Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

TV

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Tuendelee na vijana wa Amrouche au tuwatose?

Vijana Stars Tuendelee na vijana wa Amrouche au tuwatose?

Sun, 28 Jan 2024 Chanzo: Mwanaspoti

Hotuba ya Rais wa Shirikisho la Soka la Cameroon, Samuel Eto’o kwa wachezaji wa timu ya taifa hilo baada ya kupoteza mchezo wa pili wa hatua ya makundi ya fainali za Mataifa ya Afrika (Afcon 2023) ilikuwa inatuma salamu kwa vyama vingine vya soka vya Afrika.

Sehemu kubwa ya hotuba yake ilijikita katika kulaumu wachezaji kwa kutoonyesha uzalendo wa kuipigania nchi yao hadi tone la mwisho la damu, tofauti na enzi zao. Lakini akasema sehemu kubwa ya wachezaji wa kikosi hicho wamezaliwa Ulaya na wengi hawajachezea hata klabu za Cameroon, hivyo hawasikii uchungu kwa taifa lao.

Eto’o, mshambuliaji aliyechezea timu ya vijana ya Real Madrid na baadaye kwenda Real Malorca, Barcelona na Inter Milan, aliwaambia wachezaji hao kuwa mambo yatabadilika baada ya fainali za mwaka huu, lakini hakueleza yatabadilikaje.

Mafanikio ya Cameroon, nchi ya kwanza ya Afrika kuvuka hatua ya makundi ya fainali za Kombe la Dunia, yamekuwa yakitegemea sana wachezaji walio Ulaya, baadhi wakiwa ni wale wanaoitwa timu ya taifa kwa kuangalia kama wana asili yoyote ya taifa hilo la Afrika Magharibi.

Wengi wao huenda Cameroon wakati wanapoitwa kuichezea timu ya taifa inapokuwa na mechi nyumbani, lakini inapokuwa na mechi nje ya nchi, hukatiwa tiketi za ama kukutana Amsterdam na baadaye kuelekea huko wanakocheza mechi na wakimaliza hutimkia kwenye klabu zao bila ya kurudi nchini kwao.

Ni heshima kuichezea timu ya taifa na ni mafanikio kwa mchezaji iwapo timu hiyo itafuzu kucheza fainali kama hizo za Afcon au Kombe la Dunia, lakini tatizo inakuwa ni kupigania bendera.

Kwa viongozi wa soka wa nchi, mafanikio ya timu ya taifa yenye wachezaji ambao chama cha soka cha nchi hakijahusika hata chembe kuwaandaa, kwao ni mafanikio hata kama soka katika nchi yao iko chini.

Ndio maana nchi za Afrika Magharibi si tishio katika mashindano ya klabu ya Afrika. Ni mara chache sana zimeweza kutingisha soka la Afrika kwa ngazi ya klabu. Ni jambo la kushangaza kwamba Enyimba ndio klabu ya kwanza ya Nigeria kutwaa Kombe la Ligi ya Mabingwa Afrika ilipolitwaa kwa mara ya kwanza mwaka 2003 na baadaye 2004. Kabla ya mfumo wa sasa, Shooting Stars na Iwuanyanwu ziliwahi kubeba.

Wanachofanya viongozi wengi wa soka wa nchi hizo zenye wachezaji wengi barani Ulaya, ni kuhakikisha wanaweka ada kubwa ya mechi za kirafiki, kuandaa mechi za kirafiki dhidi ya mataifa makubwa na kuandaa kambi ya siku tatu au nne barani Ulaya kabla ya kucheza mech Afrika au nje ya bara hili.

Kwenye orodha ya ubora, nchi ambayo imecheza mechi za kirafiki dhidi ya Ufaransa, Italia au England huku ikishinda mechi zake za mashindano barani Afrika, itakuwa juu kwa sababu ya fomula inayotumiwa kupanga nchi katika orodha ya ubora ya Shirikisho la Kimataifa la Soka (Fifa).

Lakini nchini kwao soka linaporomoka na kinachosaidia wachezaji wao kwenda Ulaya, ukiacha wale waliozaliwa na kukulia barani humo, ni shule za soka ambazo baadhi zina ushirikiano na klabu kubwa kama Arsenal na Ajax Amsterdam. Mafanikio hayo yanaweza kuja usiku mmoja tu.

Yaani mteue kocha kama Abdoul, Yule aliyeiongoza Comoro mwaka 2019 na mwaka huu Mauritania, mpe fedha za kutosha kwenda kusaka wachezaji wenye asili ya taifa lenu, hata kama asili hiyo ni ndogo sana. Akiwakusanya tu, nchi inafanya maajabu kama Comoro na Mauritania.

Lakini njia hii, ambaye pia kocha wetu Adel Amrouche ameanza kuitumia haiwezi kusaidia maendeleo ya taifa hili katika soka. Timu ya taifa itafanya vizuri mashindanoni lakini mafanikio hayataakisi maendeleo ya nchi kisoka na wala hayataambukiza kwenye soka la ndani.

Sifa zitabakia kwa kocha, huku viongozi wa soka wa nchi wakitumia kisiasa mafanikio yatakayopatikana.

Ndio maana haikuwa ajabu kwa Amrouche kuwaacha chipukizi kama Sopu na Clement Mzize, ambao wanaweza kuwa hazina kubwa ya nchi na kwenda kuhangaika na wachezaji kama Tarryn.

Hawa watasaidia kama tumejenga soka letu vizuri, hivyo kutakiwa na timu yetu pale tu watakapokuwa na viwango kuzidi wachezaji waliokuzwa ndani.

Hapa ndipo mataifa ya Kiarabu yanapotushinda. Programu zao za maendeleo ni nzuri na kanuni zao za kulinda wachezaji wa ndani ni kali na hivyo wanakuwa na klabu zinazoshindana kwa ufanisi barani Afrika na pia timu ya taifa zenye ushindani na ndio maana nchi za Afrika Kaskazini zinaongoza kwa kutwaa ubingwa wa ngazi za klabu na ubingwa wa Afcon.

Si kwa bahati mbaya, bali kwa mipango bora na imara ya kukuza soka la ndani kuanzia ngazi ya chini.

Mafanikio ya timu ya taifa ni lazima yaakisi maendeleo ya soka la ndani. Kuanza kuhangaika na wachezaji wenye chembechembe za asili ya Tanzania bila ya mipango ya soka la ndani, ni kuua maendeleo ya chipukizi wetu.

Tutakuwa watu wa ajabu kushangilia ligi iliyojaa wachezaji wageni, huku tukifurahia timu ya taifa yenye wachezaji waliotafutiwa chembechembe za uraia wa Tanzania.

Wapo wanaosema wachezaji wageni wanaleta burudani na wamesaidia kuipandisha hadhi ligi yetu. Lakini vipi Misri, Morocco, Tunisia na Algeria? Nazo si zina wachezaji wageni? Lakini kwa nini zifanikiwe kwenye ngazi ya klabu na timu za taifa? Ni kwa sababu zimeruhusu wachezaji wa kigeni kwa tahadhari na kulinda wachezaji wazawa kwa akili, huku zikiwa na mipango kabambe ya maendeleo.

Wakati huu tunaelekea kuandaa fainali za Mataifa ya Afrika (Afcon 2027) ni muhimu sana kujiangalia upya na kwa tafakuri kubwa. Tunataka njia anayoitumia Amrouche, au wanayotumia wenzetu wa Afrika Kaskazini. Tuna miaka miwili ya kujiweka sawa.

Mimi ukiniuliza, nitakwambia kwa sasa tuweke viwango vya kuchukua wachezaji wenye asili ya Tanzania, lakini nguvu kubwa tuiweke katika wachezaji wa ndani na kocha aelewe hilo. Mafanikio ya kutumia wachezaji wenye asili ya Tanzania, ni bandia!

Chanzo: Mwanaspoti