Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Tukishawafagilia Aziz Ki na Diarra tujitazame

Djigui Diarra Maliii Tukishawafagilia Aziz Ki na Diarra tujitazame

Fri, 19 Jan 2024 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Timu yetu ya taifa ya Tanzania ‘Taifa Stars’ kwa sasa ipo kule Ivory Coast inakoshiriki fainali za Mataifa ya Afrika (Afcon) mwaka huu ikiwa imepangwa kundi F na timu za Morocco, DR Congo na Zambia.

Hii ni mara ya tatu kwa Taifa Stars kushiriki mashindano hayo ambayo huchezwa kila baada ya miaka miwili ingawa Afcon yenyewe inafanyika kwa awamu ya 34 sasa na awamu ambazo Tanzania imeshiriki ni 1980, 2019 na hii ya sasa.

Wakati Taifa Stars ikicheza mashindano hayo, macho ya mashabiki na wadau wengi wa soka Tanzania yameelekezwa pia kwa baadhi ya nyota wanaocheza soka la kulipwa hapa nchini ambao wanachezea timu tofauti ambazo ni miamba miwili ya soka hapa, Yanga na Simba.

Wachezaji hao ni Stephane Aziz Ki ambaye kwenye mashindano hayo anaichezea Burkina Faso, Djigui Diarra anayeitumikia Mali, Henock Inonga aliyepo kwenye kikosi cha DR Congo na Kennedy Musonda na Clatous Chama ambao katika mashindano hayo wanapeperusha bendera ya Zambia.

Furaha ya wengi ilionekana baada ya juzi Jumanne, Mali na Burkina Faso kuanza vyema fainali hizo kwa kupata ushindi dhidi ya Afrika Kusini na Mauritania katika makundi hayo huku Aziz Ki na Diarra wakiwamo katika vikosi vya kwanza vya timu hizo ambavyo vilipata ushindi ulioziweka kileleni kwenye makundi yao.

Azizi Ki alicheza kwa dakika 86 katika ushindi wa bao 1-0 wa Burkina Faso dhidi ya Mauritania wakati Diarra alicheza kwa dakika zote 90 za ushindi wa Mali wa mabao 2-0 mbele ya Afrika Kusini.

Ushindi huo umetafsiriwa kama mafanikio makubwa kwa soka letu Tanzania hasa kwa ligi yetu ambayo wachezaji hao wanaichezea na baadhi wanatafsiri kama mafanikio makubwa kwetu.

Sio jambo baya kuwaza hivyo lakini tunapaswa kujitafakari kwamba wakati tunashangilia wenzetu hao na sisi tumeweza kutengeneza wachezaji wazuri hapa ndani ambao wanaweza kuwa chachu ya mafanikio kwa klabu zetu pasipo kutegemea wachezaji wa nje kama wanavyozidi kutamalaki hivi sasa katika ligi yetu?

Furaha ya kuwaona Diarra na Aziz Ki wakitesa kwenye Afcon katika timu za mataifa makubwa kisoka Afrika ilipaswa kuendana na kuwa na wachezaji ambao wana ubora kulinganisha na hao ili hata pale wanapoamua kuondoka, timu zetu zisihahe kwenye kusaka warithi.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live