Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Tujifunze haya kutoka uzinduzi wa AFL

AFL Tujifunze haya kutoka uzinduzi wa AFL

Mon, 23 Oct 2023 Chanzo: Mwanaspoti

Juzi Ijumaa kulishuhudiwa uzinduzi wa mashindano ya African Football League (AFL) katika Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam kwa mchezo baina ya Simba na Al Ahly ambao ulimalizika kwa sare ya mabao 3-3.

Mabao ya Sadio Kanoute na Kibu Denis yalitosha kuifanya Simba ilinde heshima nyumbani dhidi ya miamba hiyo ya Afrika ambayo ilipata mabao yake kupitia kwa Reda Slim na Mahmoud Kahraba katika kila kipindi.

Ahly walikuwa wa kwanza kupata bao katika mchezo huo katika dakika ya 45 kupitia kwa Slim aliyeunganisha vyema kwa mguu wa kushoto pasi ya Kahraba baada ya Ahly kufanya shambulizi la kushtukiza langoni mwa Simba.

Mechi ya marudiano baina ya timu hizo itachezwa Oktoba 24 katika Uwanja wa Kimataifa wa Cairo,Misri ambapo mshindi atakutana na timu itakayofanya vizuri katika mechi baina ya Petro Luanda ya Angola na Mamelodi Sundowns ya Afrika Kusini.

Uzinduzi wa mashindano hayo kufanyikia Dar es Salaam ni jambo la heshima kubwa sio tu kwa Simba bali Tanzania nzima kwani umesaidia kuitangaza nchi yetu kutokana na tukio hilo kufuatiliwa na kutazamwa na idadi kubwa ya mashabiki wa soka Afrika na duniani kiujumla.

Ni uzinduzi ambao umekuwa na faida kubwa kisoka mojawapo ikiwa ni ukarabati wa hali ya juu wa Uwanja wa Benjamin Mkapa kuanzia katika eneo la kuchezea na mengineyo na kuufanya uwe katika sura nzuri zaidi ya ulivyokuwa mwanzo.

Yapo mengi ambayo tunaweza kujifunza kutokana na tukio hilo la uzinduzi ambayo kama nchi tukiamua kuyafabnyia kazi, yanaweza kutusaidia katika kusaidia mpira wa miguu kupiga hatua zaidi ya ulipo sasa.

Jambo la kwanza tunaloweza kujifunza na kuanza kulifanyia kazi ni uwekaji mpangilio mzuri wa masuala yanayohusu soka na kuhakikisha kila anayehusika na utendaji kazi anawajibika.

Mpangilio wa tukio la uzinduzi wa AFL ulikuwa wa hali ya juu na kila idara au mtu aliyehusika alitekeleza wajibu wake vizuri jambo lililochangia kwa kiasi kikubwa kulifanya tukio hilo kuwa lenye mvuto na msisimko.

Waliopaswa kuzalisha picha za luninga za tukio hilo, walilazimishwa kupeleka vifaa vyao mapema na kuanza kufanya majaribio huku wakiwa chini ya usimamizi wa karibu wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF).

Hiyo inasaidia kurekebisha changamoto yoyote ambayon inajitokeza kwa wakati tofauti na iwapo jambo hilo lingechelewa kwani changamoto yoyote ingeweza kujitokeza katika muda wa tukio na hivyo kulitia doa jambo ambalo lisingeleta taswira nzuri.

Kuliwekwa utaratibu mzuri wa uingiaji uwanjani kwa mashabiki ambao walikuwa na tiketi halali na kila mmoja alikaa katika eneo sahihi kulingana na daraja la tiketi yake na hata wale waliokuwa na kadi maalum walikaa katika maeneo yao sahihi waliyopangiwa.

Tukio la uzinduzi wa AFL limetufundisha pia suala la kujali muda katika soka letu ambalo lina kundi kubwa la watu ambao wamekuwa hawako makini na suala linalohusu muda.

Waandaji walijitahidi kwenda na muda kwa kila tukio ambalo lilikuwepo katika ratiba kabla, wakati na hata baada ya jambo lenyewe.

Jambo lingine ambalo tunaweza kulichota kupitia tukio la uzinduzi wa AFL ni kuhsehimu haki za wadhamini na kuwapa kipaumbele katika shughuli zilizoambatana ili wapate fursa ya kutosha ya kutangaza huduma na bidhaa.

Katika kila jambo lililohusu AFL mabango yenye nembo za wadhamini wake yalikuwepo na katika maeneo yote yanayoonekana uwanjani, waandaaji wa tukio hilo walihakikisha mdhamini anajitangaza pasipo kuathirika kwa namna yoyote ile.

Tukio la juzi limetuonyesha pia kwamba tunapaswa kulinda na kuendeleza kwa nguvu zote ukaribu na mahaba ya mpira wa miguu ambayo tumekuwa tukionyesha kwa muda mrefu sasa hasa kwa wageni wanaokuja nchini kushiriki matukio tofauti ya soka.

Viongozi wote wakubwa wa soka waliopata fursa ya kuzungumza, walionyesha kufurahishwa na ukarimu na uungwana wa hali ya juu ambao Watanzania tumeuonyesha katika kipindi chote ambacho wamekuwa hapa ili kukamilisha tukio hilo.

Katika kipindi hiki ambacho Tanzania kwa kushirikiana na wenzetu wa Kenya na Uganda tumepata fursa ya pamoja ya kuandaa Fainali za Mataifa ya Afrika (AFCON) 2027, tunapaswa kuendelea na tabia hii ili wale waliotupa nafasi wasione kuwa walikosea na wazidi kupata hamu ya kutupa matukio mengine makubwa zaidi ya soka.

Chanzo: Mwanaspoti