Kuna watu huwa tuna damu ya kunguni tukisema au kuhoji kitu tunaonekana kama tuna chuki binafsi au hatufurahii mafanikio ya watu.
Hii ndio dhana ambayo watu wenye upeo duni wamekuwa wakiitumia kujilinda pindi wanapokutana na ukosoaji badala ya kujibu hoja ambazo ndizo huwa msingi wa mjadala.
Nimejikuta ghafla tu nikiyasema haya baada ya kukumbuka mjadala fulani wa kimihemko ambao ulishikiliwa bango vilivyo na baadhi ya wachambuzi wa soka nchini kuhusu mabeki wawili wa Simba, Shomari Kapombe na Mohammed Hussein Zimbwe.
Baada ya Simba kutoka sare ya mabao 2-2 ugenini dhidi ya Power Dynamos ya Zambia, ndugu zangu baadhi wakaibuka na mjadala kuwa Zimbwe na Kapombe wameshachoka na kuzeeka hivyo kocha Robertinho anapaswa kuanza kuwapiga benchi.
Wakatumia ushahidi dhaifu wa Kapombe kupigwa chenga na Joshua Mutale ambaye baada ya tukio hilo akapika bao la kwanza la Power Dynamos lililokuwa la kujifunga la kipa Ayoub Lakred.
Kwa Zimbwe wakatumia hoja ya beki huyo kufanyiwa mabadiliko na kumpisha John Bocco.
Ulikuwa ni mjadala wa kimihemko zaidi na ni kwa sababu ulianzishwa na mashabiki hivyo tulitegemea watu wanaoaminika kwenye jamii kama wachambuzi waukwepe na wawaonyeshe mashabiki uhalisia kwamba wanachokifikiria sio kweli lakini kwa bahati mbaya baadhi yao wakaingia katika mkumbo huo.
Kilichokuja kutokea, baada ya mchezo ule, Kapombe na Zimbwe walijibu kwa vitendo kwa kuonyesha viwango bora uwanjani kuanzia katika mechi za ligi pamoja na zile za kimataifa.
Mfano katika mechi mbili za robo fainali ya Mashindano ya African Football League dhidi ya Al Ahly, Zimbwe alifanikiwa kumficha winga msumbufu, Percy Tau na kumfanya asiwe na madhara dhidi yao.
Kapombe ndiye aliyepiga krosi iliyozaa bao la Simba katika sare ya bao 1-1 ugenini dhidi ya Al Ahly.
Nadhani wale waliokuwa wanashupalia Kapombe na Zimbwe ni wazee na wamechoka wanapaswa kuendelea na msimamo wao kuliko kubaki kimya.