Wababe wa Kaskazini mwa jijini London ‘Arsenal’ wamefungua milango ya kumuuza Kiungo kutoka nchini Ghana Thomas Partey kwenye dirsha hili la uhamisho wa majira ya kiangazi Barani Ulaya.
Arsenal inapambana kuboresha safu yake ya kiungo baada ya kukosa taji la Ligi Kuu England msimu uliopita 2022/23, mbele ya Manchester City.
Kwenye mpango huo, imewaweka kwenye orodha viungo Declan Rice na Moises Caicedo ikipiga hesabu za kunasa saini zao katika dirisha hili huku wengine ikitarajia kuwafungulia mlango wa kutokea.
Partey mwenye umri wa miaka 30, mkataba wake umebakiza miaka miwili na kuna timu mbili za Italia zinahitaji saini yake.
Kiungo huyo alikuwa kwenye kiwango bora sana sehemu kubwa ya msimu, kabla ya kuja kutibua mambo mwishoni.
Meneja wa Arsenal kwa sasa anatajwa kuwa tayari kuachana naye ili kwenye nafasi hiyo amlete Caicedo, huku nafasi kubwa ikielekezwa kwenye kumnasa Rice kutoka West Ham United.
Caicedo analingana na Partey kwa majukumu yake ya uwanjani na Arsenal ilijaribu kumsajili January.
Hata hivyo, wakati huu wa dirisha la usajili la majira ya kiangazi ushindani utakuwa mkali kutokana na Chelsea na Liverpool nazo kuhitaji saini yake.
Bei yake anayoweza kuuzwa itazidi Pauni 70 milioni. Kuhusu Rice, klabu yake ya West Ham United itahitaji ada ya Pauni 110 milioni.
Kiungo mwingine anayehusishwa na mpango wa kuachana na Arsenal ni Granit Xhaka anayewindwa huko Bayer Leverkusen na Bayern Munich.