Tetesi mbali mbali za usajili za wacheza soka kutoka barani Ulaya leo Juni 1, 2022.
Klabu ya Real Madrid ya nchini Hispania inakaribia kufikia makubaliano binafasi ya kumsajili kiungo wa kimataifa wa Ufaransa Aurelien Tchouameni mwenye umri wa miaka 22 anaecheza katika klabu ya AS Monaco. Inaripotiwa Tchouameni amezikataa ofa za usajili kutoka klabu za Liverpool na PSG.
Washika bunduki wa Jiji la London klabu ya Arsenal ipo kwenye mipango yakumsajili kiungo wa Leicester City Youri Tielemans raia wa Ubeligiji. Kwa mujibu wa ripoti Arsenal inahitaji kusajili mchezaji mmoja wa safu ya kiungo na Tielemans anampango wa kuondoka Leicester katika dirisha la usajili la majira ya joto.
Mabingwa wa Coppa Italia Inter Milan ya Italia imeanza kufanya mazungumzo na Mwanasheria wa mshambuliaji wa Chelsea Romelu Lukaku ikiwa ni mpango wa kutaka kusamsajili tena mshambuliaji huyo. Lukaku alijiunga na Chelsea msimu ulioisha wa 2021-22 akitokea Inter. Bado Inter Milan hawajafanya mazungumzo na Chelsea lakini inaangaziwa wataomba wasajili Lukaku kwa mkopo.
Klabu za Manchester United, Newcastle United na Arsenal zote zimeonyesha nia yakutaka kumsajili mshambuliaji wa Everton Dominic Calvert-Lewin mwenye umri wa miaka 25 raia wa England. Everton hawapo tayari kumuuza mchezaji huyo lakini wanajua nia ya Newcastle United yakutaka kumsajili mshambuliaji huyo.
Kutoka nchini Hispania inaripotiwa kuwa kocha wa FC Barcelona Xavi Hernandez amefanya mazungumzo na Kiungo wa Wolves raia wa Ureno Ruben Neves mwenye umri wa miaka 25, ikiwa ni katika harakati za kumshawishi mchezaji huyo ajiunge na wakali hao kutoka Hispania.