Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Timu mkao wa kula Ligi Kuu Bara 2024/25

Ngao Simba Yanga Pc Timu mkao wa kula Ligi Kuu Bara 2024/25

Thu, 15 Aug 2024 Chanzo: Mwanaspoti

Wakati pazia la Ligi Kuu Bara kwa msimu wa 2024/2025 likifunguliwa kesho, timu zimetamba kuwa maandalizi ziliyofanya yanazipa matumaini ya kila moja kutimiza malengo wakati msimu utakapofikia tamati mwakani.

Mchezo baina ya Pamba Jiji na Tanzania Prisons utakaochezwa kwenye Uwanja wa CCM Kirumba mjini Mwanza kesho utafungua pazia na baada ya hapo utafuatiwa na mechi kati ya Mashujaa na Dodoma Jiji ambao utapigwa Kigoma katika Uwanja wa Lake Tanganyika keshokutwa ambapo pia Namungo itacheza na Fountain Gate.

Makocha na wachezaji wa timu tofauti zinazoshiriki Ligi Kuu wameliambia gazeti hili kuwa wanafahamu msimu utakuwa mgumu na wenye ushindani, lakini wamejipanga kuhakikisha timu zao zinapata matokeo mazuri.

"Timu nyingi zimefanya usajili mzuri na zimekuwa zikijiandaa kwa kiwango cha juu jambo ambalo tunaamini litafanya ushindani katika ligi uwe mkubwa na hakutakuwa na wepesi dhidi ya timu yoyote ile," alisema kocha wa Mashujaa FC, Mohammed Abdallah 'Baresi'.

"Kwa upande wetu Mashujaa FC tumekuwa na kambi nzuri ya kujiandaa na niseme tu kuwa tupo tayari kukabiliana na kazi iliyo mbele yetu. Malengo yetu ni kumaliza katika nafasi nzuri, hivyo nimewaambia wachezaji wangu wanapaswa kufanya kazi ya ziada."

Kocha msaidizi wa KMC, John Matambala alisema wana imani usajili na maandalizi waliyoyafanya yatawalipa na wanaamini msimu utakuwa mzuri kwao.

"Sisi tunasubiri ligi tukijua fika kwamba itakuwa ni ngumu kwa vile washindani wenzetu pia wanajiandaa vizuri na kwa timu kama KMC inahitaji kumaliza msimu ikiwa katika nafasi za juu kwenye msimamo wa ligi.

"Na kwa kuanzia tunapaswa kupata matokeo mazuri katika mchezo wetu wa kwanza dhidi ya Coastal Union ambayo ni timu nzuri na inashiriki mashindano ya kimataifa. Tukianza vizuri inasaidia kuwaweka wachezaji katika hali nzuri kisaikolojia kwa mechi ambazo zitafuata baada ya hapo," alisema Matambala.

Beki na nahodha wa Fountain Gate, Shaffik Batambuze alisema wanafahamu ugumu wa ligi utakavyokuwa, lakini hawapaswi kutumia kama utetezi na badala yake jukumu lao ni kuhakikisha wanapata matokeo mazuri.

"Tuko tayari na tunajua nini ambacho tunakwenda kukipambania na kila mchezaji yuko tayari, amefanya mazoezi vizuri na tunajua nini tunakitaka. Tuko na malengo yetu na pia tuna malengo ya kitimu," alisema Batambuze.

"Hakuna ambaye amekuja hapa kwa kusaidiwa na badala yake anaweza. Hivyo mchezaji yeyote ambaye atapewa nafasi ya kucheza anatakiwa apambane ili tufike pale tunakotakiwa kufika."

Kocha wa Singida Black Stars, Patrick Aussems alisema kuwa timu yake ni kubwa, hivyo ina malengo makubwa.

"Tumefanya maandalizi ya kama wiki tano, sita hivi na yananipa matumaini kwamba tunakwenda kuwa na msimu mzuri maana nina kikosi kizuri na kipana ambacho kinanipa wigo mzuri katika kuamua nani acheze na nani asicheze na yeyote ambaye atapata nafasi naamini ataonyesha kitu," alisema Aussems.

Kocha wa Dodoma Jiji, Mecky Maxime alisema kuwa anaamini msimu huu watafanya vizuri kulinganisha na ilivyokuwa msimu uliopita.

"Wachezaji wote wapo tayari na imebakia kwetu sisi walimu kuamua nani waanze kutuwakilisha. Mashabiki wa Dodoma Jiji hii ni timu yao na siku zote mashabiki wana mchango mkubwa kwenye timu, hivyo waje tushirikiane ili timu iweze kufikia malengo yake," alisema Maxime.

Timu 16 zitaumana kwa zaidi ya miezi minane kusaka ubingwa wa ligi hiyo msimu ujao ambao kwa sasa taji lake linashikiliwa na Yanga iliyochukua msimu uliopita ulioshuhudia Azam FC ikishika nafasi ya pili, huku ile ya tatu ikichukuliwa na Simba ilhali Coastal Union ikimaliza ya nne.

Kwa mujibu wa kalenda ya mashindano ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), Ligi Kuu Bara msimu ujao itafikia tamati, Mei mwakani.

Chanzo: Mwanaspoti