Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Turekebishe kanuni wachezaji wa kigeni?

Aziz Ki Na Inonga Turekebishe kanuni wachezaji wa kigeni?

Thu, 15 Dec 2022 Chanzo: Mwanaspoti

Kabla ya kuanza kwa ligi ya msimu huu shirikisho la soka hapa nchini TFF lilipitisha na kuongeza idadi ya wachezaji wa kigeni kusajiliwa na timu mbalimbali kutoka wachezaji 10 hadi 12 na timu hizo kupewa uwezo wa kuwatumia wote wakati mmoja katika michezo ya mashindano.

Lengo kubwa la TFF kupitia kamati zake za mashindano ni kuongeza hali ya ushindani kwa timu kwenye ligi na kusababisha kuwa washindani wazuri hasa katika mashindano ya kimataifa ya CAF wanayoshiriki - iwe Kombe la Shirikisho au Ligi ya Mabingwa Afrika

Mbali na hilo pia kuna hili ambalo tunaamini uwepo wa hawa wachezaji wa kigeni utasaidia wachezaji wazawa kuongeza bidii zaidi na kufanya vizuri baadaye iwe rahisi kama nchi kupata timu ya taifa yenye ushindani mkubwa hasa ambayo itaingia kwenye malengo yetu ya kushiriki michuano mikubwa ya Afcon pamoja na Kombe la Dunia.

Baada ya kuongezwa kwa idadi hiyo ya wachezaji na kamati za mashindano za shirikisho tumeona timu mbalimbali kama za Coastal union, Kitayosce (ya Championship), Singida Big Stars, Azam, Ihefu, Simba, Mtibwa, Yanga, Namungo na nyinginezo zimesajili wachezaji wengi wa kimataifa kutoka mataifa mbalimbali

Pigia mstari neno idadi ya wachezaji wengi.

Kwenye neno hilo la idadi ya wachezaji wengi ndani yake kama utarudi nyuma utakutana na ukosefu wa neno ubora kwa kimombo wanasema quality.

Bado timu nyingi zimesajili wachezaji kwa idadi kubwa, lakini baada ya kusajiliwa wachezaji hao wanashindwa kuwa na ubora ambao huwa tunaufikiria kuwa wanao. Kama Yanga, Azam na Simba zimesajili wachezaji wa kigeni ambao wameshindwa kuonyesha ubora vipi kwa timu za madaraja ya kati kama Namungo, Coastal, Geita, Dodoma jiji na KMC wao wana hali gani?

Bado kuna ombwe kubwa kati ya idadi ya wachezaji wanaosajiliwa na ubora wanaokuja nao wachezaji hao. Kuna shida mahala hasa kwenye mamlaka za soka kukosekana kwa vigezo vya hao wachezaji wa kigeni wanaosajiliwa na timu za Ligi Kuu Bara.

Kwa wenzetu ipo wazi kabisa mfano Morocco wameweka idadi ndogo ya wachezaji wa kigeni wanaoruhusiwa kucheza ligi zao.

Pia timu nyingi zimeweka masharti ya wachezaji wa kigeni wanaowasajili kulipwa kulingana na idadi ya michezo wanaayocheza kwenye mashindano mbalimbali. Kama utapata muda zungumza na Clatous Chama, Tuisila Kisinda na Yannick Bangala

Nafikiria kwa sauti ya chini kama kungekuwa na vigezo toshelezi basi hawa kina Kambole, Chico Ushindi, Bigirimana Gael pale Yanga wasingepata nafasi hata ya kucheza Ihefu. Kuna kina Akamiko pale Azam, halafu kuna kina Akpan, Okwa, Ouattara ambao wanakiria mbio ndefu na kina Dejan waliocheza kwa muda mfupi na kuondoka zao.

Bado kuna kina Nahimana wa Namungo halafu kuna Farouk Shikalo aliyekuja kama upepo kwenye timu za Mtibwa Sugar na KMC na kufanya madudu na kwenda zake kwao Kenya.

Hili linaweza kuokolewa na kamati za mashindano na kulisaidia taifa hasa kwenye timu ya taifa wanapaswa kutoa mwongozo na vigezo ni mchezaji wa aina gani wa kigeni anapaswa kusajiliwa. Kwa mfano wangeweka au waweke kuwa ili mchezaji wa kigeni aje kucheza basi awe kwenye taifa lililo kwenye kiwango fulani cha ubora na acheze idadi fulani ya michezo katika timu za taifa lake.

Pia TFF kupitia kamati za mashindano ziwape masharti magumu hawa wachezaji wa kigeni hasa kwenye umri na maeneo nyeti ya kusajiliwa kwao. Kwa mfano wenzetu Misri eneo la kipa halitakiwi kabisa kuwa na mchezaji wa kigeni nje ya watu wa Misri.

Kama tunataka kupata wachezaji wazuri wa kigeni na wenye kuleta ushindani mkubwa eneo la ubora - tena ubora mkubwa hatuwezi kuliepuka hilo.

Lakini kama watakuja kina Bigirimana wanaowekwa benchi na Sure Boy, kama watakuja kina Kisinda wanaotolewa kwenye relini na kina Farid Musa bado tunakuwa tutatwanga maji kwenye kinu.

Na kama tunawasajili kina Victor Akpan halafu wanakuja kupigwa mkeka na kina Mzamiru Yassini bado hawa maproo watakuwa na safari ndefu ya kuleta ushindani mkubwa kwenye ligi yetu na pia kutupatia mafanikio katika timu zetu za taifa.

Chanzo: Mwanaspoti