Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Tuchel ni nabii asiyekubalika kwao, ajipange

Thomas Tuchel Ban Tuchel ni nabii asiyekubalika kwao, ajipange

Wed, 24 Jan 2024 Chanzo: Mwanaspoti

Ni kweli Thomas Tuchel hakubaliki huko Ujerumani. Licha ya kuwa kocha wa daraja la juu anayeifundisha miamba ya soka nchini humo na mabingwa kihistoria, Bayern Munich, ni kazi bure.

Mwenyewe aliwahi kusema anaona anakubalika zaidi England kuliko nchini kwao. Yupo sahihi. Unajua kwa nini?

Achana na ule usemi wa nabii hakubaliki kwao. Ni maajabu gani amefanya hadi akubalike?

Tumtazame Xabi Alonso. Kwa nini anakubalika Ujerumani ambako sio nchini kwake. Utapata jibu la Tuchel.

Xabi anakubalika Ujerumani kutokana na kazi kubwa na nzuri anayoifanya. Ameifanya Bayern Leverkusen kutisha msimu huu na inaongoza msimamo wa Bundesliga na haijapoteza mchezo hata mmoja hadi sasa.

Ndiyo timu pekee kwenye zile ligi tano bora Ulaya ambayo bado haijapoteza, unadhani hiyo ni kawaida? anastahili pongezi. Kwa alichokifanya kama kocha hata kama asipochukua ubingwa atabaki kwenye mioyo ya mashabiki wa timu hiyo.

Sawa, Ujerumani sio nyumbani kwa Alonso, lakini vipi kuhusu Pep Guardiola mbona anakubalika kwao Hispania?

Usisahau alichofanya akiwa na Barcelona kabla ya kwenda Ujerumani. Sasa yupo zake England akiwa na Manchester City. Hata hivyo, huwaambii kitu mashabiki wa soka Hispania kuhusu Pep.

Turudi kwa Tuchel. Bayern Munich ni moja ya timu bora Ulaya. Ina wachezaji wa daraja la juu. Hata hivyo, msimu huu mwenendo wao sio mzuri. Hauwafurahishi mashabiki wa timu hiyo. Kuna shida.

Msimu uliopita Tuchel aliiongoza Bayern Munich kutwaa Ligi Kuu Ujerumani lakini ilikuwa kwa tabu sana, wababe hao walikuwa wakisuasua. Sio ile Bayern iliyozoeleka.

Sasa unawezaje kuwa kwenye mioyo ya mashabiki kwa staili hiyo? Tuchel anatakiwa kufanya kazi. Anatakiwa kuibadili Bayern kwa kuendelea kutawala kwenye soka la Ujerumani huku wakiwa tishio pia Ulaya.

Tuchel ankumbukwa sana na mashabiki wa Chelsea. Anabaki mioyoni mwao. Kwa nini? Aliwapa taji la Ligi ya Mabingwa Ulaya. Ulikuwa ni msimu wake bora kwenye kufundisha soka na alimzidi kete Guardiola kwenye fainali.

Aliondoka Chelsea wakati moyo ukimuuma lakini hakuwa na jinsi muda wote makocha huwa tayari na hutegemea hilo kulingana na kazi zao zilivyo, aliamua kupumzika kidogo kabla ya kurejea kwenye majukumu hayo.

Ili kuwa kwenye mioyo ya mashabiki ni rahisi. Wape wanachotaka. Sio kuwa nyumbani.

Alonso aliikuta Leverkusen ikiwa miongoni mwa timu zilizopo chini kwenye msimamo wa Bundesliga, kwa bajeti ndogo ameifanya kuwa tishio na wameweka rekodi kibao za kibabe.

Uhitaji wa mashabiki wa Bayern na uongozi kwa jumla ni ufalme wa Ulaya, kutwaa Bundesliga na vikombe vingine vya ndani ni jambo la kawaida na haliwezi kukufanya kuwa midomoni mwao.

Tuchel anaweza kukubalika na kupendwa mno Ujerumani kama ilivyo England kama ataiongoza Bayern kutwaa Ligi ya Mabingwa Ulaya. Ndicho mashabiki wanataka. Hata Pep lilimshinda licha ya kuiofanya timu kucheza soka safi. Kaondoka. Tuchel kazi kwake. Mashabiki watamkubali akileta Kombe la Ligi ya Mabingwa. Mengine wameyazoea.

Chanzo: Mwanaspoti