Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Tukutane Uwanja wa Taifa

70780 Taifa+pic

Sat, 10 Aug 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Mambo ni moto, mambo ni hatari ‘fire’. Baada ya kutesti mitambo katika matamasha yao ya mwaka, miamba wa soka nchini Simba na Yanga wana mtihani wa kuonyesha ubora wa vikosi vyao vipya kwa mara ya kwanza msimu huu katika mechi za Ligi ya Mabingwa Afrika leo.

Mabingwa mara mbili mfululizo wa soka nchini, Simba watakuwa ugenini nchini Msumbiji dhidi ya UD Songo, wakati Yanga wataileta burudani jijini Dar es Salaam watakapoikaribisha Township Rollers ya Botswana kwenye Uwanja wa Taifa katika mechi zao za raundi ya awali ya Ligi ya Mabingwa Afrika.

Wawakilishi wengine wa Tanzania, KMKM ya Zanzibar watakuwa wenyeji wa Azam FC wa 1’de Agosto ya Angola katika mchezo wa Ligi ya Mabingwa Afrika kwenye Uwanja wa Amani leo, huku Malindi ya Zanzibar itakiwasha ugenini Somalia dhidi ya Mogadishu City katika Kombe la Shirikisho.

Azam itawavaa Fasil Kenema nchini Ethiopia katika mechi ya Kombe la Shirikisho kesho wakati KMC itawakaribisha AS Kigali ya Rwanda jijini Dar es Salaam kesho.

Yanga vs Township Rollers

Kwenye Uwanja wa Taifa ambako mashabiki wa Yanga walifurika Jumapili iliyopita katika hafla yao ya kuwatambulisha nyota wao wapya katika kilele cha Wiki ya Mwananchi, mzuka unatarajiwa kuwa wa hali ya juu leo.

Pia Soma

Yanga wana fursa nyingine ya kuujaza uwanja huo unaobeba mashabiki 60,000 kwa ajili ya kusapoti timu yao iliyojengwa upya wakati ikisaka kulipa kisasi.

Yanga mwaka jana ilitolewa kwenye mashindano hayo na Watswana hao kwa jumla ya magoli 2-1.

Katika mchezo wa Dar es Salaam uliofanyika Machi 6 mwaka jana, asilimia kubwa ya wachezaji walioanza katika kikosi hicho na hata ambao walikuwa benchi hawapo hivi sasa ndani ya timu hiyo baada ya kocha Mcongo, Mwinyi Zahera kuunda jeshi jipya kabisa.

Wachezaji kama Obrey Chirwa alijiunga na Azam, Ibrahim Ajib, Gadiel Michael wote wametimkia Simba, Hassan Kessy (Nkana Red Devils), Pius Buswita, Pato Ngonyani na Emmanuel Martin wote walicheza mchezo huo lakini sasa wamejiunga na timu mbalimbali za Ligi Kuu wakati walioanzia benchi na hawapo ndani ya Yanga kwa sasa ni kipa Youth Rostand, Mwinyi Haji, Yusuph Mhilu na Geofrey Mwashiuya.

Wachezaji wanne tu wa kikosi cha kwanza waliocheza mchezo huo mwaka jana ndio wapo na mmoja ndio ana uhakika wa kuanza leo kwenye kikosi cha kwanza ambaye ni Papy Kabamba Tshishimbi wakati Ramadhan Kabwili ataanzia bechi sawa na Said Makapu huku Kelvin Yondani akikosekana kabisa kutokana na kuwa majeruhi.

Hata hivyo, Yanga ya sasa inatarajiwa kufanya makubwa baada ya kusajili majembe ya uhakika katika meneo yote ya uwanja kuanzia kwa kipa hadi washambuliaji.

Imemsajili kipa Farouk Shikalo kutoka Kenya na wakali kibao kama mawinga Patrick Sibomana na Issa Bigirimana, kiungo Maybin Kalengo, mastraika Juma Balinya na David Molinga Ndama ‘Falcao’ na wengine wengi.

Yanga imefika robo-fainali ya Ligi ya mabingwa Afrika mara mbili, 1969 na 1970, mara zote ikitolewa na Asante Kotoko ya Ghana, ikiwamo kutolewa kwa kurusha shilingi baada ya matokeo ya jumla kuwa sare ya 1-1. Mwaka huu inapigania kurudia mafanikio hayo au kufika mbali zaidi.

Wapinzani wao Township Rollers wamecheza Ligi ya Mabingwa mara nne tangu 2011 na kufuzu hatua ya makundi mara moja mwaka 2018 ambapo iliifunga El-Merreikh mabao 4-2 katika hatua ya awali kwa ushindi wa 3-0 nyumbani na kufungwa 2-1 ugenini ikasonga raundi nyingine dhidi ya Yanga.

Noel Mwandila, kocha msaidizi wa Yanga ambayo ilijichimbia kambini Zanzibar kwa siku tatu, amesema wako tayari kwa ajili ya mchezo huo leo hivyo mashabiki wafike kwa wingi uwanjani ili kuwapa sapoti.

Simba vs UD Songo

Simba ambayo imetua kibabe Msumbiji kwa ndege binafsi ya kukodi, itawashukia UD Songo kama mwewe ikiwa na mzuka wa mafanikio ya kufika robo-fainali ya Ligi ya Mabingwa msimu uliopita.

‘Mnyama‘ Meddie Kagere ‘MK14’ ameuanza msimu huu na moto ule ule aliomaliza nao msimu uliopita akipiga ‘hat-trick’ katika ushindi wa 3-1 dhidi ya Power Dynamos ya Zambia katika tamasha la Simba Day Jumanne iliyopita.

Kocha wa Simba, Patrick Aussems, alisema timu yake haitakuwa kamili kwa asilimia 100 kwa sababu kuna baadhi ya wachezaji hakuwa nao mazoezini wakati wakijiandaa na mchezo huo kutokana na kuwa timu ya Taifa, lakini hilo lisiwape hofu mashabiki kwani ushindi ni lazima.

Chanzo: mwananchi.co.tz