Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Timu ya bure inayoweza kukupa ubingwa

Dgfjj Timu ya bure inayoweza kukupa ubingwa

Thu, 4 Jan 2024 Chanzo: Mwanaspoti

Mambo ni moto. Klabu mbalimbali za soka huko Ulaya zimetega kwenye dirisha hili la Januari zikijaribu kusaka wachezaji ambao watafaa kuingia katika vikosi vyao moja kwa moja ili kuwania mataji.

Lakini, kwenye vikosi hivyo kuna orodha ya wachezaji wanaomaliza mikataba yao mwisho wa msimu, ambao unaweza kuwanasa bure kabisa kwenye dirisha hili la Januari kwa kuwasainisha dili za awali.

Na kinachovutia zaidi ni kwamba kwenye orodha ya wachezaji ambao unaweza kuwasajili bure kwenye Ligi Kuu England unaweza kuunda kikosi cha kwanza kitakachokuwa na uwezo wa kushindania mataji popote pale.

Klabu kama Manchester United, Chelsea, Arsenal na Liverpool zote kwenye vikosi vyao kuna wachezaji ambao wamebakiza miezi sita kwenye mikataba yao, hivyo wanakuwa huru mwisho wa msimu.

Kuonyesha uhodari wa mastaa hao, kikosi hicho kizima kimeundwa na wachezaji waliobeba mataji 129.

Golini ni kipa anayetarajia kuachana na Newcastle United mwishoni mwa msimu, Loris Karius.

Kipa huyo wa zamani wa Liverpool, akiwa na miaka 30, amecheza mechi moja tu Newcastle tangu alipojiunga na timu hiyo miezi 18 iliyopita. Lakini, bado ana uwezo mkubwa wa kuipa timu ubingwa.

Kwenye beki ya kulia, yupo mkali wa Arsenal, Cedric Soares, 32.

Beki huyo alijiunga na Arsenal akitokea Southampton miaka minne iliyopita, lakini msimu huu bado hajacheza mechi yoyote ya Ligi Kuu England kwenye kikosi hicho cha kocha Mikel Arteta.

Soares alionyesha kiwango kikubwa alipokuwa Fulham msimu uliopita, bado kuna kitu anaweza kukifanya.

Upande wa beki ya kushoto utalindwa na staa wa Bournemouth, Lloyd Kelly.

Licha ya kwamba alitimiza umri wa miaka 25, Oktoba mwaka jana, Bournemouth haitaki kumpa dili jipya. Mchezaji huyo mwenye uwezo mkubwa wa kutumia mguu wa kushoto yupo kwenye rada za miamba ya Italia, Juventus na AC Milan, zikihitaji huduma yake.

Kwenye beki ya kati, kutakuwa na mkongwe wa Chelsea, Thiago Silva, ambaye ataachana na maisha ya Stamford Bridge mwishoni mwa msimu huu. Umri wake ni miaka 39, lakini Mbrazili huyo bado yupo vizuri.

Kwenye ukuta, pacha wake Silva ni beki wa Man United, Raphael Varane, 30.

Kuna klabu kadhaa za Saudi Arabia zinahusishwa na Mfaransa huyo, ambaye atafunguliwa mlango wa kutokea na Man United baada ya msimu huu kumalizika, hivyo atakuwa huru kujiunga bure na timu yoyote.

Kikosi hicho cha wachezaji wa bure, kwenye sehemu ya kiungo itakayokuwa na mastaa watatu, wawili ni nyota wa Arsenal, Jorginho na Mohamed Elneny, ambao wataunda safu hiyo na fundi wa mpira wa Liverpool, Mhispaniola Thiago Alcantara. Kiungo hiyo yote ina wakali wa kupiga pasi na wenye uzoefu.

Mo Elneny, 31, Jorginho, 32, na Alcantara, 32, kombineshi ya miaka 95. Uzoefu ni mwingi.

Fomesheni ya 4-3-3 itatumika kwenye kikosi hiki, ambapo kwenye ile safu yao ya wakali watatu mbele, itaundwa na Mbrazili wa Fulham, Willian, 35, mkali wa Brighton, Danny Welbeck, 33 na straika wa Mashetani Wekundu, Anthony Martial, 28. Kikosi cha kibabe kabisa unachoweza kukisajili kwa uhamisho wa bure itakapofika mwishoni mwa msimu huu.

Chanzo: Mwanaspoti