Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Tripu hii, mtakoma

Pape Ousmane Sakho Mapinduzi.jpeg Pape Ousmane Sakho

Sun, 1 Jan 2023 Chanzo: Mwanaspoti

Achana na rekodi za nyuma michuano ya Kombe la Mapinduzi ilipoasisiwa mwaka 1965 ama zile za 1998, 2001, 2002 na 2004 ambapo timu za Zanzibar zilikuwa zikicheza zenyewe michuano hiyo, tangu 2007 michuano ilipoanza kutambulika rasmi timu za Zenji zimehenyeka kinoma.

Ndio, timu za visiwani humo zimekuwa kama wasindikizaji kwa kushindwa kufurukuta mbele ya wababe kutoka Tanzania Bara ama wageni waalikwa, kwani rekodi zinaonyesha ni mara moja zilivyoweza kufanya kweli kwa kubeba ubingwa, kazi hiyo ikifanywa na Miembeni iliyobeba mwaka 2009.

Pia rekodi zinaonyesha tangu mwaka 2012, pale Jamhuri Pemba ilipofika fainali na kufungwa na Azam, hakuna timu yoyote ya visiwani Zanzibar iliyowahi kutimba hatua hiyo, achilia mbali kubeba tena ubingwa, kwani baada ya Miembeni kuifunga KMKM mabao 2-0 2009, msimu uliofuata Ocean View ilitinga fainali lakini ikafungwa bao 1-0 na Mtibwa Sugar.

Ndipo 2012, ikawa zamu ya Jamhuri kutesti zali, lakini nayo haikufua dafu na tangu hapo hakuna tena timu ya visiwani iliyofika fainali ama kubeba taji hilo na siri imefichuka juu ya unyonge huo wa timu za Zanzibar ambazo msimu huu zinawakilishwa na timu sita zilizochimba mkwara msimu huu kazi ipo. Wakati michuano hiyo inaanza leo, Mwanaspoti imezungumza na Mwenyekiti wa Kamati ya Michuano hiyo na baadhi ya makocha na kuanika sababu zinazozikwamisha timu za visiwani hivyo.

NJAA KALI

Inaelezwa moja ya sababu ya timu za Zanzibar kutofautiana na zile za Bara, licha ya kuwa za nchi moja ni njaa kali kwa timu za visiwani na mkwanja mnene kwa zile za Bara zinazofanya usajili wa kishindo kwa fedha nyingi yaani usajili wa mchezaji mmoja Bara unaweza kuwa ni bajeti ya mwaka mzima ya timu tatu za Zenji ukizijumlisha pamoja.

Ukiachana na hilo, mshahara wa staa wa Bara pia unaweza ukalipa wachezaji wote wa timu moja ya Zanzibar kama inavyoelezwa na kigogo wa maandalizi hayo.

Mwenyekiti wa Kamati ya Mashindano ya Kombe la Mapinduzi, Khamis Abdallah Said kwanza anasema maandalizi kwa ajili ya mashindano hayo yamekamilika kwa asilimia 100 na wanachosubiri ni timu kuanza kuwasili kuanzia leo.

“Kila kitu kimekwenda kama kilivyopangwa kwa asilimia zote tumekamilisha maandalizi ikiwemo hoteli ambazo timu zitafikia, viwanja na vitu vingine vingi. Said anasema kihistoria michuano ya Mapinduzi ilianza mwaka 1965, baada tu ya Mapinduzi ya Zanzibar Januari 12, 1964.

“Serikali ya wakati huo ilifanya mashindano ya Mapinduzi kwa mara ya kwanza mwaka 1965 na timu kutoka Dar es Salaam ndio ilichukua kombe baadaye yakapotea na kurejea tena miaka 12 iliyopita,” anasema Said.

Anafafanua baadaye michuano ilienda ikiboreshwa zaidi hadi kupata msisimko mkubwa kuanzia 2007 hadi leo na kuifanya iwe ni kati ya michuano inayofuatiliwa kwa karibu na wadau wa soka wa Ukanda wa Afrika Mashariki baada ya michuano ya Kombe la Kagame.

Kuhusu kukwama kwa timu za Zanzibar, Said anasema ukosefu wa fedha na udhaifu wa ligi ndiyo chanzo kikubwa cha kutofanya vizuri kwenye michuano ya Mapinduzi kwa miaka mingi, lakini anaamini msimu huu mambo yatakuwa tofauti.

“Kule Bara wenzetu usajili wao ni bora zaidi, kwani wana wachezaji wenye uzoefu zaidi tofauti na Zanzibar ambako ligi haikuwa vizuri. Timu zetu za Zanzibar hazipati fursa ya kucheza mechi nyingi za mashindano ya kimataifa tofauti na Simba, Yanga na Azam, ambazo zinacheza mashindano mengi yakiwamo ya kimataifa pia zinafanya usajili mkubwa ndio maana zinafanya vizuri.

“Huku Zanzibar timu nyingi zina ukata wa fedha na hazina uwezeshaji sasa huwezi kupata matunda mazuri kama hukuwekeza.

“Thamani ya mchezaji mmoja wa Simba au Yanga ni sawa na thamani ya wachezaji wa timu tatu za Zanzibar. Mfano mshahara wa Chama tu pekee unaweza kukuta ni bajeti ya ya mshahara wa timu moja ya Zanzibar kwa mwaka mzima lakini ukiangalia kiwango chake unaweza kukuta hakitofautiani sana na mchezaji wa huku mfano muangalie Feisal,” anasema Said.

WASIKIE MAKOCHA

Kocha wa Malindi, Abdulghany Msoma anasema wanajipanga vizuri kushangaza msimu huu, akiamini timu mojawapo ya Zanzibar itafika fainali na hata kutwaa ubingwa.

“Tuko tayari kwa mashindano, wachezaji wangu wako fiti kuhakikisha tunafanya vizuri katika mashindano haya. Kila timu iliyopo kwenye mashindano ni nzuri na hatuidharau timu yoyote.”

Anapoulizwa timu za Zenji zinakwama wapi? Msoma anasema kweli timu za Bara zimekuwa zikitikisa kwenye mashindano hayo kwa miaka 10 iliyopita lakini wanashukuru msimu huu ligi ya Zanzibar imeamka kutokana na udhamini waliopata ukiwemo kutoka Azam, hivyo utaleta chachu ya timu za huko kufanya vizuri kwenye michuano hiyo.

“Tunashukuru msimu huu tumeanza kupata udhamini hivyo umetupa nguvu ya kusajili wachezaji mahiri pia tumeanza kuona wachezaji wazuri wanatoka nje ya Zanzibar na kuja kucheza ligi ya hapa.

“Miaka ya nyuma tulikuwa hatuna mambo hayo na kama unavyojua mpira ni ajira hivyo mchezaji anatafuta sehemu yenye maslahi ndio maana hata timu ya taifa ya Zanzibar unaweza kuunda kwa wachezaji waliopo bara tu kwa sababu wengi walienda kucheza huko kwa maslahi mazuri.”

Chanzo: Mwanaspoti