Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Tetesi za kijinga usajili wa Ulaya 2023

Tetesi Pic Tetesi za kijinga usajili wa Ulaya 2023

Mon, 19 Jun 2023 Chanzo: Mwanaspoti

Dirisha la usajili wa majira ya kiangazi ndio kwanza limefunguliwa na sasa klabu mbalimbali huko Ulaya zipo bize kunasa saini za mastaa wapya kwa ajili ya kuboresha vikosi vyao viwe vya kibabe msimu ujao.

Na kama ilivyo kwenye madirisha ya usajili yanapofunguliwa, kumekuwa na tetesi nyingi, nyingine zinaonekana kama za kijinga hivi kutokana na wachezaji wanaohusishwa kwenda kwenye aina ya timu ambazo kimsingi huoni kama uhamisho huo unaweza kutokea.

Tayari kwenye dirisha hili la uhamisho wa majira ya kiangazi huko Ulaya umeshuhudia dili kadhaa zikiwa zimekamilika, masupastaa Lionel Messi na Karim Benzema wakiachana na soka la Ulaya, wakimtikia Marekani na Mashariki ya Kati mtawalia.

Kiungo Jude Bellingham amekamilisha dili lake la pesa nyingi, Pauni 115 milioni kwenda Real Madrid, huku uhamisho mwingine wa moto ni ule unaomhusu bingwa wa Kombe la Dunia 2022, Muargentina Alexis Mac Allister akitua zake Anfield kukipiga kwenye kikosi cha Liverpool chini ya kocha Jurgen Klopp.

Kwenye dirisha hili la uhamisho wa majira ya kiangazi huko Ulaya umesikia mengi, lakini haya matano hakika yaligeuka kuwa kichekesho kikubwa kwenye usajili huu wa majira ya kiangazi kutokana na wachezaji kuhusishwa na timu hizo ambazo hufikirii kabisa kama uhamisho huo unaweza kufanyika.

NEYMAR KWENDA NEWCASTLE

Miaka kadhaa nyuma, uhamisho huu usingefikiriwa kabisa, lakini kutokana na utajiri wa Newcastle United kwa sasa ndiyo kunakuwa na uthubutu wa kumhusisha supastaa wa Kibrazili, Neymar na timu hiyo. Wanasema hakuna kinachoshindikana, lanini Neymar ndiye mwanasoka ghali zaidi duniani kwa sasa - akiwa amesajili kwa Pauni 198 milioni aliponaswa na PSG kutokea Barcelona mwaka 2017. Lakini, kwenye dirisha hili, Neymar alihusishwa na Newcastle United kwamba atakwenda kujiunga na timu inayonolewa na Eddie Howe.

Hebu vuta hisia, Neymar na Allan Saint-Maximin wanacheza kwenye kikosi kimoja.

EDEN HAZARD KWENDA BURNLEY

Ripoti ya Fichajes imedai kwamba Burnley imevutiwa na mpango wa kunasa huduma ya winga anayeachana na Real Madrid, Real Madrid kwenye dirisha hili la uhamisho wa majira ya kiangazi. Na hilo limechochewa zaidi baada ya Hazard kuachana na Los Blancos, huku Burnley kunolewa na Vincent Kompany, ambaye walicheza kwa mafanikio makubwa na Hazard kwenye timu yao ya taifa ya Ubelgiji.

Jambo hilo linaweza kumrudisha Hazard kwenye mikikimikiki ya Ligi Kuu England kwa mara nyingine, akienda kutamba uwanjani Turf Moor, licha ya kwamba kitu hicho hakionekani kama litakwenda kutokea.

LIONEL MESSI KWENDA CHELSEA

Baada ya kutangaza kwamba ataachana na PSG, uhamisho wa kwenda MLS au Saudi Arabia ndio ulionekana kuwa na nafasi kubwa ya kutokea kwa supastaa Lionel Messi. Hata hivyo, hilo halikuzuia kuibuka kwa uvumi mwingine, hasa ule wa kumhusisha Muargentina huyo na miamba ya Stamford Bridge, Chelsea.

Vyanzo kibao vya habari vilidai kwamba mmiliki wa Chelsea, bilionea Todd Boehly amepanga kumpa Messi dili la kibabe sana ili atue Stamford Bridge. Lakini, hilo limeshindwa kutimia, Messi, 35, ameachana na PSG na kwenda kusaini kuichezea Inter Miami ya Marekani na kuachana rasmi na soka la Ulaya na kufuta ndoto za wengi kumwona kwenye Ligi Kuu England.

GARETH BALE KWENDA WREXHAM

Winga wa Wales Gareth Bale ametangaza kustaafu soka, lakini hilo halikuzuia kuibuka na uvumi mwingi katika dirisha hili la uhamisho wa majira ya kiangazi huko Ulaya. Sawa, Wrexham ilifanikiwa kumtoa kipa Ben Foster kutoka kwenye kustaafu na kurudi uwanjani, lakini suala la kumshawishi Bale arudi uwanjani kucheza kwenye League Two si kitu kinachowezekana kirahisi hata tajiri Ryan Reynolds hatafanikiwa hilo.

Wakala wa Bale, Jonathan Barnett, alisema umekuwa muda mwafaka kwa mteja wake kutundika daruga na sasa ataendelea kufurahia tu maisha yake baada ya kuvuna mkwanja wa kutosha kwenye maisha yake huko Real Madrid.

ROBERTO FIRMINO KWENDA MAN UNITED

Ushasikia miaka ya karibuni kwamba kuna mchezaji anatoka Liverpool moja kwa moja kwenda Manchester United? Si kitu kinachowezakana kutokea kirahisi. Lakini, kwenye dirisha hili la uhamisho wa majira ya kiangazi baada ya supastaa wa Kibrazili, Roberto Firmino kutangaza ataachana na Liverpool, basi mchezaji huyo akahusishwa na mpango wa kwenda Man United.

Mtaalamu mmoja wa masuala ya usajili Ekrem Konur kuna wakati alidai kwamba Firmino amejitoa ofa mwenyewe kwenda Man United. Kwa namna ambavyo Liverpool iliagana na Firmino, huoni kama kama mchezaji huyo atawatibua mashabiki wa timu hiyo na kwenda Liverpool. Huo uvumi ni wa kijinga.

Chanzo: Mwanaspoti