Matajiri wa Chamazi, klabu ya Azam imetangaza kufikia ukomo na Kocha wake Msaidizi Aggrey Moris Ambros aliyehudumu klabuni hapo tangu 2009.
Huo ni muendelezo wa panga pangua kwenye timu hiyo na vilabu vingine ikiwa ni maandalizi ya msimu wa 2023/24.
Kupitia ukurasa rasmi wake rasmi wa Instagram, Azam imeandika: “Ahsante sana kwa mchango wako ndani ya klabu yetu ukiwa kama nahodha, kocha msaidizi. Ulikuja Azam FC ukiwa mdogo sana mwaka 2009 kama mchezaji hadi leo unaondoka ukiwa sehemu ya benchi letu la ufundi,”imesema taarifa ya klabu hiyo.
Azam ilimaliza nafasi ya tatu Ligi Kuu Tanzania Bara msimu wa 2022/23 ikikusanya alama 59 katika michezo 30 sambamba na kumaliza nafasi ya pili ya Kombe la Shirikisho Azam baada ya kufungwa 1-0 katika mchezo wa fainali dhidi ya Yanga.
Mwanzoni mwa wiki Azam ilitangaza kuachana na Kaimu Kocha Mkuu Kalimangonga Ongala Kocha wa magolikipa Dani Cadena na wa viungo Dk Moadh Hiraoui huku wachezaji wakiwa ni nahodha Bruce Kangwa, Rogers Kolla, Ismail Aziz Kader na Daniel Amoah.