Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Timu zijiandae na mateso 2024

Kumekucha Mapinduzi Cup! Simba, Yanga Ndani! Timu zijiandae na mateso 2024

Tue, 26 Dec 2023 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Mechi za Ligi Kuu Bara kwa mwaka 2023 zimemalizika rasmi kwa mchezo kati ya Tabora United na Yanga uliopigwa kwenye Uwanja wa Jamhuri, jijini  Dodoma, usiku wa Desemba 23.

Japo awali mpango ulikuwa mechi ziendelee hadi mwaka mpya, lakini imekuwa ngumu kutokana na ratiba ya michuano ya Kombe la Mapinduzi ambalo mwaka huu limeandaliwa kitofauti.

Michuano hiyo ambayo lengo lake ni kuyaenzi Mapinduzi ya Zanzibar ya Januari 12, 1964 ambayo mwaka huu yanafikisha miaka 60...hivyo kutakuwa na sherehe za aina yake.

Timu nyingi zimealikwa na ratiba itaanza mapema zaidi (Desemba 28) tofauti na miaka yote ambapo huchelewa kidogo (Desemba 31 au Januari Mosi).

Pia kutakuwa na mechi maalumu ya uzinduzi wa Uwanja wa Amaan, kati ya Kilimanjaro Stars na Zanzibar Heroes.

Mechi hii maarufu kama Samia Derby, itachezwa Desemba 27 hivyo kufanya mambo kuwa magumu zaidi kwa Ligi Kuu.

Mechi kadhaa za Ligi Kuu ambazo zilitakiwa kuchezwa, hasa viporo vya Yanga na Simba, sasa zitachezwa baada ya safari ya Taifa Stars kwenye michuano ya Fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika (Afcon) 2023 inayoanza Januari 13 mwakani na kumalizika Februari 12.

Taifa Stars ambayo iko kundi F sambamba na Morocco, Zambia na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, itamaliza mechi zake za makundi Januari 24 dhidi ya JK Kongo.

Endapo Stars itafanikiwa kufuzu kwa hatua ya 16, jambo ambalo watanzania tunaliombea, maana yake ligi itabidi iendelee kusubiri.

Lakini endapo itashindwa kuvuka hatua ya makundi, jambo ambalo kiuhalisia ndiyo linalitarajiwa, basi ligi itarejea mara moja.

Hadi ligi inasimama, Yanga imecheza jumla ya mechi 11 tu na Simba (10), ikiwa ndio pekee wenye mechi chache, huku timu nyingine kama KMC zikiwa na mechi 14.

Hizi mechi ambazo Yanga na Simba hawajacheza maana yake zitachezwa mara tu ligi itakaporejea ili raundi ya kwanza ikamilike.

Yanga bado haijacheza na Mashujaa ya Kigoma (nyumbani), Tanzania Prisons ya Mbeya (ugenini), Kagera Sugar (ugenini) na Dodoma Jiji (nyumbani).

Viporo vya Simba ni dhidi ya Mashujaa ya Kigoma (ugenini), Azam FC (nyumbani), Tabora United (ugenini), Geita Gold (ugenini) na JKT Tanzania (ugenini).

MATESO

Mechi hizi zitapangwa katika kipindi kifupi na kufanya timu zicheze mechi nyingi ndani ya muda mfupi sana.

Haitokuwa ajabu timu kucheza tarehe 17, 19, 21 na kuendelea...yaani kila baada ya siku mbili.

Haya yatakuwa mateso makubwa sana kwa wachezaji na timu husika kwa ujumla.

Ratiba ngumu ya namna hii kwenye viwanja vibovu kama vya nchi yetu ambayo haina mifumo na taratibu nzuri za lishe kwa wachezaji na tiba za kurudisha miili katika hali ya kawaida, ni mateso sana.

Mzigo wote huu utakuja kubebwa na wachezaji na gharama zake kulipwa na makocha.

Maana wachezaji lazima watachoka sana na kushindwa kucheza kwa uwezo wao wote.

Ikiwa hivyo maana yake matokeo yatakosekana. Na matokeo ndiyo yanayolinda ajira za makocha, yakikosekana na ajira zimekosekana.

Sasa pata picha kocha anafukuzwa kwa sababu matokeo hayakupatikana kutokana na ratiba ngumu ambayo imepangwa na Bodi ya Ligi...lakini CEO wa Bodi ya Ligi yuko salama ilhali yeye ndiyo chanzo.

Bodi ya Ligi imekuwa nyepesi sana kupangua ratiba ya ligi kwa sababu nyepesi nyepesi.

Kwa mfano mechi ya Simba na Azam FC ya Novemba 28 haikutakiwa kuondolewa. Lakini bodi ya ligi iliiondoa mechi hiyo ili kuipa Simba muda wa kujiandaa na mchezo wa Ligi ya Mabingwa dhidi ya Jwaneng Galaxy ya Botswana, Desemba 2.

Hata hivyo, Simba iliondoka nchini Novemba 30, kwenda Francistown Botswana. Wangeweza kabisa kucheza mechi hiyo Novemba 28.

Lakini kwa kuwa Bodi ya Ligi ilikuwa nyepesi, ikaoindoa mechi hiyo kiwepesi wepesi hivyo hivyo...matokeo yake viporo vimekuwa vingi na kusababisha mrundikano wa mechi nyingi kwenye kipindi kifupi na kutesa wachezaji.

Achana na Yanga, Simba na Azam FC ambazo angalau zina jeuri ya kusafiri kwa ndege na kupumzisha wachezaji, hizi timu nyingine ni hatari.

Kusafiri safari ndefu kwa mabasi, tena wakati mwingine vile vibasi vidogo aina ya Coaster, ni mateso kwa wachezaji.

Wengine miguu huvimba kutokana na kukaa kwa muda mrefu, ikizingatiwa siti zenyewe ni ndogo na fupi.

Inatakiwa kufika angalau siku mbili kabla kwenye kituo cha mechi ili miguu irudi kawaida.

Lakini kwa ratiba ya kila baada ya siku mbili mechi, hilo halitowezekana, matokeo yake wachezaji watacheza na miguu iliyovimba...mateso makubwa sana.

Katika mazingira kama haya tunapunguza ushindani kwenye ligi yetu ambayo imekuwa ikikua kwa kasi.

Haya matatizo yanajirudia kila mwaka lakini wahusika wameshindwa kuyapatia ufumbuzi.

Tujiulize, wenzetu kama England kwa mfano wanawezaje?

Maana wao wana mashindano mengi kuliko sisi na wanaenda vizuri tu.

Tumeshuhudia wasimamizi wa ligi kutoka nchi nyingi za Afrika wakifanya ziara nchini kujifunza namna ya kuendesha ligi.

Kwanini wasimamizi wa ligi yetu nao wasiende kujifunza angalau namna ya kuipanga ratiba kutoka kwa wanaofanikiwa kama England?

Au wanadhani ligi yao kuwa namba tano Afrika basi wanajua kila kitu hivyo hawapaswi kujifunza kitu?

Au basi....tusubiri mateso mwakani!

Chanzo: www.tanzaniaweb.live