Muda uliobaki kwa ligi kuanza unahesabika, kwani kila kitu kitaanza hivi karibuni ikiwa ni msimu mpya unaotarajiwa kuwa na ushindani mkubwa.
Ni Yanga walitwaa ubingwa wa ligi msimu wa 2022/23 wanakazi ya kuutetea kwa msimu mpya wa 2023/24.
Ikumbukwe kwamba Yanga walitwaa Ngao ya Jamii pia msimu wa 2023 kwa ushindi dhidi ya Simba Uwanja wa Mkapa.
Iwe ni kwenye anga za kitaifa na kimataifa ni muhimu kuwa na maandalizi mazuri kwenye kila idara.
Kinachotakiwa kwa sasa kuanzia kwa wachezaji ni kukamilisha mipango kwa umakini huku wakiwa tayari kupata changamoto mpya kwenye mechi ambazo watacheza.
Kuna mashindano mengi msimu mpya ikiwa ni Ligi Kuu Bara, Kombe la Azam Sports Federation, Ligi ya Mabingwa Afrika, Kombe la Shirikisho Afrika na Kombe la Mapinduzi.
Uwepo wa mashindano haya unamaanisha kwamba, ni muhimu wachezaji kujituma ili kupata matokeo kwenye kila hatua wanayoshiriki, jambo ambalo litawaongezea muda wa kuendelea kuwa katika ushindani.
Ni muhimu wachezaji kuongeza umakini katika kutimiza majukumu yao kwa muda uliobaki, ili kupata matokeo mazuri.
Iwe ligi yawanawake, kila sehemu katika mashindano ya mkoa ni lazima umakini uongezeke bila kusahau Championship ambapo timu zote zinapambana kupanda daraja na kushiriki Ligi kuu Bara.
Tunaona Ngao ya Jamii namna wachezaji wanavyopambana katika mchezo wa kuumizana ndani ya uwanja kwa makusudi, hii sio sawa, ni muhimu kila mchezaji kuwa makini.
Ngao ya Jamii inavyokwenda, ni picha ya kuanza rasmi kwa msimu mpya. Hivyo kuna mengi ya kujifunza kuanzia kwa waamuzi, wachezaji kutambua kwamba likizo imekwisha na kazi inaanza.
Itapendeza endapo kila mchezaji atakuwa mlinzi wa mwenzake na maamuzi ya waamuzi yakawa ya haki, hii itaepusha lawama baadaye.Ukweli ni kwamba muda ni mchache, mambo ni mengi kila kitu kiwe kwenye mpangilio wake.