Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Tusizikubali ligi za mchongo

Uwanja Wa Jamhuru Moro Tusizikubali ligi za mchongo

Sat, 13 May 2023 Chanzo: Mwanaspoti

Miaka miwili tu imebaki kabla ya kufanyika kwa Uchaguzi Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambao tutachagua Rais, Wabunge na Madiwani wa kutuongoza hadi mwaka 2030.

Kipindi kama hiki cha kukaribia uchaguzi, wale ndugu zetu ambao wamekuwa na nia ya kugombea ubunge na udiwani, utawaona wanajiweka karibu sana na sisi wananchi katika shughuli mbalimbali.

Usidhani kama ukaribu huo utakuwa wa kudumu. Ni urafiki wa kutaka kutushawishi tu tuwapeleke kule mjengoni makao makuu au kwenye mabaraza ya halmashauri wapige hela.

Hivyo kwa fedha wanazopata kule unadhani watakubali kirahisi kukosa kura za kuwahakikishia kuitwa waheshimiwa? Hapana hawawezi kukubali kirahisi na wako tayari kujiweka sana karibu na sisi ili tuwape tu kura zetu.

Ukaribu wao wa sasa na sisi ni kama unapocheza mchezo wa draft na mtu. Ukiona anasukuma kete kukupa ili ule, ujue atakupiga tatu (tutusa) hadi anaingia king na hivyo kumuweka katika nafasi nzuri ya kushinda mechi hiyo.

Sasa mahali ambako jamaa wamekuwa wakipatumia sana kulainisha mipango yao ya kwenda mjengoni au kuwa mabosi wa kata ni huku kwenye michezo hasa soka.

Basi nyakati kama hizi watajifanya ndio wao wana uchungu sana na michezo kwenye hii nchi, watatafuta mipira yao 20 watagawa mmojammoja kwa kila kata halafu baada ya hapo watatoa seti moja ya jezi kwa kila kata kisha wataanzisha ligi za kata na kutoa kauli nyingi za kuonyesha wana mikakati ya kuhakikisha sekta ya michezo inapiga hatua.

Na kwa vile wameshatuzoea, wanajua fika tutawasapoti na baadaye kuwapigia kura. Lakini kiuhalisia, hawana nia ya dhati ya kuhakikisha mchezo wa soka na mingine inapiga hatua zaidi ya kujenga ushawishi tu kwa wapiga kura.

Emu tujiulize, mmoja kwa kata unawezaje kuleta maendeleo ya soka kwenye kata? Kata ambayo ina vijiji zaidi ya vitano inawezaje kutumia mpira mmoja na ikaibua vipaji vya vijana? Jezi seti moja itatumiwa na timu ngapi kwenye kata?

Kuanzia sasa inabidi tuanze kuzikataa ligi zao na tuwaambie ukweli kuwa hazisaidii lolote kwenye kata au majimbo zaidi zipo kwa ajili ya kuwanufaisha wagombea binafsi.

Hawa watu wangekuwa na uchungu na sekta ya michezo, tungewaona wakiwa mstari wa mbele kulinda viwanja na maeneo ya wazi ambayo hutumiwa kwa shughuli ya michezo yasiuzwe na kujengwa yadi za magari au majengo makubwa ya biashara.

Wangekuwa na uchungu na michezo, wangepambana kuhakikisha Tanzania inakuwa na vituo vya soka na vyote vinakuwa na bajeti kutoka serikalini.

Hivi vyote hawafanyi matokeo yake wanaleta ligi za kugombea jezi seti tatu na mipira kwa kata nzima au jimbo, itasaidia nini?

Tuwakatae na ligi zao pengine itasaidia kuwakumbusha wajibu wao kwetu michezoni.

Chanzo: Mwanaspoti