Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Thank You & Welcome, mwisho na mwanzo wa enzi mpya Azam FC

Feisal Azam  KL.jpeg Thank You & Welcome, mwisho na mwanzo wa enzi mpya Azam FC

Thu, 22 Jun 2023 Chanzo: Mwanaspoti

AZAM FC huko mitandaoni imenoga kwa sasa, kila baada ya muda kadhaa wanachapisha picha yenye maneno ya Kiingereza 'Thank You', iliyoambatana na mchezaji, kocha au mtu mwingie aliyekuwa mtumishi wa timu hiyo.

Pia kuna machapisho yamekuwa na neno 'Welcome', hayo yalianza kwa kocha mkuu mpya Youssouph Dabo kutoka Senegal na kiungo fundi Feisal Salum 'Fei Toto' kutoka Yanga na neno 'Welcome' kugota hapo lakini Mwanaspoti linafamu kuwa siku chache zijazo watatambulishwa mastaa wengine wapya wawili sambamba na wataalamu wengine wa benchi la ufundi.

Huenda huo ukawa mwisho wa enzi. Hapa zikizungumzwa enzi za kile kizazi pendwa kwa mabosi wa Azam lakini kilichozingua uwanjani. Kizazi kile kilichoichukulia Azam kama Mama yao, hata kikimwaga mboga hakiwezi kufukuzwa nyumbani. Mtaani walikiita kizazi mayai. Ndio hicho kinaondoka Azam.

Wakati kizazi hicho kikionekana kuondoka Azam, huo ni mwanzo wa enzi ya kizazi shupavu. Kizazi Dume. Kizazi kitakachokuja kuzichangamsha Simba na Yanga katika mashindano ya ndani na kutisha Afrika nzima. Tusubiri tuone.

THANK YOU

Kitendo hicho cha kusafisha kikosi chao kilianza mwanzoni mwa msimu juzi kwa mtindo huo huo wa 'Thank You', waliachwa wachezaji kibao wa kikosi hicho wakiwemo kina Paul Peter, Mudathir Yahya, Salum Abubakar 'Sure Boy' na Frank Domayo. Moja ya kizazi kilichokuwa kimejitengenezea ufalme pale Chamazi yalipo masikani ya Azam.

Msimu huu Azam imeendelea kufanya usafi kwa kuondoa watu ambao inaona hawafai kuvaa jezi zao nyeupe, bluu na nyeusi kwa msimu ujao hata wale wa benchi la ufundi.

Tayari imeachana na aliyekuwa kocha makipa, Dani Cadena, mtalamu wa viungo Moadh Hiraoui sambamba na aliyekuwa kaimu kocha mkuu, Kally Ongala kwenye benchi la ufundi.

Haijaishia hapo, Azam imewapa Thank You, beki wake wa muda mrefu Bruce Kangwa, mshambuliaji Rogers Kola, viungo Keneth Muguna, Ismael Kader na Cleophace Mkandala, kipa Wilbol Maseke na aliyekuwa nahodha wake wa muda mrefu pia kocha msaidizi Agrrey Moris aliyudumu kikosini hapo kwa miaka 14.

Bado Azam haijamaliza kusafisha kikosi chake kwani imewaita wachezaji wake waliokuwa kwa mkopo kwenye timu nyingine ili kocha Dabo awaone na ambao ataona hawamfai basi watapewa 'Thank You' za kila mmoja kimpango wake.

Mwanaspoti limepenyezewa, Yahya Zayd, Shaban Chilunda, Iddi Nado na Ali Ahmada nao wapo kwenye uangalizi maalumu chini ya Dabo na kama hataridhika nao basi wanaweza kujishindia 'Thank You' kabla ya timu kuanza maandalizi ya msimu ujao.

WELCOME

Ukiachana na hao walioondoka, Azam iliwakaribisha wengine wapya. Matajiri hao walianza kwa kumkaribisha Dabo kutoka Senegal mapema tu hata kabla ya msimu haujaiasha.

Azam inaamini Dabo ndiye mjenzi wa enzi mpya za ushindani, ubabe na utawala katika soka Tanzania na Afrika kwa ujumla.

Ili kuhakikisha Dabo anajenga enzi mpya ndani ya Azam, Matajiri hao wa Chamazi wamemruhusu kusajili wachezaji anaowataka pamoja na kuleta wataalamu wa benchi la ufundi wapya anaoamini kwa pamoja wataifikisha timu hiyo kwenye nchi ya ahadi.

Tayari Dabo amewapa mabosi wa Azam mapendekezo ya watu anaowataka kuja kumuongezea nguvu kwenye benchi la ufundi ambao hawapungui watatu na muda wowote watashushwa kikosini hapo.

Pia amewapa mapendekezo ya wachezaji wapya anaowataka na kati yao wapo wawili wa uhakika kutua viunga vya Chamazi mmoja akiwa beki wa kati na mwingine mshambuliaji ambao watatambulishwa mwisho wa mwezi huu.

Aidha Azam imemshusha Fei Toto ikimtoa Yanga alikosema alikuwa akila ugali na Chapati lakini leo anafurahia maisha ya Waoka mikate hao. Usajili wa Fei Toto utaongeza ubora eneo la kiungo la Azam licha ya kwamba kuna mafundi wengi katika eneo hilo.

UBABE KURUDI?

Kila mtu kwa sasa kichwani kwake anajiuliza, baada ya hizo 'Thank You' na 'Welcome', Azam itarudisha ubabe wake wa kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu kama ilivyofanya msimu wa 2013/2014 bila kupoteza mechi yeyote?

Majibu yapo kwa watendaji wapya wa Azam na vitendo vyao katika kazi zao. Uongozi unatakiwa kutimiza majukumu yao kwa ufasaha hivyo hivyo kwa wataalamu wa benchi la ufundi, wachezaji na hata mashabiki pale Jukwaani.

Azam licha ya kutotwaa ubingwa wa ligi lakini sio timu mbaya ya kubeza. Kwa mara kadhaa imezisimamisha Simba na Yanga zisitambe licha ya kupokezana mataji ya ligi lakini pia imetwaa makombe mengine ikiwemo, Mapinduzi na Kombe la ASFC kwa nyakati tofauti.

Kwa maana hiyo Azam inauwezo wa kufanya vizuri zaidi msimu ujao na pengine kutwaa mataji lakini njia pekee ya kuhakikisha hilo linatimia ni kila mtu ndani au nje ya timu hiyo lakini kama inamuhusu kwa namna moja ama nyingine, basi atimize majukumu yake kwa ufasaha.

ITAKUWA HIVI

Baada ya maingizo ya Fei Toto na wachezaji wengine wapya wakiwemo hao wawili ambao mmoja ni beki wa kati na mwingine ni mshambuliaji huenda timu ikabadilika na hivi ndivyo itakavyokuwa.

MAKIPA

Kama Ahmada atasalia Azam, basi eneo la golini litakuwa na makipa watatu, wakiongozwa na Iddrisu Abdulai, Zuberi Foba na Ahmada na tayari kutakuwa na uimara wa kutosha kutokana na uzoefu wa Ahmada na Iddrisu sambamba na ubora wa chipukizi Foba.

MABEKI

Azam huenda ikashusha wageni wapya wawili na mzawa mmoja na kuungana na Lusajo Mwaikenda, Pascal Msindo, Pape Ndoye, Abdallah Kheri, Daniel Amoah, Nathanael Chilambo, na Edward Manyama na hapo kocha atachagua awatumie kina nani.

VIUNGO

Baada ya ongezeko la Fei Toto, Azam haina mpango wa kusajili kiungo mwingine hivyo viungo na mawinga watabaki kuwa Sospeter Bajana, Isah Ndala, James Akaminko, Kipre Junior, Yahya Zayd, Iddi Nado, Tepsei Evance, na Ayoub Lyanga ambapo pia Dabo atakuwa na machaguo mengi.

WASHAMBULIAJI

Dabo tayari amewapa Azam jina la mshambuliaji wa kati ambaye wako mbioni kumshusha kikosini hapo ili aungane na Prince Dube, Idriss Mbombo na Abdul Seleman kwenye safu hiyo kwa msimu ujao na kulingana na ubora wa kila mchezaji katika eneo hilo huenda wakacheka na nyavu zaidi.

KIKOSI KITAKAVYOKUWA

1. Iddrisa 2. Lusajo 3. Manyama 4. Amoah 5. Anatafutwa 6. Ndala 7. Dube 8. Akaminko 9. Anatafutwa 10. Fei Toto 11. Kipre Jr

Mfumo 4:3:3

Chanzo: Mwanaspoti