Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Thuweni Ally mfungaji bora wa muda wote Tanzania kwenye AFCON

Capture (600 X 404) Thuweni Ally mfungaji bora wa muda wote Tanzania kwenye AFCON

Tue, 17 Oct 2023 Chanzo: Mwanaspoti

Tanzania imefuzu kwa mara ya tatu kucheza Fainali za Mataifa ya Afrika (Afcon) baada ya kufanya hivyo 1980 na 2019.

Katika mara mbili zilizopita Tanzania ilifunga jumla ya mabao matano; matatu mara ya kwanza 1980 na mawili mara ya pili 2019.

NIGERIA 1980

8/3/1980

Nigeria 3–1 Tanzania

-Juma Mkambi 54’

12/3/1980

Misri 2–1 Tanzania

-Thuweni Ally Waziri 86’

15/3/1980

Ivory Coast 1–1 Tanzania

-Thuweni Ally Waziri 59’

MISRI 2019

23/6/ 2019

Senegal 2–0 Tanzania

27/6/ 2019

Kenya 3–2 Tanzania

-Saimon Msuva 6’

-Mbwana Samatta 40’

1/7/ 2019

Tanzania 0–3 Algeria

Katika mabao hayo matano, mabao mawili yalifungwa na mtu mmoja. Mtu huyo ndiye Thuweni Ally Waziri ambaye hadi sasa ndiye mfungaji bora wa Tanzania kwenye fainali za Afcon.

Thuweni alifunga mabao mawili na kukaribia kuwa mmoja wa wafungaji bora wa jumla wa fainali hizo.

Mfungaji bora wa jumla wa Afcon ya 1980 pale Nigeria alikuwa na mabao matatu, moja tu akimzidi Thuweni Ally Waziri wa Tanzania.

Waliofunga mabao matatu walikuwa wawili, Khalid Labied wa Morocco na Segun Idegbami wa Nigeria.

Bahati njema kwa wawili hawa ni kwamba timu zao zilifika hadi siku ya mwisho ya mashindano nao wakafunga.

Khalid Labied wa Morocco alifunga mabao mawili kwenye mechi ya kutafuta mshindi wa tatu dhidi ya Misri.

Hii ina maana hadi anafika siku hiyo, alikuwa na bao moja tu.

Segun Idegbami wa Nigeria naye timu yake ilifika fainali na yeye akafunga mabao mawili siku hiyo.

Mabao yake hadi fainali alikuwa na bao moja.

Tanzania ya Thuweni Ally Waziri ilitoka hatua ya makundi tu, lakini yeye akawa na mabao mawili.

Unaweza ukajiuliza, je timu yake ingefika angalau nusu fainali, ingekuwaje?

WAFUNGAJI BORA AFCON 1980

Mabao matatu

Khalid Labied - Morocco

Segun Odegbami - Nigeria

Mabao mawili

Lakhdar Belloumi - Algeria

Tedj Bensaoula - Algeria

Muda Lawal - Nigeria

Thuwein Waziri - Tanzania

NANI HUYU THUWENI ALLY WAZIRI?

Ni mmoja wa wachezaji waliounda kikosi cha Taifa Stars kilichofuzu Afcon 1980 kwa kuwatoa Zambia mwaka 1979 jijini Ndola.

1: Juma Pondamali (Pan Africa - Dar Es Salaam)

2: Leopard Tasso (Balimi FC -Bukoba)

3: Mohammed Kajole, (Simba- Dar Es Salaam)

4: Salim Amir (Costal Union - Tanga)

5: Jella Mtagwa (Pan Africa- Dar Es Salaam)

6: Leodegar Tenga (Pan Africa- Dar Es Salaam)

7: Hussein Ngulungu (Pan Africa- Dar Es Salaam)

8: Omari Hussein (Yanga - Dar Es Salaam)

9: Peter Tino (African Sports - Tanga)

10: Mohamed Salim (Costal Union - Tanga)

11: Thuweni Ally (Simba SC - Dar Es Salaam)

Thuweni Ally Waziri alikuwa mmoja wa mawinga hodari sana kutoka hapa Tanzania akivuma kwa mashuti yake makali ya mguu wa kushoto.

Alizaliwa Aprili 6, 1959 visiwani Zanzibar na kupata elimu yake hapohapo visiwani akianzia shule ya Darajani kwa elimu ya msingi na elimu yake ya sekondari alipata kwenye Shule ya Sekondari ya Haile Selassie.

Kama ulivyo utamaduni wa wachezaji, alianza kucheza soka shuleni halafu akachezea timu za watoto Everton na Small Simba katika soka la Juvinile na Cental, kwa utamaduni wa Zanzibar.

Mwaka 1975 akasajiliwa na timu ya Malindi ya Zanzibarna akadumu nayo hadi 1979 aliponaswa na Simba SC ya Dar es Salaam.

Mwaka huo ndiyo ule ambao Simba SC iliweka historia kwa kupindua matokeo ya kichapo cha 4-0 nyumbani na kushinda 5-0 ugenini dhidi ya Mufurira Wanderers ya Zambia, mjini Ndola.

Katika mchezo huo uliohudhuriwa na Rais Kenneth Kaunda wa Zambia, Thuweni Ally Waziri alifunga mabao matatu peke yake.

Mwaka 1982 aliondoka Simba na kutimkia Kenya kujiunga na Belham ambayo ilikuwa daraja la pili.

Huu ulikuwa uhamisho wa kimkakati kwani timu hiyo ilikuwa kama njia ya kutimkia Uarabuni ambako ndiko kulikuwa soko la wacheaji wa Tanzania wakati huo.

Kutokea Tanzania moja kwa moja ilikuwa vigumu sana kwani Serikali iliweka vizuizi vingi.

Alikaa klabuni hapo kwa miezi mitatu tu kisha akatimkia Abu Dhabi, Falme za Kiarabu kujiunga na timu ya jeshi la nchi hiyo.

Mwaka 1987 akajiunga na timu ya Al Suwaiq ya Oman. Alikaa hapo hadi alipostaafu soka mwaka 2002 na kuamua kuendelea kuishi hukohuko hadi sasa.

Wakati Tanzania ikiwa na uhakika wa kucheza Afcon mbili zijazo, 2024 na 2027, bado Thuweni Ally Waziri anaendelea kutamba kama Mtanzania pekee aliyefunga mabao mengi kwenye fainali hizo.

Kama watakuwepo mwakani na kuwa na michezo mizuri, Mbwana Samatta na Saimon Msuva wana nafasi kubwa ya kumfikia mwamba huyo na hata kumpita kwani wachezaji hao wako nyuma kwa bao moja pekee kila mmoja.

Chanzo: Mwanaspoti