Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Tujaribu kuwaelewa Irankunda, Kamungo

Bernard Kamungoo Vs Messi Tujaribu kuwaelewa Irankunda, Kamungo

Fri, 17 Nov 2023 Chanzo: Mwanaspoti

Baada ya kuibuka kwa habari za vipaji vyao vya kucheza soka katika nchi za Australia na Marekani, Watanzania tukaanza kuwapigia hesabu ndefu vijana Bernard Kamungo na Nestory Irankunda.

Tulivyosikia stori tu kuwa hawa ni watoto wawili wenye vipaji waliozaliwa katika ardhi yetu kule Kigoma hatukutaka kusikia kingine chochote zaidi ya kutamani kuwaona wakiwa na jezi za timu yetu ya taifa.

Na ni sahihi maana hakuna mwanadamu asiyependa kitu kizuri kiwe upande wake. Kamungo ni staa mkubwa pale Marekani akiwa anaichezea FC Dallas huku Irankunda akitamba pale Adelaide United hadi kuvutia na kusajiliwa na Bayern Munich.

Tukaanza harakati za kuhakikisha vijana hao wanachezea Taifa Stars ambayo hivi sasa kiukweli inaonyesha muelekeo mzuri kutokana na mikakati bora ambayo imewekwa na TFF na serikali pamoja na kukua kwa thamani ya soka letu.

Kamungo tulimuita na alikuja hadi hapa nchini akafanya mazoezi na Taifa Stars iliyokuwa ikijiandaa kukabiliana na Niger katika mechi ya kuwania kufuzu fainali za Mataifa ya Afrika (AFCON) zitakazofanyika Ivory Coast lakini hakucheza mechi hiyo kwa kile kinachotajwa ni kutokamilika kwa masuala yake ya uraia.

Ghafla tukasikia ameitwa katika kikosi cha Marekani cha umri chini ya miaka 23 kwa ajili ya kushiriki mashindano ya kuwania kufuzu Olimpiki na tayari ameshakichezea mechi kadhaa.

Huyu Irankunda yeye ndio hatujafanikiwa hata kumleta nchini, tayari ameshachezea timu ya vijana ya umri wa chini ya miaka 17 ya Australia na kuna uwezekano mkubwa akachezea timu yao ya taifa siku chache zijazo.

Bado wana nafasi ya kuichezea Taifa Stars lakini hata ikitokea wakishindwa kufanya hivyo, tunapaswa kuheshimu tu uamuzi wao kwa sababu ni matokeo ya sheria yetu ngumu ya kuzuia uraia pacha ambayo inawaogopesha wachezaji kama hao maana wanajua watapoteza haki za muhimu huko walipo hivi sasa.

Lakini pili watachezea mataifa ambayo yanawapa uhakika wa kushiriki Kombe la Dunia na kufika hata raundi ya 16 bora na hata robo fainali kuliko sisi ambao kufuzu AFCON tu tunahaha.

Chanzo: Mwanaspoti