SOKA limebadilika sana siku hizi, mshambuliaji yeyote Duniani lazima atacheza kwa kujiamini kama magoli hayatakauka miguuni mwake.
Mshambuliaji wa Yanga, Fiston Kalala Mayele, Mkongomani huyu, alianza vizuri ndani ya Yanga na sasa ndie kila kitu kwenye makaratasi ya Mwalimu Mohammed Nabi anapomuwaza mshambuliaji wake kinara.
Wapi Fiston anafanikiwa zaidi?
Soka la sasa haliwezi kutupa kila aina ya mchezaji ndani ya uwanja bali mwalimu atatazama wale ambao watasimama katika mbinu zake kuelekea katika mchezo husika.
Mwalimu Nabi anatumia 4-2-3-1, tofauti ya Makambo na Fiston ni kubwa kwa maana ya uchezaji ingawa wote ni washambuliaji, Makambo anacheza kama striker na Fiston anaweza kucheza kama forward, nimekuchanganya? Ngoja nikufafanulie.
Forward ni mchezaji yeyote wa mbele, anaweza kuwa winga wa kulia au kushoto au mshambuliaji wa kati lakini striker ni mshambuliaji wa kati pekee.
Mfano Mohammed Salah na Sadio pale Liverpool ni ma forward lakini unapotaja striker hapo anaweza kuingia Lewandowsky, Kun Aguero na wengineo.
Kwanini Fiston nasema anaweza kucheza kama forward au striker, ni zile movement (mikimbio ) zake na uwezo wa kutengeneza link up play katika eneo la final third.
Faida kubwa ya Fiston anapofanya mikimbio ya kuwatoroka walinzi anavunja mstari wa ulinzi wa timu pinzani na kuwalamizisha waache gapes nyuma yao na hapo sasa ndo yanapokuja madhara ya Moloko na Yacouba kukimbia nyuma ya walinzi.
Makambo ni mfungaji zaidi, deadly striker anaeweza kukupa magoli kama utamtengenezea system ya yeye kusimama zaidi kama target man lakini Mayele anaifanya system anayoitumia Nabi kuwa hai kule mbele.
Ndivyo mpira wa kisasa ulivyo, hauwezi kukupa kila unachokipenda, umenielewa?.