Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Timu kaeni mkao wa kula, Ligi Kuu inarejea

Simba, Yanga Warejea Ligi Kuu Jumamosi Timu kaeni mkao wa kula, Ligi Kuu inarejea

Sun, 28 Jan 2024 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Bodi ya Ligi (TPLB) bado haijatoa ratiba ya Ligi Kuu Bara iliyosimama kwa muda kupisha michuano ya Kombe la Mapinduzi 2024 na ile ya Kombe la Mataifa ya Afrika (Afcon) 2023, lakini wadau wa soka wamekuwa na hamu ligi hiyo ianze ili washuhudie ushindani baada ya timu kusajili kupitia dirisha dogo.

Ligi hiyo ilisimama tangu Desemba 23 mara baada ya mechi ya Tabora United na Yanga iliyopigwa jijini Dodoma na watetezi wa ligi hiyo, Vijana wa Miguel Gamondi kutoka na ushindi wa bao 1-0, ukiwa ni mchezo wa 11 kwa Yanga, lakini ukikamilisha raundi ya 14 ya ligi hiyo inayoongozwa na Azam kwa sasa.

Hata hivyo, baada ya timu ya taifa ya Tanzania ‘Taifa Stars’ kutolewa mapema hatua ya makundi Afcon na huku asilimia kubwa ya wachezaji wa Simba, Yanga na Azam wakiwa wamesharejea, wadau wana hamu ya kutaka kuona mbungi inapigwa kwenye viwanja ili kumaliza tambo zinazoendelea mtaani na mitandaoni.

Msemaji wa Bodi ya Ligi, Karim Boimanda jana aliweka wazi alipokuwa anazungumza na Azam Tv, akisema kwamba Desemba 23 walipotangaza kusimama kwa Ligi Kuu kupisha majukumu ya Stars walizingatia mambo muhimu ambayo kwayo hawana budi kuyarejea ili utamu wa ligi uendelee kama kawaida.

“Tulisema endapo kama timu ya taifa itakuwa imemaliza majukumu ya Afcon, basi hatutakuwa na sababu ya kusubiri na waliobakia kwenye majukumu ya timu za taifa zao ni wachache sana hawawezi kufanya tusiendelee na ligi,” alisema Boimanda.

“Hivi karibuni tutatangaza ratiba ya Ligi Kuu, maana wamesalia wachezaji watatu kwenye timu zao za taifa. Hilo haliwezi kuzuia timu kuendelea na mechi za kumalizia msimu huu.”

Wachezaji waliobaki Afcon wanaocheza Ligi Kuu kutoka Yanga ni Aziz Ki (Burkina Faso) na Djigui Diarra (Mali) ambao timu zao zitashuka uwanjani keshokutwa Jumanne, huku kwa Simba akisalia beki Henock Inonga (DR Congo) ambao leo wanavaa na Misri katika mechi ya 16 Bora zilizoanza rasmi jana.

Bodi ikitoa ufafanuzi huo, nyota wa zamani wa Simba, Emmanuel Gabriel alisema; “Binafsi kuna timu zimesajili wachezaji wa ndani na nje, natarajia kuona wanaongeza nguvu kwenye vikosi vyao, ukiondoa Simba, Yanga na Azam FC, kuna Mtibwa Sugar ambayo ipo nafasi mbaya kwenye msimamo, je waliongezeka watafanya nini. Nimeona baadhi ya wachezaji waliowatangaza kama kipa Mburundi, Justin Ndikuman, Jimson Mwanuke, Charles Ilanfya na wengine je wataisaidia Mtibwa isishuke daraja.”

Kwa upande wa staa wa zamani wa Yanga, Edibily  Lunyamila alisema burudani yao ni kuangalia mpira, hivyo anatarajia Ligi Kuu itakapoanza ataona ushindani mkubwa.

“Kuna wachezaji tumewasikia wamesajiliwa Simba, Yanga na Azam FC Majina yao yamekuwa makubwa, tunahitaji kuwaona uwanjani wanazisaidiaje hizo timu, si hizo tu kuna nyingine zipo nafasi mbaya kwenye msimamo wa Ligi Kuu, ongezeko la wachezaji wapya wataleta manufaa gani,” alisema Lunyamila aliyewahi kuwika pia na Biashara Shinyanga, Simba, Malindi na Taifa Stars.

ZISIKIE TIMU SASA

Kocha wa Mashujaa, Abdallah Mohammed ‘Bares’, alisema “Kwa vyovyote vile  ligi italazimika kuendelea, sisi tulijiandaa kwa muda wote, ili kuonyesha ushindani.” 

Kwa upande wa Mecky Mexime kocha wa Ihefu, alisema “Maandalizi yanakwenda vizuri, ligi ikianza tupo tayari kwa ajili ya ushindani.”

Nahodha wa Prisons, Benjamin Asukile alisema: “Tupo tayari kwa ushindani ligi ikianza, tumefanya maandalizi naamini mashabiki watafurahia kuona burudani za mechi.”

Elias Maguri, nahodha wa Geita Gold alisema: “Timu zimesajili hivyo natarajia ushindani utakuwa mkubwa na ngumu kwani tutaelekea kumaliza msimu huu, zipo zinazopiga mahesabu ya ubingwa na kutoshuka daraja.”

Chanzo: www.tanzaniaweb.live