Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Tunamwaga mboga aisee! Yanga yamgomea Fei Toto Azam

Feisal Salum Winning Goal Feisal Salum

Mon, 26 Dec 2022 Chanzo: Mwanaspoti

Uswazi kuna msemo maarufu “kama unamwaga mboga mie namwaga ugali” ili tukose wote, na sasa ndivyo hali inavyoelekea kuwa baada ya mabosi wa Yanga kuamua kumchenjia kiungo Feisal Salum ‘Fei Toto’ na dili lake la kutaka kutua Azam baada ya kuvunja mkataba ghafla juzi.

Mwanaspoti lililofichua juu ya dili hilo la Fei na Azam na jinsi kiungo huyo fundi alivyotumia mwanya wa mkataba wake na Yanga kuilipa Sh112 milioni ili kuwa huru, mabosi wa Yanga wamecheka sana na kusema “tuone sasa”, kwa kuamua kumrudishia fundi huyo fedha zake zote.

Sio kurudisha fedha, lakini wameamua kukomaa naye wakisema watamburuza Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) kabla ya kukimbilia Shirikisho la Soka la Kimataifa (Fifa), huku wakisisitiza Fei Toto bado ni mali yao, lakini baadhi ya wanasheria na wadau wametoa misimamo yao na kusema Azam na Fei wanatoboa kiulaini tu.

Ipo hivi. Baada ya mabosi wa Yanga kujua Fei hatanii kutaka kuondoka kutokana na madai ya kulipwa mshahara mdogo kulinganisha na wachezaji wa kigeni wasioitumikia timu kwa asilimia zote, wameamua kukomaa naye kiaina kwa kumng’angania.

Habari kutoka ndani ya Yanga zinaeleza kuwa Rais wa klabu hiyo, Hersi Said na wenzake waliitana faragha kumjadili Fei na Azam inayotajwa ndio iliyomtia ndimu ili kuwaburuza TFF na ikishindikana waende Fifa wakiona wamefanyiwa uhuni.

Chanzo hicho kinasema awali tangu Fei ahusishwe na Azam baadhi ya viongozi waligawanyika wapo waliotaka atimke kwa hoja Yanga ni kubwa na iwapo hata kama kiungo huyo atasepa na wengine wakiona kwa kipaji anastahili kujenga maisha yake ya kesho kimaslahi kwa vile wenyewe hawampi.

Lakini kuna waliopinga kwa sababu Yanga ya sasa inamtegemea zaidi kutengeneza shoo tamu uwanjani na kumfanya Fiston Mayele ateteme kila mara na ndio walioamua kumkomalia baada ya kushtuka kweli amesainishwa mkataba na Azam baada ya majuzi kuingiza fedha Sh100 milioni kuvunja mkataba na Sh12 milioni za mishahara ya miezi mitatu kulingana na vipengele vya mkataba wake.

“Mabosi wameamua kumkomalia kwani kilichofanyika ni uhuni. Tayari wameshazirudisha fedha alizoingiza na unafanywa utaratibu wa kumburuza TFF na hata Fifa, yeye na Azam yenyewe,” kilisema chanzo hicho. Lakini mapema ilidaiwa katika kumpoza Fei, viongozi walimfuata mama yake aliyekuja jijini Dar es Salaam ili kupata baraka za kumzuia, japo inaelezwa mipango imekwama kwani bi mkubwa alishatoa baraka kwa mchezaji huyo kujiunga Azam kwa ahadi nono zilizotolewa.

“Walienda hadi kwa mama yake kuzungumza naye, lakini wameahidi kumboreshea mkataba alionao kwa sasa kwa kumtaka aongeze mwingine na mshahara utakuwa Sh20 milioni,” chanzo hicho kilisema na kufafanua awali mabosi walikuwa tayari kumuongezea mshahara kutoka Sh4 milioni hadi 10 milioni lakini kama atasaini mkataba mpya wa miaka miwili kwa vile wa sasa ni ngumu kumboreshea.

Jana ilielezwa kuwa Yanga walipeleka barua ya malalamiko TFF na kusema kuwa watatoa tamko Jumanne. “Tumepeleka barua TFF ya malalamiko kuhusiana na ishu ya Fei, lakini kwa kuwa sasa mawazo yetu yapo kwenye mechi tutatoa tamko rasmi Jumanne,” kilisema chanzo, huku Fei akiwaaga rasmi wana yanga kupitia mitandao ya kijamii.

WASIKIE WANASHERIA

Wakili na mwanamichezo mzoefu nchini, Aloyce Komba alitoa ufafanuzi juu ya dili la Fei Toto kutua Azam akisema: “Yanga wamefanya uzembe wenyewe na wasije wakathubutu kukimbilia Fifa kama walivyofanya kwa Bernard Morrison itakula kwao. Waangalie vizuri mkataba wa mchezaji unaeleza nini, watapoteza muda zaidi.

“Ninachokiona Yanga walimpa mkataba Fei ambao hauna faida kwao. Unawekaje kiasi hicho cha pesa kuvunja mkataba wake wakati unaona kabisa kiwango cha mchezaji kilivyo. mchezaji hawezi kuacha pesa hasa kama mkataba wake unaruhusu kuununua ama kuuvunja.

“Sioni kama Azam wamekosea na ni timu ambayo inazingatia sana masuala ya kisheria katika kuvunja mikataba ya wachezaji wao ama wanaposajili mchezaji. Azam siyo wajinga kiasi hicho wakurupuke tu kumsajili Fei Toto pasipo kuzingatia taratibu za kimkataba.

“Wanachotakiwa kukifanya Yanga ni kuulezea umma ama wanachama na mashabiki juu ya hilo, lakini mengine ni kuleta siasa tu kwenye mpira.”

Kwa upande wa Wakili Alex Mgongolwa ambaye ni makamu mwenyekiti wa Kamati ya Sheria na Hadhi ya Wachezaji ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), alisema endapo Yanga wataona mkataba umekiukwa basi wapeleke malalamiko katika kamati hiyo.

Chanzo: Mwanaspoti