibaya baada ya kupoteza mchezo huu sababu tumecheza vizuri lakini Benin walikuwa na bahati, nina matumaini makubwa kwa baadhi ya wachezaji naamini tutaenda kufanya vizuri nchini Benin…
“Tulitengeneza nafasi nyingi lakini tumeshindwa kutumia kipindi cha kwanza, Simon Msuva, alipata nafasi nzuri akashindwa kuitumia nafikiri Benin wameondoka hapa wakiwa na furaha kwa kuondoka na ushindi wa bao 1-0.”
“Kipindi cha pili tulijaribu kuongeza nguvu nafikiri kila mtu alikuwa na hisia kuwa muda wowote Tanzania itapata bao, tulitengeneza nafasi lakini tukapoteza mwisho tukaadhibiwa na uwezo binafsi wa namba tisa, Mounie nafikiri ndiyo nafasi pekee ambayo Benin waliitengeneza kipindi cha pili,” amesema Poulsen.
Tayari Stars ipo Benin baada ya kuondoka jana mchana kwa ajili ya mechi hiyo inayotarajiwa kuchezwa kesho kwenye mji wa Porto Novo.