Klabu ya Tottenham inaamini Julian Nagelsmann atakuwa chaguo sahihi kuwa kocha mkuu kwa ajili ya msimu ujao kwa mujibu wa ripoti.
Spurs ilianza mazungumzo ya chini chini ili imteue kocha huyo wa zamani wa Bayern Munich aje kuchukua mikoba ya Antonio Conte.
Kwa mujibu wa ripoti, Tottenham inataka kukamilisha mpango yao kwanza ya msimu ujao, wakati Nagelsmann akisubiri kuona mkurugenzi gani mpya atakayechaguliwa, kabla ya kufanya uamuzi.
Kuibuka kwa Johannes Spors kama mgombea wa ukurugenzi wa michezo wa klabu hiyo kumezua maswali kwani ana uhusiano wa rafiki wa karibu Nagelsmann, huku mgombea mwenza akiwa Lee Dykes ambaye ni mkurugenzi wa ufundi wa sasa wa Brentford.
Spurs imesisitiza Nagelsmann ndiye atafaa kuwa kocha mkuu msimu ujao kwani mpaka sasa hana mpinzani katika kinyang’anyiro hicho.
Awali Nagelsmann alipewa nafasi kubwa ya kuwa kocha wa Chelsea, lakini alijiondoa.
Naglesmann amefungua milango ya kutua Ligi Kuu England, huku Tottenham ikiwa bado haijapata kocha mkuu tangu ilipomtimua Conte.
Nafasi ya juu ya kazi iliyobaki ni ndani ya klabu ya Real Madrid ambayo inaweza kuwa wazi endapo Carlo Ancelotti ataondoka, hiyo inamaanisha huenda Nagelsmann akabadili uamuzi akatimkia Hispania kwa mujibu wa ripoti.
Licha ya Bayern kumtimua Nagelsmann, itaingiza faida ya Pauni 10 milioni endapo atapata timu nyingine ya kuifundisha msimu ujao.