Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

 Tukutane robo fainali CAF

Simba 5 1  Tukutane robo fainali CAF

Mon, 14 Mar 2022 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

SIMBA wanacheeeeka! Wanasema tukutane robo fainali Afrika. Hiyo ni baada ya kuwachapa Waarabu, RS Berkane ya Morocco kwa bao 1-0 kwenye Uwanja wa Mkapa jijini Dar es Salaam, jana Jumapili katika mchezo wa Kombe la Shirikisho Afrika.

Ushindi huo umewasogeza Simba katika nafasi nzuri ya kutinga robo fainali ya michuano hiyo. Bao hilo pekee lilifungwa kitaalamu na kwa ufundi mkubwa na kiungo Msenegali, Pape Ousmane Sakho dakika ya 43, aliyeichambua ngome ya Berkane kutokea kushoto mwa uwanja, akiwapiga chenga mabeki kabla ya kufunga akimuacha mlinda mlango akiwa amezubaa asijue la kufanya huku akishuhudia mpira ukiingia kambani.

Asingeweza kuudaka mpira ule kwa kuwa ulipigwa kiufundi, na hakujua kama utapigwa kwa wakati ule. Lilikuwa ni tukio la ghafla na ni moja ya mabao makali, aina ya yale ambayo hufungwa katika mechi kali kwenye ligi kubwa za Ulaya.

Simba walianza kushambulia dakika za mwanzo kabisa wa mchezo na ilionekana kuwa watapata bao, kwani ndani ya dakika 5 za kwanza tayari walikuwa wameshafanya mashambulizi matatu ya hatari langoni mwa Berkane.

Lakini dakika ya 19, Simba walipata faulo ya kwanza karibu na lango, Larry Bwalya akapiga shuti lililogonga ukuta wa Waarabu hao. Dakika 25 za kwanza zilikatika huku Simba wakionekana kushambulia zaidi tofauti na wapinzani wao Berkane ambao walicheza kwa kujilinda ili wasiruhusu bao la mapema.

Berkane walianza kipindi cha pili kwa kasi wakifanya mashambulizi ya kushtukiza huku Simba wakiwa imara na kujilinda vyema. Dakika ya 64, Simba walifanya mabadiliko ya kwanza, alitoka Kibu Denis akaingia Bernard Morrison ambaye alichangamsha mchezo.

Morrison alitengeneza nafasi nyingi na kukosa mabao kadhaa akicheza kwa ustadi mkubwa tangu alipoingia. Ushindi huo unawafanya Simba kuongoza Kundi D wakiwa na pointi saba, wakifuatiwa na Berkane kabla ya mchezo wa usiku kati ya Asec na USGN ambao matokeo yake hayana madhara kwa Simba kuendelea kuongoza kundi hilo.

Simba sasa mchezo wake unaofuatia katika michuano hiyo ni dhidi ya Asec Mimosas ugenini Machi 20, kabla ya kumaliza hatua ya makundi jijini Dar kwa mchezo dhidi ya USGN Aprili 3.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live