Meneja wa klabu ya Chelsea, Mjerumani, Thomas Tuchel amemtaka Kiungo Mshambuliaji kutoka nchini Morocco Hakim Ziyech kuimarika zaidi, ili kuiwezesha klabu hiyo kupata matokeo mazuri katika michezo ijayo.
Tuchel ametoa kauli hiyo kwa Ziyech, baada ya kuifungia Chelsea bao 1-0 dhidi ya Malmo, katika mchezo wa Ligi ya Mabingwa Barani Ulaya juzi Jumanne (Novemba 02).
Bao hilo lilikuwa la kwanza kwa Ziyech tangu alipofunga kwenye UEFA Super dhidi ya Villarreal, Agosti na la tatu kwenye Ligi ya Mabingwa Ulaya katika michezo 13 aliyocheza akiwa na ‘The Blues’.
Mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 28, alionekana kuwa kwenye kiwango bora zaidi katika mchezo huo uliopigwa nchini Sweden akifunga kwa kuunganisha pasi ya Hudson-Odoi.
Tuchel, ambaye alimsifia nyota huyo baada ya mchezo huo, amesema anataka kuona mengi zaidi kutoka kwa Ziyech.
“Alikuwa na mchezo mzuri na kwa hakika nampongeza kwa hilo,” amesema Tuchel.
“Bado naona kuna nafasi kwake yeye kuendelea kuimarika zaidi. Anaweza kuwa bora zaidi ya alivyo sasa.
“Bado hajawa fiti kwa asilimia 100 kama ambavyo anatakiwa kuwa, lakini ninaamini ataimarika zaidi.”