Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

TV

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Thibaut Courtois: Man City ijipange, haitakuwa rahisi

Curtois Mlinda mlango wa Real Madrid Thibaut Courtois

Thu, 11 May 2023 Chanzo: Dar24

Mlinda Lango wa Mabingwa wa Soka Barani Ulaya Real Madrid, Thibaut Courtois amesisitiza wana uwezo mkubwa kutokana mafanikio waliyopata katika Ligi Mabingwa Barani humo, huku akiitahadharisha Manchester City ijipange kwenye mchezo wa Mkondo wa Pili wa Nusu Fainali ambao utapigwa Uwanja wa Etihad mjini Manchester, juma lijalo.

Kwenye Mchezo wa Mkondo wa Kwanza uliopigwa juzi Jumanne (Mei 09) katika Uwanja wa Santiago Bernabeu nchini Hispania, timu hizo zilitoka sare ya bao 1-1, mabao yakifungwa na Vinicius Jr na Kevin De Bruyne.

Kwa matokeo hayo, Mchezo wa Mkondo wa Pili utakuwa mgumu zaidi kwa sababu Manchester City haijapoteza mchezo nyumbani katika msimu huu 2022/23.

Kwa upande wa Real Madrid haitakubali kupoteza mchezo huo kirahisi kwa mujibu wa Mlinda Lango Courtois kufuatia sare hiyo.

Akizungumza kupitia kituo cha televisheni cha BT Sports, Courtois amesema: “Ulikuwa mchezo mzuri pande zote. Tulilinda lango letu kwa kiwango kikubwa. Kama unataka kulinda unampa wakati mgumu Erling Haaland.

“Tulicheza vizuri, nadhani itakuwa kama fainali kwenye mechi ya marudiano. Naamini kila mtu ataiweka akilini kwa sababu mechi itakuwa ugenini.

“Nachofahamu sisi ni wazuri zaidi kwenye mechi kama hizi kutokana na uzoefu wetu. Haijalishi tunacheza wapi, tunajua tunachotaka siku zote.

“Real Madrid ilionyesha kiwango bora kipindi cha pili baada ya kuanza kwa kusuasua kipindi cha kwanza cha mchezo huo, hata hivyo ikabadilika na kuanza kulishambulia lango la Man City.

Mshindi wa jumla wa mchezo huo atacheza Fainali dhidi ya Mshindi wa jumla wa Nusu Fainali ya Pili kati ya AC Milan dhidi ya Inter Milan, ambazo jana Jumatano zilicheza mchezo wa Mkondo wa Kwanza mjini Milan.

Inter Milan ilichomoza na ushindi wa mabao 2-0, na sasa inalazimika kujiandaa sambamba na kulinda ushindi huo kuelekea mchezo wa Mkondo wa Pili ambao utapigwa Jumanne ya juma lijalo.

Chanzo: Dar24