Siku chache tu tangu Yanga imtangaze mdhamini mpya wa mechi sita za Kombe la Shirikisho Afrika, kampuni ya SportPesa ambayo ni Mdhamini Mkuu wa klabu hiyo nayo imetoa tamko la kusikitishwa na kilichofanywa na wenzao, lakini pande zote mbili zimefafanua ishu hiyo.
Yanga iliingia makubaliano na kampuni ya Haier ya China na kuwa na uhakika wa kuvuna Sh 2.1 Bilioni katika mechi hizo za CAF, huku Rais wa Yanga akinukuliwa kwamba walipata ridhaa ya SportPesa ambayo jana mchana ilikanusha kuwepo kwa muafaka huyo na kufananua kilichotokea.
Awali SportPesa ilitoa taarifa ya kueleza kusikitishwa na kilichofanywa na Yanga huku kukiwa bado hakuna muafaka baina yao huu ya kampuni gani itumike eneo la kifuani mwa jezi za timu hiyo kwa mechi za kimataifa kutokana na mgongano wa kimasilahi uliopo dhidi ya kampuni ya kubeti inayodhamini michuano hiyo ya CAF.
Hata hivyo, mmoja wa mabosi wa juu wa Yanga amesema mapema baada ya timu yao kufuzu hatua ya makundi waliwatafuta SportPesa na kuwajulisha juu ya zuio la kutoka CAF katika mechi za hatua ya makundi na kuendelea.
“Tulipowaandikia kuwajulisha juu ya zuio la CAF, wenzetu (SportPesa) walitujibu kuwa tuwathibitishie kimaandishi juu ya zuio hilo la CAF, tukawasiliana na CAF na wakatupa huo uthibitisho na tuliwarudishia kimaandishi,” alidai bosi huyo.
“Hawakutujibu na tukawakumbusha lakini wakawa kimya, baadaye tukawaambia, kuna kampuni tumeipata ambayo haina mgongano nao kimaslahi tukiwaomba watudhamini katika hizi mechi chache tu tukitolewa hatutakuwa nao,” alisema kigogo huyo aliyefafanua waliwajulisha SportPesa kuwa lengo lilikuwa ni kupata fedha za kupunguza makali ya uendeshaji.
“Baada ya kuwaandikia hivyo wakatutaka tuwajulishe jina la hiyo kampuni, tukawajibu haraka lakini baadaye wakatujibu kwamba hawakubaliani na hilo wakatupa jina la kampuni nyingine pia wakatuambia kama hatutakubaliana tutumie maneno ‘Visit Tanzania’.
“Tulipoangalia ile kampuni tukaona bado ni aina nyingine ya kampuni kama wao tukasema tuwaulize CAF nao wakatujibu hawaruhusu hiyo kampuni kwa kuwa bado ina mgongano na kampuni wadhamini wao.
“Tulipowajibu hawakujibu hadi sasa, Yanga tukaona tuingie huu mkataba kwa kuwa ni wa muda mfupi lakini haya yote yanazungumzika tutawatafuta na kuongea nao tujue hoja zao zaidi.
Hata hivyo, Meneja Uhusiano na Mawasiliano wa SportPesa, Sabrina Msuya alipoulizwa jana alisema taarifa waliyotoa awali ndio msimamo wa kampuni, lakini alifafanua kwamba walishangaa kuona Yanga wakimtambulisha Haier kabla hawajafikia muafaka wa mazungumzo yao.
“Sisi tunajua kuwa hatua ya makundi hatuwezi kukaa kwenye jezi za Yanga na tulijadiliana cha kufanya ikiwamo kuwapa LiveScore ambayo walisema inahusika na beting na imekataliwa na CAF, tukaomba ushahidi wa maandishi kwa kujua hii inaonyesha matokeo ya mechi na sio kubeti,” alisema Sabrina na kufafanua kuwa, wakati wakisubiri kujua cha kufanya wakaona wenzao usiku wakizindua jezi na kumtangaza mdhamini mpya.
Alisema, tayari wameanza kuchukua hatua ya kuhifadhi haki yake kutoka kwa mamlaka, kwa kuzingatia wana mkataba na haki ya kuwa kifuani mwa jezi za Yanga kwa miaka ya soka ya 2022 -2025.
Baada ya kumtafuta Rais wa Yanga injinia Hersi Said alisema; “Tupeni muda tutatoa taarifa kamili hili sio jambo la kutoa taarifa kwa haraka,”alisema Hersi ambaye atawala wake umehusika katika mikataba yote miwili, huku Tarimba Abbas, Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa SportPesa, alipotafutwa akiwa jijini Dodoma bungeni alisema hawezi kusema lolote.