Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Tuchel anatabasamu tu kuhusu harry Kane

Kane Picha Data Tuchel anatabasamu tu kuhusu harry Kane

Sun, 23 May 2021 Chanzo: www.mwanaspoti.co.tz

LONDON, ENGLAND. MWENYE kisu kikali ndo atakula nyama. Straika, Harry Kane atakwenda wapi msimu ujao, Stamford Bridge, Etihad au Old Trafford.

Supastaa Kane ameiambia klabu yake ya Tottenham Hotspur kwamba anataka kuondoka wakati dirisha lijalo la uhamisho wa majira ya kiangazi litakapofunguliwa.

Chelsea, Manchester City na Manchester United zote zimeonyesha dhamira ya dhati ya kunasa huduma ya straika huyo wa kimataifa wa England tangu alipotangaza anataka kuhama kwenda kujiunga na timu itakayompa nafasi ya kubeba mataji kabla ya nyakati hazijaanza kumtupa mkono.

Kocha wa Chelsea, Thomas Tuchel alipoulizwa kuhusu mpango wake wa kumnasa Kane kwenye dirisha lijalo la uhamisho wa majira ya kiangazi, hakusema chochote cha zaidi na alitabasamu tu.

Kane alipopasua jibu kwamba anataka kuondoka, hapo hapo ametaka kupata nafasi ya kuzungumza na mwenyekiti wa Spurs, Daniel Levy kujadili na kukubaliana juu ya hatima yake ya maisha ya baadaye.

Man United na Man City zinatajwa kuongoza kwenye mbio za kunasa huduma ya mshambuliaji huyo wakichuana jino kwa jino, lakini Chelsea nao wanakwenda kimyakimya kwenye mchakamchaka huo wa kunasa huduma ya Kane.

Kocha wa Chelsea, Tuchel hakutaka kusema kitu kama timu yake ina dhamira ya kusaini huduma ya Kane, lakini kitendo chake tu kilizungumza kwa sauti kubwa kuliko maneno wakati alipoulizwa swali hilo.

Ni kama vile alifahamu kile ambacho ataulizwa, lakini hakuthibitisha wala kukanusha mpango huo wa kunasa saini ya Kane, mwenye mabao 22 kwenye Ligi Kuu England msimu huu, ambayo leo Jumapili itafika tamati.

Ni jambo la wazi kabisa, kocha wa klabu yoyote ile angependa kuwa na huduma ya mchezaji mwenye kiwango cha kama Kane, hasa inapofahamika kwamba huduma ya mchezaji huyo inapatikana.

Kutokana na hilo, Tuchel hakutaka kujifungia milango kuwa yupo kwenye mipango ya kunasa saini ya mkali huyo.

Tuchel akiwa mwenye tabasamu pana, alisema: “Kama utampata kocha yeyote duniani atakwambia hatapenda kuwa na Harry Kane kwenye timu yake, nipigie.

“Ningependa sana nipate muda wa kuzungumza na yule mtu anipe mbinu zake za kufunga na kushambulia.

“Kila mtu anampenda Harry Kane, lakini lazima tuwe wakweli kwenye hili, yeye ni mchezaji wa Tottenham.

“Ana mkataba mrefu kwenye timu hiyo na hatuwezi kuhusika kwenye mikutano ya waandishi wa habari kuzungumzia hilo au kufanya utovu wa nidhamu wowote juu ya jambo hilo.”

Hata hivyo, Tuchel alisema maneno mengi juu ya Kane kuliko kocha wa Man City, Pep Guardiola - ambaye kikosi chake kinapewa nafasi kubwa zaidi ya kunasa saini ya Kane kwe-nye dirisha lijalo.

Guardiola alipoulizwa na waandishi kuhusu Kane alijibu hivi: “Swali jingine. Yeye ni mchezaji wa Tottenham Hotspur, tafadhali.”

Chanzo: www.mwanaspoti.co.tz