Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Tshishimbi aeleza mkataba mnono aliopewa na Simba

100498 Pic+shishimbi Tshishimbi aeleza mkataba mnono aliopewa na Simba

Sat, 28 Mar 2020 Chanzo: mwananchi.co.tz

KIUNGO nyota na nahodha wa Yanga, Papy Kabamba Tshishimbi jana alitua klabuni Jangwani na kuteta na viongozi lakini akaweka wazi kwamba mkwanja uliopo kwenye mkataba alioletewa nyumbani na Simba ni balaa.

Staa huyo ameliambia Mwanaspoti kuwa Simba wamempelekea mkataba wa kazi nyumbani kwake na una ofa nzuri lakini Kocha Luc Eymael amesisitiza kwamba mchezaji huyo raia wa DR Congo haondoki Jangwani.

Akizungumza na Mwanaspoti jana, Tshishimbi alisema mkataba wake umebaki miezi minne Jangwani lakini atawapa kipaumbele kwavile amefanya nao kazi vizuri sana na tayari amefanya mazungumzo na bosi wa GSM, Hersi Said, kabla ya jana kutua Jangwani saa 6 mchana na kukaa na viongozi kwa muda wa dakika 30 kuwaeleza hali halisi kisha akasepa zake mtaani.

“Yanga nimeitumikia kwa miaka mitatu sasa ni lazima uwe na heshima kwa klabu ya namna hiyo kabla ya kufanya uamuzi mwingine wowote, ndio maana nimeanza kuwapa wao nafasi ya kuongea na mimi, tumezungumza na Hersi (Said) lakini hatukumalizana, tusubiri wiki kama mbili kutoka sasa kipi kitaendelea kwa kuwa huwa sipendi kufanya uamuzi wakati mkataba umemalizika kabisa,” alisema Tshishimbi.

SIMBA WAMEENDA

Tshishimbi alisema presha ya Simba katika kusaka saini yake imekuwa kubwa ambapo mara kadhaa amelazimika kukwepa kuonana na watu nje ya ghorofa analoishi ambao kila akipokea simu zao wanadai wamekwenda na mkataba kutoka Simba.

Pia Soma

Advertisement
“Kuna wakati unaona gari ukipokea simu unaambiwa kuna mzigo wameleta na hao ni Simba, presha imekuwa kubwa sana lakini mimi sio mtu wa kutaka kufanya uamuzi kwa haraka, nimeshajua ni kiasi gani cha fedha wanataka kunipa lakini kwasasa acha kwanza.

“Tusubiri huu muda niliokwambia upite tuone kipi kitaendelea ndio maana siku zote nimekuwa nikikataa kusubiri mkataba ufike kama hapa unaweza kufanya uamuzi wowote,” aliongeza mchezaji huyo ambaye kila Alhamisi ana safu yake kwenye gazeti hili la Mwanaspoti.

EYMAEL AJA JUU

Kocha wa Yanga, Luc Eymael ambaye yuko likizo kwao Ubelgiji, anasema anafahamu Tshishimbi, David Molinga na Tariq Seif mikataba yao inamalizika mwisho wa msimu huu lakini amewaambia viongozi wasimuachie.

“Unajua mchezaji kama Tshishimbi ambaye yupo katika kiwango bora halafu anamaliza mkataba na timu moja lazima klabu nyingine zitamtaka, lakini kwangu nimeongea na mchezaji mwenyewe na kumueleza asiende kokote kwani Yanga watampatia vitu ambavyo anahitaji,” alisema Eymael.

“Kwa ambavyo nimekuwa nikiwasiliana na viongozi pamoja na GSM nina imani kubwa Tshishimbi atabaki, nimemwambia atulie kwani bado ninamhitaji. Nimezungumza naye, ila Tshishimbi mwenyewe ndio ana uamuzi wa mwisho kubaki Yanga kama ambavyo nahitaji au kwenda katika timu nyingine ambazo zinamuhitaji kama Simba na Azam,” aliongeza kocha huyo.

Mwanaspoti linajua pia kwamba, Tshishimbi ana mkataba wa Yanga mkononi lakini hajausaini akishinikiza dau liongezwe.

MSIKIE JUMA ABDUL

Beki wa kulia wa Yanga, Juma Abdul alisema; “Kila mtu ana mipango yake kimaisha, ana familia na uamuzi binafsi, huenda ameangalia maslahi kwa sababu mpira ni kazi ingawa kikawaida napenda kuona tunaendelea kuwa pamoja Yanga. Binafsi naheshimu uamuzi wa mtu.”

Huu ni msimu wa tatu kwa Tshishimbi kuichezea Yanga tangu aliposajiliwa kwenye dirisha dogo la Januari, 2018 akitokea Mbabane Swallows ya Eswatini.

Tshishimbi ana uwezo wa kucheza kiungo wa kati na kiungo mkabaji kwa kiwango cha juu na aliwavutia mashabiki tangu siku ya kwanza alipoupiga mwingi dhidi ya Simba mwaka huo.

WAANDISHI: TOBIAS SEBASTIAN, KHATIMU NAHEKA, CLEZENCIA TRYPHONE NA DORIS MALIYAGA

Chanzo: mwananchi.co.tz