Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

TV

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Tunahitaji timu ya kueleweka, siyo wachambuzi

Taifa Stars AFCON Vazi Tunahitaji timu ya kueleweka, siyo wachambuzi

Wed, 7 Feb 2024 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Serikali inataka kutumia nguvu kubwa kwenye mambo madogo. Shida ya mpira wa Tanzania sio wachambuzi. Nchi yetu haifanyi vizuri kwenye soka kwa sababu ya kukosa akademi za kutosha za kuzalisha wanamichezo, miundombinu ya michezo ni tatizo la kudumu, teknoloji kwenye michezo bado iko nyuma na mengine mengi.

Inasikitisha kuona serikali inataka kuandaa kozi za uchambuzi. Huku ni kupoteza muda na rasilimali. Huku ni kutaka kuchezea kodi za wananchi. Tanzania haihitaji kuandaa wachambuzi, inahitaji kuandaa wanamichezo. Serikali iache kutumia nguvu nyingi kwenye vitu vidogo.

Shida ya michezo ya nchi hii sio wachambuzi. Serikali inapaswa kuona ni kwa namna gani wanaweza kuboresha Umiseta na Umitashumta kwa sababu ndiko wanakopatikana wanamichezo wengi tena wakiwa kwenye umri mdogo.

Ningefurahi kusikia tunaanzisha shule maalumu za michezo nchi nzima. Ningefurahi kuona baada ya Umiseta na Umitashumta vijana wote wenye vipaji wanapelekwa shule maalumu kwenda kuendelezwa zaidi.

Uchambuzi ni kitu kidogo sana. Sioni hata sababu ya msingi ya kutaka kutumia nguvu kubwa. Hili ni jambo la ziada sana kwenye nchi. Tungeshughulika na mambo ya msingi kwanza. Mpira  hauwezi kuendelea kwa kuwa na wachambuzi wengi hodari. Kwa hili la kuanzisha kozi maalumu za uchambuzi, ni matumizi mabaya ya mali za umma.

Hakuna hata chuo kimoja Ulaya kinachofundisha uchambuzi wa michezo kwenye vyombo vya habari.

Uchambuzi wa kusomea ni ule wa kiufundi ambao watu huajiriwa kama wachambuzi kwenye timu za mpira na wengi hukaa hadi kwenye mabenchi ya ufundi. Kwa mfano kuna watu ni wataalamu wa kuchambua video za mechi husika kwa haraka kabisa ikiwa inaendelea.

 Tatizo letu  tunataka kupita njia ya mkato. Wachambuzi wetu kwenye vyombo vya habari sio tatizo la msingi kwenye ustawi wa michezo yetu.

Wenzetu wanachokifanya ni kutumia zaidi wachezaji na makocha wa zamani ambao wameuishi mchezo husika halafu wanampatia mafunzo kidogo ya vyombo vya habari. Ukimchukua mtu kama Amri Kiemba, Boniface Pawasa na kumpatia mafunzo ya vyombo vya habari anakuwa mchambuzi mzuri sana. Hakuna haja ya kuandaa somo la uchambuzi ni matumizi mabaya ya pesa za umma. 

Tungewekeza zaidi kwa wachezaji na makocha wa zamani. Shida kubwa ya makocha na wachezaji wa zamani, wengi uelewa wa mambo uko chini kidogo. Anaweza kuwa alikuwa mchezaji mzuri, lakini hata kuelezea tu mchezo wenyewe akashindwa. Tunahitaji kuwajengea uwezo.

Wachezaji wa zamani wakipatiwa mafunzo kidogo ya vyombo vya habari wanaweza kufanya vizuri zaidi. Serikali ingerudi na kuanza kutatua shida za msingi sio mambo ya wachambuzi. Hili ni jambo dogo ambalo halikupaswa kuwa ajenda ya serikali.

Nchi nyingi za Afrika zinazofanya vizuri na hasa kwenye soka, hazijawahi kutegemea wachezaji - wanaandaliwa na kukulia Afrika. Ukiachilia mbali Afrika Kusini, hakuna Taifa lingine lolote kubwa linalotegemea soka la Afrika kufanikiwa kwenye Afcon.

Mataifa makubwa yote msingi wake ni wachezaji ama waliokulia na kulele Ulaya au wanaocheza ulaya kwa sasa. Serikali, wadau na TFF wangeweza kukaa na kuandaa mpango wa nchi wa namna tunavyoweza kupata wachezaji wengi wenye uwezo wenye asili ya Tanzania, lakini wanaishi nje.

Serikali na wadau wake wanaweza kutengeneza njia ya kupeleka watoto wengi nje ya nchi kupata msingi mathubuti wa michezo.

Ni kama tunavyoweza kupeleka vijana kwenye vyuo vikuu nje. Ni Kama tunavyoweza kupeleka watoto wenye vipaji maalumu nje kusoma. Hili ndiyo lingekuwa jambo la msingi kabisa kuliko kutaka kuanzisha kozi za uchambuzi.

Sisi bado hatuna cha kuchambua. Bado tunajitafuta tu. Tunaanzisha kozi ya uchambuzi wakati hatuna hata kinachochambuliwa. Nashauri serikali na wadau watengeneze utaratibu wa kupeleka vijana nje.

Tukipata watoto kama 200 utakuwa mwanzo mzuri kwetu. Tutengeneze kwanza wachezaji kabla ya wachambuzi. Tuboreshe kwanza miundombinu ya wachezaji kabla ya wachambuzi. Huku ndiko serikali inapaswa kuanzia. Wachezaji kama Nickson Kibabage, Abdul Suleiman ‘Sopu’, Clement Mzinze, Ladack Chasambi, Aboutwalib Mshery unapaswa kuwa mkakati wa nchi kuwapeleka nje. Hawatakiwi kucheza tena nchini msimu ujao. Klabu, TFF na serikali lakini wawe na ajenda ya pamoja.

Tunahitaji kutengeneza kina Mbwana Samatta wengi wa baadaye. Tunahitaji kuwa na kina Novatus Dismas wengi siku za usoni. Tuachane na mpango wa kuanza kutafuta wachambuzi bora wakati bado hatuna wachezaji.

Tunahitaji kuendeleza makocha wetu nje ya nchi. Tunahitaji kuwa na makocha wazawa pia wenye uwezo mkubwa. Makocha wetu  wengi wazawa bado wanahitaji kujengewa uwezo. Tukiwa nao hata 20 ambao wako nje ya nchi wanajifunza na kutafuta uzoefu, kuna mahali tutasogea muda si mrefu.

Uchambuzi sio hitaji letu la msingi. Kuna mambo mengi  tunahitaji kuyaweka sawa kabla ya kurukia la wachambuzi. Serikali, wadau (kwa maana ya klabu) na TFF wanahitaji kuja na mkakati wa pamoja wa kupeleka wachezaji nje na wawe wenye asili ya Tanzania kurudishwa nyumbani.

Hili ndilo limefanikisha mataifa mengi ya Magharibi na Kaskazini mwa Afrika kupiga hatua kwenye michezo sio wachambuzi. Tuache kupoteza muda kwenye mambo madogo na kukwepa mambo ya msingi.

 Wachambuzi bora hawatatupeleka Kombe la Dunia. Tunahitaji kuwa na timu bora ili tuweze kushindana vizuri na vigogo wa Afrika, sio wachambuzi.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live