Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Try Again aondoke Simba, ili aje nani?

Try Again Hj Try Again aondoke Simba, ili aje nani?

Mon, 13 Nov 2023 Chanzo: Mwanaspoti

Salim Abdallah Muhene. Huku mtaani anafahamika zaidi kama Salim ’Try Again.’ Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya Simba. Aliteuliwa kwa mara ya pili mwaka huu na bilionea na mwekezaji wa klabu hiyo, Mohamed Dewji ‘MO’ katika nafasi hiyo.

Kwa mujibu wa katiba ya Simba inayotumika sasa, ndiye kiongozi mwenye mamlaka zaidi ndani ya klabu. Ndiye anayeitisha vikao vya bodi na kuvisimamia. Ndiye mtu wa juu zaidi katika uongozi wa klabu ya Simba. Ni yeye.

Huyu Murtaza Mangungu ambaye ni mwenyekiti wa Simba, kwenye vikao vya bodi ya wakurugenzi ni kama mjumbe tu. Ndiyo katiba ya Simba iko hivyo. Mwenyekiti wa bodi anatoka upande wa mwekezaji na kwa sasa ni Try Again.

Nimeona maneno mengi mitaani yanaendelea baada ya Simba kupoteza mchezo wa dabi kwa mabao 5-1. Ni kipigo kikubwa zaidi kwa Simba kutoka kwa watani zao tangu mwaka 1968. Ni miaka mingi kwelikweli. Nini kimetokea? Ni swali ambalo linawachanganya Wanasimba wengi.

Baada ya kipigo hicho, mabosi wa Simba walikutana na kuamua kumfurusha Kocha Roberto Oliveira ‘Robertinho.’ Yalikuwa ni maamuzi sahihi kabisa. Kocha anayefungwa tano kwenye dabi hapaswi kuendelea kusalia nchini kwa hata siku moja zadi. Anapaswa kufukuzwa tena kwa aibu.

Ni bora kupoteza mechi tano za Ligi Kuu, kuliko kufungwa tano na mtani wako. Robertinho hawezi kuelewa machungu aliyoacha nchini. Watu wa Simba watasemwa na kusimangwa kwa miaka nenda rudi bila kujali wanafanikiwa vipi. Machungu haya yatakwisha siku wakishinda kwa kishindo kwenye dabi.

Baada ya kocha kufurushwa, bado baadhi ya Wanasimba wameendelea kupiga kelele kutaka baadhi ya viongozi wa Simba wajiuzulu kutokana na kipigo hicho. Wakaanza na Murtaza Mangungu. Mwenyekiti waliyemchagua kwa kura zao. Huyu ndiye anawawakilisha katika bodi.

Kosa la Mangungu ni lipi? Baadhi ya wanachama wanadai kuwa uongozi wa timu yao sio imara ndio sababu timu imefungwa mabao mengi kwenye dabi. Yawezekana wana hoja, lakini sidhani kama zinatosha kusema Mangungu ajiuzulu.

Baada ya hapo, wengine wakasema Mwenyekiti wa Bodi, Try Again naye aachie ngazi katika nafasi yake kutokana na matokeo ya dabi. Nikawasikiliza na kucheka kwa sauti.

Yawezekana watu wengi wa Simba hawafahamu hata namna timu yao inavyoendeshwa. Kwanza, Try Again hawajibiki moja kwa moja kwa wanachama. Ni mwakilishi wa mwekezaji wa klabu, Mohamed Dewji. Ndiye aliyemteua na ndiye mwenye mamlaka ya kumwajibisha.

Yawezekana katiba ya Simba haikuweka hayo mamlaka ya mwekezaji kumtoa mtu aliyemchagua. Labda ndio sababu hata Dewji mwenyewe akiona haridhishwi na vitu anaishia kulalamika katika mitandao ya kijamii, badala ya kuwawajibisha watu aliowateua mwenyewe.

Ila ukweli ni kwamba, kila nikitazama ile Bodi ya Wakurugenzi ya Simba, hakuna mtu wa kuvaa viatu vya Try Again. Ndio sababu Dewji alipotaka kuachia nafasi hiyo alimchagua.

Kuwa Mwenyekiti wa Bodi ya Simba sio jambo jepesi hata kidogo. Kwanza lazima uwe unajiweza kifedha. Kitu ambacho Try Again anacho. Ni mfanyabiashara aliyefanikiwa. Ana utajiri wa kutosha, japo sio kama MO Dewji.

Kwanini nasema uwe unajiweza? Nitakwambia. Namna Simba na Yanga zinavyoongozwa, fedha ndiyo kila kitu. Kuna wakati mambo yanakwama, na mnapaswa kutoa fedha mfukoni ili yaende.

Sasa kama mwenyekiti hana fedha, atawaambia nini wajumbe? Hakuna.

Ndio sababu kuna wakati Dewji hayupo, na timu haina fedha, Try Again anatoa fedha zake mfukoni kuokoa jahazi. Nani anaweza kuvaa viatu vyake kirahisi? Kwa waliopo Simba kwa sasa hakuna. Labda Musley Ruwei. Ila huyu hapendi mambo ya uongozi wa juu.

Sasa wakati huu mishahara tu pale Simba inafikia zaidi ya Sh 400 milioni kwa mwezi, lazima awepo mtu imara kiuchumi. Kumbuka kwamba Dewji anatoa fedha, ila siyo kila wakati. Kuna muda anaweza kutingwa na mambo yake ya biashara na timu inahitaji fedha. Nani ataokoa jahazi?

Mashabiki wanaona timu inafanya vizuri tu uwanjani, lakini nyuma ya pazia kuna watu wanaumia. Kuwa Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi Simba lazima utoboke. Kwa msimu unaweza kushindwa kuhesabu hata kiwango cha fedha ulichotumia.

Huyu Try Again tunayemzungumza hapa, ndiye jicho la Simba. Anatatua matatizo ya wachezaji, watendaji wa timu na bado wao mashabiki wanakwenda kwake na matatizo yao binafsi ya kifamilia awasaidie.

Ukifika ofisini kwake Lumumba utaelewa vizuri. Utakuta watu wa Simba kibao wanaenda kuomba chochote.

Kwenye minajili kama hii bado kuna watu wanaamini kama Try Again akitoka, timu itafanya vizuri. Ni vyema mtu akisema Try Again akitoka, aje nani?

Zama hizi za soka kuhitaji fedha nyingi zinahitaji matajiri. Wale viongozi wenye kelele nyingi wa zamani wa kushinda kwenye vijiwe vya kahawa hawawezi hata kidogo kuendesha mpira huu wa kisasa.

Ndiyo maana pale Yanga wamemweka Hersi Said Injinia. Huyu ana fedha. Ni tajiri. Halafu anaaminiwa na mfadhili wa timu, Gharib Said Mohamed. Kwanini? Kwa sababu soka la sasa linahitaji fedha na sio maneno.

Mwisho niseme kuwa Try Again ana sifa nyingi za kuwa kiongozi bora. Ni mwadilifu, anaweza kusimamia wenzake na amekuwepo Simba kwa zaidi ya miaka 20 sasa.

Unapata watu mtu mwingine kama huyo katika nafasi yake?

Chanzo: Mwanaspoti