Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Tujaribu kumuelewa Cafu au tumpuuze?

Caf.jpeg Tujaribu kumuelewa Cafu au tumpuuze?

Sun, 3 Dec 2023 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Wanazaliwa tena wachezaji wazuri wa pembeni kama Cafu wa Brazil? Siamini sana. Mzuri kama alivyo, akiwa na Big G mdomoni, Cafu alikuwa mmoja kati ya mabeki bora wa pembeni kuwahi kutokea katika ulimwengu wa soka.

Wanadai kwamba kila siku vipaji vinatoweka? Yuko wapi Cafu wa Real Madrid? Yuko wapi Cafu wa Manchester United? Yuko wapi Cafu wa Barcelona? Yuko wapi Cafu wa AC Milan. Nyakati zimekwenda wapi?

Lakini wiki iliyopita Cafu mwenyewe alinichekesha kidogo. Ametoa kauli ambayo imetusiganisha mawazo. Cafu anaamini kwamba nafasi ya Brazil kutwaa Kombe la Dunia inapotea kwa kadri wachezaji wake wanavyoamua kwenda England.

Anadai kwamba England wachezaji wanasifiwa sana na kuonekana wana viwango vya dunia wakati ni wachezaji wa kawaida tu. Kauli hii ya Cafu imenishangaza kidogo. Upande mwingine ana hoja upande mwingine hana hoja.

Ni kweli Waingereza wana tabia ya kusifia wachezaji wanaocheza ligi yao, hasa wachezaji wao wa Kiingereza. Hili lipo wazi. Waingereza wana mdomo hasa. Lakini napata shida ninapoitazama historia ya Brazil katika michuano hii ya Kombe la Dunia.

Ni kweli Brazili imetawala Kombe la Dunia. Inaongoza kwa kuchukua. Imechukua mara tano ikifuatiwa na Ujerumani pamoja na Italia ambazo zimechukua mara nne. Brazil imechukua mwaka 1958 pale Sweden, kisha 1962 pale Chile, halafu mwaka 1970 pale Mexico, kisha mwaka 1994 pale Marekani halafu mara ya tano wakachukua mwaka 2002 katika michuano iliyoandaliwa Korea Kusini na Japan.

Tukiachana na mara tatu za mwanzo ambazo walichukua katika michuano miaka iliyokaribiana, Brazil imekuwa na tabia ya kukaa vipindi virefu bila ya kuchukua Kombe la Dunia. Kuanzia mwaka 1970 mpaka mwaka 1994 walikuwa wamekaa miaka 24 bila ya kutwaa.

Baada ya hapo wakaja kuchukua miaka minane iliyofuata mwaka 2002. Kuanzia hapo mpaka leo Brazil haijatwaa tena Kombe la Dunia. Ni takribani miaka 21 sasa. Haiwezi kutushangaza sana kwa sababu waliwahi kukaa miaka 24 bila ya kutwaa Kombe la Dunia.

Katika kipindi hicho cha miaka 24 ambacho walikaa bila ya kutwaa Kombe la Dunia hakukuwa na wachezaji wengi wa kigeni katika soka la Kiingereza. Sio tu wa Wabrazil bali hata wa mataifa mengine hawakuwepo wengi katika soka la Kiingereza. Wachezaji wengi waliokuwa wanacheza Ligi Kuu ya England wakati huo walikuwa wanatoka katika nchi za Kiingereza. Scotland, Wales, Ireland na Ireland Kaskazini.

Kwanini katika kipindi hicho Brazil ilishindwa kutwaa taji la dunia? Bahati mbaya sio tu kutwaa taji, lakini walishindwa hata kufika fainali. Mwaka 1994 walifika fainali na kutwaa kwa matuta dhidi ya Italia. Wote tunazikumbuka fainali zile za Romario na Bebeto na penalti iliyopaa ya Roberto Baggio.

Wachezaji wengi wa kigeni walianza kutua England kuanzia mwaka 1992 baada ya Ligi Kuu ya England kufanya mabadiliko makubwa ya kiundeshaji na kimfumo ambapo sasa Ligi hiyo ilikwenda kuwa Ligi Kuu badala ya daraja la kwanza kama ilivyokuwa inafahamika awali.

Hata hivyo, kuanzia hapo mpaka sasa hakuna wachezaji wengi wa Brazil ambao wametua England na kuwa tegemeo katika mpira wa Brazil. Mwaka 2014 nilikuwepo Brazil wakati walipoandaa fainali za Kombe la Dunia na kuchapwa mabao saba na Wajerumani.

Katika kikosi kile cha Brazil kulikuwa na wachezaji watatu tu walioanza wakitokea katika Ligi Kuu ya England. Kikosi kilichoanza kilikuwa na Julio Cesar, Maicon, David Luiz, Dante, Marcelo, Luiz Gustavo, Fernandinho, Hulk, Bernard, Fred na Oscar.

Hapo ni David Luiz, Oscar na Fernandinho tu ndio ambao walikuwa wanacheza katika Ligi Kuu ya England. Wengine walikuwa wanacheza katika ligi nyingine na cha kustaajabisha wengine walikuwepo pia waliokuwa wanacheza katika ligi ndogo.

Achana na michuano mingine ya Kombe la Dunia iliyopita hapo katikati lakini michuano ya karibu zaidi ya Kombe la Dunia imefanyika mwaka mmoja kamili uliopita pale Qatar. Brazil walitolewa kwa matuta na Croatia katika pambano ambalo lilianza huku Brazil ikiwa na wachezaji wanne wanaocheza Ligi Kuu ya England.

Hao ni Richarlison, Alisson Becker, Raphinha na Thiago Silva. Wengine na walioingia baadae wote hawachezi England. Kulikuwa na timu zenye wachezaji wengi wanaocheza Uingereza ambao walikwenda mbali zaidi katika michuano hiyo.

Lakini hata mwaka 2018 wakati wa fainali za Kombe la Dunia pale Russia Waingereza wenyewe walifika mbali zaidi kuliko Wabrazil. Waingereza walifika nusu fainali wakati Brazil iliishia robo fainali. Brazil yenyewe ina matatizo makubwa kuliko hili hapa ambalo Cafu ametuletea.

Ni kweli Hispania kuna mpira mzuri lakini hauwezi kuondoa ukweli kwamba kwa sasa ligi mbili kubwa duniani ni England na Hispania. Mchezaji akicheza humo ataimarika maradufu kuweza kuiwakilisha timu yake ya taifa hasa kama anacheza katika timu kubwa.

Kama Arsenal na Manchester City zina nafasi kubwa zaidi ya kutwaa Ligi ya Mabingwa wa Ulaya msimu huu, unataka mchezaji wako acheze wapi zaidi? Sidhani kama Cafu yupo sahihi katika hili. Kitu ambacho Cafu anasahau ni ukweli kwamba wachezaji kama yeye hawazaliwi tena Brazil.

Ukitazama kikosi cha Kombe la Dunia cha mwaka 2002 pale Korea Kusini na Japan, Brazil ilikuwa na watu kama yeye ambaye alikuwa nahodha, Ronaldinho, Ronaldo de Lima, Kaka, Rivaldo, Roberto Carlos na wengineo. Hawazaliwi tena kirahisi wachezaji kama hawa.

Taifa lake limeshindwa kutuletea wachezaji mahiri kiasi cha kwamba kwa miaka 15 Lionel Messi na Cristiano Ronaldo walikuwa wanabadilishana tuzo ya mwanasoka bora wa dunia. Lakini hata sasa wameondoka bado tuzo haitazamiwi kwenda kwa mchezaji wa Brazil.

Vinicius Jr itabidi apambane kweli kweli kurudisha tuzo nyumbani Brazil mbele ya Erling Haaland na Kylian Mbappe. Huu ndio ukweli ambao Cafu inabidi aumeze. Hawazaliwi tena wachezaji kama yeye na hilo ni tatizo kubwa kwa Wabrazili. Asitafute mchawi.

England inaweza kuwa tatizo kwa Wabrazili lakini hata katika ligi nyingine hakuna Wabrazili wakubwa wanaotamba. Wengi wao ni wachezaji wa kawaida tu ambao wanaishia katika hadhi za kawaida tu lakini hawawezi kumtisha Mbappe wala Haaland.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live