Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

TV

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Tigers Queens yakiri mambo magumu WPL

Tigers Wpl Tigers Queens yakiri mambo magumu WPL

Sat, 1 Apr 2023 Chanzo: Mwanaspoti

Licha ya mwenendo mbovu kwenye Ligi Kuu ya Wanawake, Kocha msaidizi wa The Tigers Queens, John Bosco amesema timu hiyo haitashuka daraja na watafanya kila liwezekanalo kuibakisha huku akikiri kazi ipo kutokana na kikosi chake kuonesha kiwango cha chini.

Tigers yenye maskani yake jijini Arusha imevuna pointi saba pekee katika michezo 12 iliyocheza ikikamata nafasi ya nane kati ya timu 10 za ligi hiyo, ambapo Alhamisi iliyopita ilichapwa mabao 4-1 na Alliance Girls baada ya kubamizwa mabao 7-0 na Simba Queens.

Timu hiyo imeshinda mechi mbili, sare moja na kupoteza tisa huku ikifunga mabao saba na kuruhusu 36 ikizidiwa na Amani Queens iliyoruhusu mabao 40 baada ya kushinda mechi moja, sare moja na kupoteza 10 ikifunga mabao sita.

Kila timu imebakiza mechi sita kuhitimisha ligi, ambapo imesimama kwa siku saba kupisha kambi ya timu za taifa iliyoanza Machi 24 hadi 31, na itarejea Aprili 5, ambapo Tigers itawakaribisha Baobab kisha Ceassia Queens Aprili 12 kwenye Uwanja wa Black Rhino, Karatu.

Bosco aliliambia Mwanaspoti kuwa kinachowakwamisha kwa sasa ni kuvurugika kwa timu yao waliyokuwa nayo msimu uliopita ambapo kwa sasa inachukua muda mrefu wachezaji waliopo kutengeneza muunganiko.

Alisema mchezo uliopita waliopoteza kwa mabao 4-1 mbele ya Alliance Girls katika Uwanja wa Nyamagana, Mwanza ni kwa sababu ya uchovu wa safari ambapo walishindwa kufanya maandalizi, huku akisisitiza wanahitaji kupambana kutoshuka daraja.

“Kuna makosa mengi tumetengeneza lakini pia tuliathiriwa na uchovu wa safari tulifika Mwanza usiku na kushindwa kufanya recovery tunarudi nyumbani kujiandaa tutakaa na vijana wetu tutafanya kila linalowezekana tunaamini hatuwezi kushuka daraja,” alisema Bosco na kuongeza;

“Tulitengeneza timu nzuri msimu uliopita lakini ikavurugika waliopo wanachukua muda kutengeneza muunganiko lakini tutaendelea kulitatua kazi kubwa ni kupambana tusishuke ili tujiandae na msimu ujao.”

Chanzo: Mwanaspoti