Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Tunahitaji wachambuzi wabobevu wa michezo

Wachambuzi Local Tunahitaji wachambuzi wabobevu wa michezo

Mon, 5 Feb 2024 Chanzo: Mwanaspoti

Taarifa ya Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo inaandaa mtalaa kwa ajili ya kutoa mafunzo ya elimu ya uchambuzi wa michezo, inaweza kuchukuliwa ni sehemu ya kawaida ya mipango ya maendeleo ya serikali.

Kwamba sasa nyanja ya uchambuzi imeongezeka upana, hivyo inahitaji mwongozo wa kitaaluma ili uchambuzi usifanyike kiholela na ulenge kitu fulani na uwe na ufanisi ambao unaweza kupimwa.

Bila shaka ndivyo serikali inavyofanya kazi, lakini kuna kitu zaidi ya alichokisema Naibu Waziri bungeni wakati akitoa taarifa hiyo katika moja ya majibu ya maswali ambayo wizara yake iliulizwa.

Kumekuwepo na lawama nyingi dhidi ua wachambuzi, nyingi zikionekana mitandaoni ambako ndiko hasa kuliko na watumiaji wa habari zinazotangazwa na kuchambuliwa na vyombo vya habari.

Kwa umoja wachambuzi wanaweza kujitokeza na kujitetea kama kundi, lakini wakiondoka kila mtu anakwenda kujifanyia mambo yake ya ajabu, baadhi wakijikita kwenye uchambuzi unaozingatia mambo muhimu, huku wengine wakijifanyia ili mradi.

Baadhi hudiriki kuwatukana wachambuzi, kuwakebehi, kupuuza uchambuzi wao kwa madai kuwa unahusiana na maslahi binafasi kama kutetea wachezaji walio katika menejimenti zao, kuponda baadhi ya watu kwa sababu za kibinafsi, kutojikita kwenye hoja muhimu za maendeleo ya michezo kwa kuhofia kuwagusa wafadhili wao binafsi, chuki binafsi na mapenzi ya klabu pendwa.

Wako wachambuzi waliofikia kuwa watabiri wa matokeo ya mechi, hasa za kimataifa zinazohusisha Simba na Yanga pekee, wako wanaojikita kuponda mchezaji yeyote mpya na wapo wanaosifia tu kila kinachofanywa na viongozi fulani. Wapo wachambuzi ambao wameibuka kuwa ni watoaji wa habari motomoto (breaking news) kuhusu watu fulani, kama huyo wa juzi aliyemtuhumu Kocha wa Taifa Stars anachukua mlungula ili ateue na kupanga wachezaji, wako wanaotoa habari mchezaji fulani hakuwa kwenye umiliki wa klabu yake ya sasa na ana taarifa hajauzwa na klabu hiyo bali fedha zimeenda kwingine.

Wapo ambao wanajaribu kuzungumzia masuala ya kitaalamu bila ya kufanya utafiti kujua lipi ni lipi, mfano kumponda Mkurugenzi wa Ufundi wa Shirikisho la Soka (TFF) kutokana na timu ya taifa kutofanya vizuri, au kudai wanachama na maashabiki wa klabu hawanunui jezi za timu ndio maana kiwango chao cha hisa hakiwezi kufikia asilimia 51 kama kanuni za umiliki zinavyotaka. Yaani ili mradi vurugu tu.

Ni taabu tu kila unapoangalia vipande vya video (kwa sababu ni ngumu kusikiliza kipindi cha saa tatu nzima redioni), unajiuliza ilikuwaje huyu akafikia kusema haya au kutabiri hili au kutoa habari hii!

Kuna kituo ambacho wakati wa uchambuzi kinahangaika na maneno ambayo Msemaji wa Yanga aliyesimamishwa, Haji Manara na TFF anatoa kwenye kurasa zake za mitandao kuhusu matukio ya soka.

Unashangaa huyu jamaa kwa sasa habebi dhamana ya taasisi yoyote ile, lakini bado anafuatiliwa kila anachokiandika kana kwamba bado anaiwakilisha taasisi yake.

Ni kupoteza muda na rasilimali kumzungumzia mtu ambaye hawakilishi taasisi yoyote au inaweza kuchukuliwa ni chuki binafsi ambazo zinaingizwa kwenye kipindi kinachokwenda kwa mamilioni ya watu.

Kwa hiyo, taarifa ya wizara ingeweza kutafsiriwa kirahisi tu, serikali imeona tatizo katika uchambuzi na hivyo inataka iweke mwongozo ili dhana hiyo isitumiwe vibaya kukandamiza watu, kuinua watu wasiostahili, kupotosha watumiaji wa habari, kupotosha mwelekeo wa mijadala ya kitaifa kuhusu maendeleo ya michezo, kujenga umaarufu kwa watu wasiostahili na kustawisha maslahi binafsi yasiyo na umuhimu wowote kwa taifa.

Tunahitaji uchambuzi kwa sababu hutusaidia kuelewa mambo kwa mapana na marefu yake kwa kuturahisishia ufahamu, lakini uchambuzi unapokwenda kombo si rahisi watu kuelewa jambo kwa mapana na marefu yake.

Ni lazima wachambuzi wawe ni wale waliobobea kwenye eneo moja, hivyo kuhitajiwa na vyombo vya habari pale kunapotokea jambo kwenye eneo hilo. Haiwezekani mchambuzi akawa mahiri wa kila kitu. Kwamba leo kuna suala la mfumo wa mchezo, wanaojadili ni walewale; leo kuna matatizo ya Katiba ya Simba kuhusu umiliki, wanaojadili ni walewale; kuna tatizo la kanuni za uchaguzi za Chama cha Mpira wa Wavu, wanaojadili ni walewale; kuna mwelekeo chanya wa wanariadha wa Kenya katika mbio fupi, wanaojadili ni wale wale na mengine mengi.

Na kibaya zaidi, hawa hawaitwi studio kwa sababu ya ubobezi wao katika nyanja fulani, bali wanakuwa wako zamu kwa ajili ya kuchambua.

Iwe wana ufahamu wa kutosha kuhusu jambo linalokusudiwa kuchambuliwa au hawana.

Watachambua kwa upeo wao. Hapo kuna uwezekano mkubwa wa kupiga nje na halafu mitandao ikajaa kejeli.

Ukichanganya siku hiyo studio wanaweza kuwa watu wanne hadi watano wote wanataka kujadili suala hilohilo, ni dhahiri muda mfupi wanaoupata utatumika kuzungumzia kile anachokijua kuhusu suala hilo. Kama akipiga nje, lawama kwa wachambuzi kesho.

Ukiongeza kwamba hawa wako kazini siku nne au tano kwa wiki, unagundua kuwa ni lazima wanakosa huo muda wa kutosha wa maandalizi ambao huhusisha kukusanya taarifa nyingi na kuongea na watu tofauti ili kuelewa kitu kwa mapana na marefu.

Kuchambua si kuingia Google kutafuta kitu fulani kina maana gani na kwenda kukisema kwenye mjadala, bali kuwa na ufahamu wa mapana na marefu yake, kihistoria, kiuchumi na kiutamaduni kuweza kuzungumzia vizuri jambo lililotokea leo.

Kwa hiyo mpango wa wizara usingejikita kwa kundi dogo la wachambuzi, bali kwanza kuzungumza na vyombo vyao ili kujua watarekebishaje hali hii inayosababisha wachambuzi wazungumzwe kwa kejeli na mzaha na ikiwezekana vyombo hivyo viandae miongozo yake ya jinsi ya kuendesha mijadala kuhusu mambo mbalimbali ya kimichezo.

Tunaona SuperSport hutumia wachezaji wa zamani kuchambua mechi, hutumia waandishi wakongwe kujadili masuala mbalimbali makubwa ya kimichezo, kati Shirika la Utangazaji la Uingereza (BBC) hutumia watu waliobobea kama kwenye siasa za Mashariki ya Mbali, au Amerika Kusini kuchambua matukio yanayotokea maeneo hayo.

Hali kadhalika DW la Ujerumani, Al Jazeera na mashirika mengine ya kimataifa.

Kwa nini kwetu hapa kila mtu awe anaweza kuchambua kila kitu? Huo uwezo anautoa wapi? Jibu ni, kufanya hivyo ni kushusha thamani ya maudhui, kupotosha wasikilizaji, kupotosha mwelekeo wa mijadala na kuvuruga masuala mbalimbali kwa kujua au kutojua.

Kesho ukiuliza maoni ya wananchi kuhusu jambo fulani, utapata kitu cha ajabu kwa kuwa wamelishwa maajabu!

Kuna tatizo katika uchambuzi, lakini halitokani na kukosa mafunzo, bali mambo kuendeshwa kiholela na vyombo vya habari. Vikijipanga vizuri, kero za uchambuzi zitapungua.

Tatizo si elimu, bali ni mfano Tanzania imefuzu kucheza fainali za Mataifa ya Afrika (Afcon 2023).

Uchambuzi hatakiwi kwenda Google na kuangalia kama iliwahi kufanya hivyo huko nyuma na kutafuta majina ya walioiwezesha kufuzu wakati huo.

Bali ni kujua ilifuzu vipi, mazingira ya wakati huo, hamasa, idadi ya timu zilizokuwa zinafuzu, idadi ya mechi ambazo timu ilicheza hadi kufikia fainali hizo, mazingira ya kambi na benchi la ufundi, kwa uchache.

Chanzo: Mwanaspoti