mara ya mwisho kwa wachezaji wazawa wa Simba kufunga kwenye mechi ya Ligi Kuu Bara ni Desemba 30, mwaka jana kwenye ushindi wa mabao 7-1 dhidi ya Tanzania Prisons na katika michuano ya Kombe la Shirikisho la Azam (ASFC), dhidi ya African Sports Machi 3.
Baada ya hapo, hakuna mzawa aliyefunga kwenye mechi zilizofuata hadi sasa na mabao yote yamefungwa na wachezaji wa kigeni ikiwa ni kwenye michuano ya ASFC, Ligi Kuu na Ligi ya Mabingwa Afrika wakiongozwa na Jean Baleke.
Ni wazi upepo mzuri upo kwa nyota wa kigeni licha ya uwepo wa wazawa uwanjani na mchango wao mkubwa.
Mwanaspoti linakuchambulia mechi walizofunga nyota wa kigeni baada ya wazawa kufunga mara ya mwisho dhidi ya Tanzania Prisons 7-1 kwenye Uwanja wa Mkapa, jijini Dar es Salaam Desemba 30, Simba ikipata hat trick mbili za nahodha John Bocco na Said Ntibanzokiza ‘Saido’ na Shomary Kapombe.
Kwenye michuano ya ASFC, hatua ya 16 bora wazawa wa mwisho kufunga mabao ni Mohamed Mussa, Jimmyson Mwanuke, Kennedy Juma dhidi ya African Sports ya Tanga huku Baleke akitupia moja kwenye ushindi wa mabao 4-0.
Baada ya hapo ni wageni ndo wamekuwa wakiongoza mauaji ya Wekundu wa Msimbazi na kuleta furaha kuanzia kwa mechi za Ligi Kuu Bara, FA na Ligi ya Mabingwa Afrika.
SIMBA VS MBEYA CITY (Januari 18)
Mechi dhidi ya Mbeya City, Simba ilishinda mabao 3-2 mabao hayo yalifungwa na wageni ambao ni Saido (dakika 11 na 49 ) na Pape Sakho dakika 56, wafungaji wa City ni Richard Ngodya na Juma Shemvuni pia ulikuwa mchezo wa Ligi Kuu.
DODOMA JIJI VS SIMBA (Januari 22/2022)
Simba ikishinda bao 1-0 dhidi ya Dodoma Jiji, Uwanja wa Jamhuri mfungaji Baleke ilikuwa mechi yake ya kwanza kwenye Ligi Kuu baada ya kusajiliwa dirisha dogo. Straika huyo kutoka DR Congo alinyakuliwa na Simba kwa mkopo kutoka TP Mazembe na alianza hesabu ya mabao yake kwenye mechi hiyo.
MTIBWA VS SIMBA (Machi 13)
Simba iliichapa Mtibwa kwenye Uwanja wa Manungu, Morogoro mabao 3-0 Baleke akifunga hat-trick dakika ya 3, 7 na 34 na kumfanya straika huyo mwenye umri wa miaka 21 kufikisha jumla ya mabao manne kwenye ligi hiyo.
MECHI ZA CAF
SIMBA VS HOROYA (Machi 18)
Simba ilishinda mabao 7-0 Uwanja Mkapa, Chama alipiga hat -trick , Sadio Kanoute na Sakho wakitupia mawili kila mmoja, ingawa mechi ya kwanza ilipoteza kwa bao 1-0 ugenini.
VIPERS VS SIMBA (Feb 25)
Simba iliifunga Vipers kwa jumla ya mabao mawili nchini Uganda alifunga Henock Inonga Baka, marudiano Uwanja wa Mkapa alitupia Chama.
RAJA VS SIMBA (Aprili 1)
Pamoja na kwamba Simba ilichapwa mabao 3-1, ugenini dhidi ya Raja Casablanca, Baleke alizitikisa nyavu za wapinzani wao wakifunga bao la kufutia machozi, pia mchezo wa kwanza uliopigwa kwa Mkapa, Wekundu wa Msimbazi walipoteza kwa mabao 3-0.
SIMBA VS IHEFU (Aprili 8)
Mchezo mwingine Simba ikishinda dhidi ya Ihefu mabao 5-1, hakuna mzawa alifunga waliohusika na mabao hayo ni Baleke kafunga hat -trick Saido na Sakho kila mmoja akifunga moja.
MSIKIE BALEKE
Baleke ambaye amekuwa na wastani mzuri wa kufunga tangu asajiliwe dirisha dogo, hadi sasa ana hat-trick mbili kwenye Ligi Kuu na ASFC jambo ambalo anasema anatamani kufunga sana kadri awezavyo kuhakikisha huduma yake inakuwa muhimu ndani ya Simba.
“Mchezaji unaposajiliwa dirisha dogo ina maana uongeze nguvu kwa wachezaji uliowakuta, bado kazi inaendelea na mimi nipo tayari kuifanya kwa kadri niwezavyo,” anasema.
WAONAVYO WADAU
Kocha wa zamani wa timu hiyo, Abdallah Kibadeni, anasema si jambo zuri wazawa kutofunga mechi nyingi, kwani ndio wanaotegemewa kwenye kikosi cha Taifa Stars.
“Japokuwa Stars inaundwa na wachezaji mbalimbali, Simba na Yanga ndizo zinazotoa wengi zaidi kulingana na uzoefu wao wao kimataifa, hivyo wanapaswa kujiuliza kwa nini wageni wanafunga na wao wanakwama,” anasema.
Kwa upande wa staa wa zamani wa Yanga, Kipanya Malapa anasema; “Inashangaza kuona straika hafungi ila akifunga mwingine anakuwa wa kwanza kushangilia, kwa nini asiwe wa kwanza kwenda kuyafanyia kazi mapungufu yake, lazima wazawa wabadilike na kujituma kwenye majukumu yao.”