Shabiki wa Klabu ya Simba, Mjata Mjata anasema kuwa mojawapo ya sababu iliyowapelekea watoke sare kwenye mechi dhidi ya Power Dynamos ni wachezaji kushindwa kujituma na kuwa makini kwenye eneo la umaliziaji huku akiwaangushia lawama, yeye anawalaumu wachezaji wa Simba akiwemo Jean Baleke na Saido Ntibazonkiza.
Kauli hiyo ya Mjata Mjata inakuja baada ya Simba kutoa sare ya bao 2-2 dhidi ya Power Dynamos ya Zambia juzi Jumamosi, Septemba 16, 2023 wakati wa mchezo wao wa Ligi ya Mabingwa Afrika uliopigwa katika Dimba la Levy Mwanawasa nchini humo.
“Kauli ya mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya Simba (Salim Abdallah ‘Try Again) alitueleza kuwa mtaiona Simba ya Afrika itacheza leo (juzi), ukisikiliza hiyo kauli na Simba ilivyocheza ni vitu viwili tofauti, kwa matarajio yangu nilidhani nitaona kitu cha ziada kuliko kile kilichofanyika.
“Ukiniuliza sababu ya msingi ya kupata sare na Power Dynamos ninakwenda moja kwa moja kuwalaumu wachezaji. Sidhani kama kinahitajika kitu gani straika kama Jean Baleke na Saido Ntibazonkiza kukosa goli kama zile.
“Ninaamini kwamba wachezaji walijiamini kupita kiasi ndiyo maana matokeo yakawa vile. Yale hayakuwa matokeo halisi kwetu kwa sababu ukiweka Simba na Power Dynamos hapa, unaona utofauti. Matarajio yetu hayakuwa yale, tulitarajia kushinda mechi.
“Ukisema mateokeo ya ugenini ni sawa lakini kauli za viongozi haziko sawa, ndiyo maana mimi napenda kusikia kauli za mkuu wa Benchi la Ufundi badala ya kauli za utawala, hawasemi uhalisia. Tulichokitarajia ni tofauti na tulichokiona,” amesema Mjata Mjata.