Hofu imetanda Emirates Stadium kufuatia kuumia kwa Beki kutoka nchini Uholanzi Jurriën David Norman Timber, huku taarifa zikisema huenda akawa nje ya Uwanja kwa zaidi ya mwezi mmoja.
Timber aliyesajiliwa Arsenal majuma kadhaa yaliyopita akitokea Ajax Amsterdam ya nchini kwao Uholanzi kwa Pauni 34 milioni, alishindwa kumaliza mchezo wa Ufunguzi wa Ligi Kuu mwishoni mwa juma lililopita dhidi ya Nottingham Forest.
Katika mchezo huo Arsenal iliyokuwa nyumbani Kaskazini mwa jijini London, iliibuka na ushindi wa 2-1.
Timber mwenye umri wa miaka 22, alipata pigo mara mbili kwenye mchezo huo, lakini pigo la pili lilimfanya ashindwe kuendelea na mchezo, na kulazimika kutolewa nje ya dimba.
Awali alitarajiwa huenda angekaa nje ya Uwanja kwa majuma kadhaa, lakini ripoti zinaeleza kuwa, Beki huyo huenda akashindwa kujiunga na wenzake kwa kipindi cha hivi karibuni, kwani itamchukuwa zaidi ya mwezi mmoja.