Zama zinakuja na kupita. Kila nyakati zina ubora na ubaya wake, lakini ni vyema tukakumbuka mema zaidi.
Ni kama zama za makipa nchini zinavyokuja na kupita. Tangu miaka hiyo Tanzania imekuwa ikibarikiwa makipa wengi mahiri. Wengi walikuja nyakati zao na kupita. Tangu enzi za kina Omar Mahadh, Athuman Mambosasa, Juma Pondamali ‘Mensah’, Idd Pazi ‘Father’, Mohamed Mwameja, Hamis Kinye, Joseph Fungo, Steven Nemes, Riffat Said na wengineo. Zikaja enzi za kina Peter Manyika, Ivo Mapunda, Juma Kaseja na wengine.
Mwishoni wakaja hawa kina Ally Mustapha ‘Barthez’, Deo Munishi ‘Dida’, Ali Mwadini na sasa tuna Aishi Manula. Ndiyo zama zilivyo. Mambo mazuri huja na kupita. Kila mmoja aliacha alama katika zama zake. Ndio sababu hadi leo bado kuna mjadala juu ya nani ni kipa bora zaidi kuwahi kutokea katika historia ya Tanzania.
Kila mmoja ana maoni yake kutokana na zama alizoishi. Walioishi miaka hiyo watakwambia Mambosasa ni bora kuliko Kaseja, ila wapo ambao watasema tofauti. Watasema Kaseja alikuwa mahiri zaidi. Kila mmoja anasema alichokiona.
Ukweli ni kwamba Mambosasa wakati wake alikuwa kipa mahiri kweli. Alitetemesha nchi. Waliobahatika kuhudhuria katika viwanja ya soka nyakati hizo watasema hilo. Na ndiyo ukweli.
Ukimuuliza Sunday Manara, Abdallah Kibadeni na wengineo watakuelezea ubora wa Mambosasai. Ambao hawakubahatika kuwepo watabaki kusikiliza simulizi hizi. Lakini waliomuona Pondamali watakwambia hakuna kipa mahiri kama yeye. Huyu alikuwepo kwenye kikosi cha Taifa Stars kilichokwenda Afcon 1980. Alikuwa hodari kweli.
Katika zama zake, Pondamali alifanya kila alichojisikia. Angeweza kudaka mpira na kumpiga nao mshambuliaji kisha akaudaka tena. Wakati fulani aliwahi kufanya hivyo na mambo nusura yamuendee mrama. Kuna tukio aliwahi kufanya Shamba la Bibi, sasa Uwanja wa Uhuru kwa kufanya mbwembwe kwenye mechi ya Yanga dhidi ya African Sports, timu yake ikiwa mbele kwa bao 1-0, Victor Mkanwa akafanya yale matokeo yakawa 1-1. Fred Felix ‘Minziro’ aliwaka kidogo kiwake, lakini mkwara wake na kule kuwa karateka ukazima kila kitu.
Ila ukweli ni kwamba walioshuhudia soka miaka ya 1970 na 1980 watakiri ubora wa Pondamali. Alikuwa kipa mahiri. Ni kama ilivyokuwa kwa Idd Pazi wa Simba. Huyu alikuwa mshindani wa Pondamali katika zama zake. Wakati ule ilikuwa vigumu kumuweka benchi pale Simba. Alikuwa imara kweli. Wengi watasema hayo.
Baada ya hapo nchi ikawa katika mikono salama ya Mwameja. Alitamba zaidi mwishoni mwa miaka ya 1980 na miaka ya 1990. Alitamba pale Coastal Union. Akatua Simba na kufanya makubwa. Akaweka alama zake pia kwenye kikosi cha Taifa Stars.
Mwameja alikuwa sehemu ya kikosi cha Simba kilichofika fainali ya Kombe la CAF mwaka 1993. Akatwaa mataji ya Kagame na Simba. Akashinda mataji ya Cecafa na Taifa Stars. Alikuwa mahiri kweli.
Watu wa zama zake watasema huyu alikuwa mahiri kuliko wengine. Ni kweli alikuwa mahiri, ila ni ngumu kusema aliwazidi kina Pondamali na Mambosasa. Kila mtu na nyakati zake. Baada ya kutamba pia kwa Peter Manyika aliyekuwa Yanga. Huyu naye alikuwa mahiri. Wengi tunamkumbuka namna alikuwa akivalia kofia yake kuzuia jua. Alipokuwa langoni, mashabiki wa Yanga waliona wako salama.
Akaja Kaseja. Kipa mwenye mwili wa tofauti na hao wengine. Kaseja ana mwili mdogo, lakini mambo yake yalikuwa makubwa langoni. Wengi hawakuamini katika mwili wake, lakini aliwaaminisha watu kwa kutumia mikono yake.
Kaseja ni miongoni mwa makipa wachache waliodumu kwenye ubora kwa miaka mingi. Alipotua Simba, aliifanya nchi nzima imzungumze. Kila kipa katika zama zake alitaka kudaka kama Kaseja.
Ni Kaseja ambaye alibadili fikra za watu wengi kuwaita makipa mahiri majina ya wale wa Ulaya au Amerika. Kipa mahiri aliyeibukia nchini alifananishwa na Kaseja. Huu ni mfano tosha wa kuonyesha namna alikuwa mahiri.
Akacheza Simba, kisha Yanga. Akarudi Simba kisha Yanga tena. Ndiye kipa pekee katika historia ambaye ameweza kucheza Simba na Yanga kwa nyakati mbili tofauti. Kwanini?
Ni kwa sababu alikuwa mahiri. Wote walitamani awe kwao. Katika zama zake, ukiwa kipa namba mbili nyuma ya Kaseja ni ngumu kupata nafasi ya kucheza. Angepangwa hata akiwa na homa. Ndiyo sababu hawa kina Barthez, Dida na wengineo walihama Simba na kutafuta nafasi kwingineko.
Ni Marcio Maximo tu aliyeamini tofauti. Akaamini ikipa mahiri lazima awe na mwili mkubwa na mrefu. Akamchagua Ivo Mapunda mbele ya Kaseja. Hata hivyo wananchi walimpinga. Pamoja na historia nzuri za makipa hao, zama hizi tumejaliwa kuwa na Aishi Manula.
Kipa mahiri kweli. Ndiye kipa bora wa zama hizi. Ametwaa tuzo kwenye ligi yetu kwa miaka nenda rudi. Manula alikuwa imara tangu akiwa Azam FC, japo mafanikio makubwa ameyapata akiwa Simba. Ameshinda mataji mengi zaidi. Amecheza mechi nyingi zaidi za kimataifa.
Ni uwepo wa Djigui Diarra ambao umempa ushindani Manula. Wengine wote walishindwa. Kwanini? Jibu ni jepesi tu, Manula ni bora zaidi katika zama hizi. Bahati mbaya tunamchukulia poa. Tunatengeneza sababu nyingi za ovyo kumfanya Manula aonekane kipa wa kawaida. Ila ukweli ni kwamba katika zama hizi, hakuna kipa anayemkaribia Manula.
Amewaacha mbali sana. Tunaweza kuwa na mjadala mkub juu ya kina Mambosasa, Pondamali, Mwameja na Kaseja kwa kuwafananisha na Manula, lakini kwa zama hizi tukiri Manula anaishi katika dunia ya peke yake na anastahili maua hata kama wapo wengine wasiotaka kukubali ukweli. Jamaa anajua kulinda lango na anajiamini.