Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Tumuombee Miquissone asije akawa Coutinho mwingine

Jose Luis Miquissone Noma.jpeg Luis Miquissone

Tue, 10 Oct 2023 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Wakati mwingine ndoto tamu inakatizwa na kelele. Unatamani uendelee kuota tena lakini haiwezekani. Jose Luis Miquissone ameanza kunitia wasiwasi. Nini kinamtokea? Sijui. Lakini inanitia wasiwasi kwa sababu imewahi kuwatokea wachezaji wengine.

Wakati mwingine unalazimika kuhama na kuondoka zako. Bahati mbaya mambo hayawi yale yale kama yalivyokuwa. Unajaribu kurudisha vitu njiani lakini haiwezekani tena. Unatamani usingehama. Iliwahi kumtokea Phillipe Coutinho alipokuwa Liverpool. Alikuwa kipaji hasa. Ndoto ya kila timu kuwa naye.

Ghafla akahama kwenda Barcelona. Hispania ni kati ya timu ndoto za wachezaji wa Amerika Kusini. Maisha hayakuwa yaleyale tena. Ghafla akashuka. Barcelona hawakumuhitaji tena. Akaenda zake Bayern Munich kwa mkopo. Mambo hayakwenda sawa. Akarudi zake Barcelona mambo hayakwenda sawa.

Akaenda zake Aston Villa mambo hayakwenda sawa. Fikiria, miaka michache tu nyuma ilikuwa inaonekana kama ndoto kwa Aston Villa kumpata mchezaji wa hadhi ya Coutinho lakini sasa wakampata na bado akawa anasugua benchi. Ukikaa chini na kutafakari unatamani Coutinho asingehama Liverpool.

Hii inatokea kwa Miquissone? Sina uhakika. Ninachojua ni kwamba natamani asingeondoka Simba. Hata hivyo, kwa wakati ule kulikuwa hakuna cha kumzuia Mmakonde kuondoka. Ada ya uhamisho kubwa, pesa yake aliyopewa awake mfukoni kusaini Al Ahly ilikuwa kubwa, mshahara mkubwa, alikuwa anakwenda timu kubwa Afrika. Isingewezekana kumzuia.

Lakini sasa Al Ahly wameturudishia Miquissone ambaye hatukuwapa. Mwanzoni ilitajwa kwamba alikuwa amenenepa. Ni kweli ungeweza kumuona kabisa akiwa amenenepa. Baadaye ikatajwa kwamba amekata uzito. Ni kweli ungeweza kumuona amepungua.

Kilichokuwa kinamtatiza ni uzito? Kwa sasa amekata uzito. Tatizo baada ya kukata uzito bado hatumuoni Miquissone tuliyempenda na kumuhusudu. Juzi aliachiwa mpira mmoja akiwa peke yake. Katikati ya uwanja. Mlinzi mmoja wa Singida Fontaine Gate alijaribu kumuweka aotee lakini ikaonekana kama vile alikuwa hajaotea.

Alikimbia na mpira kwa kile ambacho mwenyewe aliona ni kasi lakini ukweli ni kwamba haikuwa kasi ile ya Miquissone ambayo tulimjua na kumzoea. Akakutwa na mlinzi huyu huyu ambaye awali alikuwa amemuacha kwa mita 20. Ingekuwa wakati ule anawasili tungeweza kudai ni uzito lakini sasa Miquissone amekata uzito.

Lakini katika pambano hilo Miquissone aliingia katika kipindi cha pili. Jiulize, Miquissone wa kweli anawezaje kukaa benchi katika pambano gumu la ugenini dhidi ya Singida? Hakuna shabiki yeyote aliyepiga kelele kwa sababu hapa karibuni walimuona akicheza na hakuwa amefanya maajabu.

Mashabiki wetu ni wanazi haswa lakini sio wajinga. Kama Miquissone angekuwa katika ubora wake halafu Robertinho akamuweka benchi katika pambano dhidi ya Singida ugenini nadhani angekiona cha mtema kuni. Hata hivyo, mashabiki hawajalaumu kwa sababu wanajua wamerudishiwa mchezaji mwingine na Al Ahly.

Tuendelee kumsubiri arudi katika ubora wake lakini nimeanza kupata shaka kidogo na kukumbuka stori ya Coutinho. Wakati mwingine mchezaji akihama anajikuta hawezi kurudi tena katika ubora wake. Wakati mwingine mchezaji akirudi kwa mara ya pili klabuni anajikuta hawezi kurudi tena katika ubora wake.

Awali, nilikuwa sina na wasiwasi na Miquissone kwa sababu ya uzito wake. Nilijua akikata uzito wake atakuwa moto kama ilivyokuwa kabla hajaondoka. Hata hivyo, najikuta naanza kupatwa na wasiwasi kwa sababu uzito umeondoka lakini bado uamuzi wake na kasi yake sivioni uwanjani.

Lakini pia nilikuwa na wasiwasi na umri. Kwamba licha ya kumsubiri arudi na kutuonyesha vitu vyake huenda umri ulikuwa unamtupa mkono. Hapana. Ana umri wa miaka 28 tu kwa mujibu wa mtandao wa Wikipedia. Sidhani kama ni suala la umri kama ilivyokuwa katika ujio wa pili wa Serge Wawa hapa Tanzania.

Kitu kingine ambacho niliamini kwamba Miquissone ataingia moja kwa moja katika soka letu ni ukweli anayafahamu vema mazingira ya soka la Tanzania. Sio mgeni. Anajua vyakula vyetu, anavijua viwanja vyetu, na anawajua pia baadhi ya wachezaji aliowaacha klabuni kama kina Clatous Chama ambaye ni rafiki yake.

Nilidhani angeingia moja kwa moja na makali yake katika kikosi cha kwanza tofauti na wachezaji wageni. Hata hivyo, inaonekana kama vile amekuwa mgeni kuliko kina Che Malone. Nitaendelea kumsubiri Miquissone kwa sababu Simba inamuhitaji zaidi kuliko wakati mwingine wowote ule.

Hii ni kwa sababu hapa katika miaka ya karibuni Simba inaonekana kama vile imekosea kusajili. Kuna wachezaji wengi ambao wamekuja na kuondoka lakini hawakuweza kuziba pengo lake. Hawa ni kama vile kina Pape Sakho na Peter Banda. Ilionekana kama vile anakuja kuchukua ufalme wake moja kwa moja lakini hali haijawa hiyo.

Kama vile haitoshi, hata katika dirisha hili inaonekana kama vile Simba imechemka tena kuwachukua baadhi ya wachezaji. Rafiki yetu Osamba Onana aliingia nchini kwa mbwembwe lakini kadri siku zinavyosonga mbele anaonekana kuwa mchezaji laini na Simba imeanza kurudi tena kuwategemea kina Kibu Dennis.

Kama Miquissone hatarudi kuwa yule tena basi maisha yanaweza kuwa magumu kwa Simba ambayo muda si mrefu itaingia uwanjani katika michuano miwili mikubwa ya Afrika. Watu wanategemea kuiona ile Simba ya Chama na Miquissone lakini wakati mwenzake Chama akiwa amerudi vema baada ya kuchemka Morocco, Miquissone hajarudi kama alivyoondoka.

Licha ya kuwasubiri kwa hamu wachezaji wapya kina Onana lakini ilionekana kama vile Miquissone ndiye aliyekuwa usajili mkubwa zaidi katika dirisha kubwa lililopita la uhamisho. Na inasemekana Simba walitumia dau kubwa zaidi kumrudisha kutoka Al Ahly. Anapaswa kurudi kuwa kama alivyokuwa kama kweli Simba wanataka kufanya vema katika michuano hii.

Wasiwasi mkubwa asiwe kama Coutinho. Kwamba uhamisho unatibua kila kitu katika maisha yake ya soka. Asiwe kama Fernando Torres ambaye uhamisho wake kutoka Liverpool kwenda Chelsea uliharibu kila kitu katika maisha yake ya soka. Alijaribu kujipambanua ili arudi katika fomu lakini haikuwezekana. Alikwenda AC Milan akarudi kwao Atletico Madrid kwa mkopo lakini haikuwezekana.

Wakati mwingine huwa inatokea kwa wachezaji mbalimbali barani kote. Maisha hayaendi sawa pale unapoamua kubadili upepo. Hata wenyewe, kwa nyakati kadhaa huwa wanaelezea majuto ya kuhama kutoka katika klabu moja kwenda nyingine jinsi yalivyositisha uwezo wake. Hata hivyo, kwa wakati huo hawakuwa na jinsi zaidi ya kuhama!

Chanzo: www.tanzaniaweb.live