Tetesi za Soka Ulaya 07.11.2021: Vinicius Jr, Solskjaer, Rangnick, Merino, Shevchenko, Wilder, Insigne
Real Madrid itaweka kipengele cha kumruhusu Vinicius Jr, 21 kiasi cha Euro bilioni 1 itakapompa mkataba mpya mshambuliaji huyo Mbrazil mwishoni mwa msimu. (AS in Spanish)
Hatua ya Newcastle United kumtangaza Eddie Howe kama kocha wao mpya inasuasua baada ya kushindwa kuafikiana na Jason Tindall ili awe msaidizi wa Howe. (90 Min)
Manchester United imemuweka kocha wa zamani wa RB Leipzig Ralf Rangnick katika orodha yake ya watakaorithi mikoba ya Ole Gunner Solskjaer iwapo atatimuliwa na Mjerumani huyo anavutiwa na mpango wa kuchukua kazi hiyo Old Trafford. (Christian Falk, Bild Sport head of football)
Kocha wa Tottenham Antonio Conte amekuwa akihusishwa kutaka kurejea kwenye klabu yake ya zamani ya Inter Milan na kusajili baadhi ya wachezaji lakini Meneja wa klabu hiyo ya Serie A, Simone Inzaghi, anasema tetesi hizo hazimuumizi kichwa na "ni mapema mno kufikiria kuhusu dirisha la usajili la Januari". (Football Italia)
Kiungo wa Real Sociedad na Hispania Mikel Merino, 25, ananyatiwa na Liverpool ili kuboresha kikosi chao huku dau la usajili la nyota wa kimataifa wa England anayechezea Borussia Dortmund Jude Bellingham, 18, likionekana kuwa kubwa kwa wekundu hao wa Anfield. (Fichajes.net - in Spanish)
Meneja wa Everton Rafael Benitez amepuuzilia mbali kwamba klabu hiyo ya Goodison Park itamwaga mapesa ya usajili katika dirisha la mwezi Januari. (Times - subscription required)
Mshambuliaji wa zamani wa Chelsea Andriy Shevchenko anatarajiwa kutangazwa kuwa kocha mpya wa Genoa baada ya klabu hiyo ya Italia kumtimua Davide Ballardini. (La Gazzetta dello Sport, via Mirror)
Kocha wa zamani wa Sheffield United Chris Wilder amekubali kuchukua mikoba ya kuinoa Middlesbrough baada ya kuondoka kwa Neil Warnock klabuni hapo. (Teesside Live)
Juventus huenda ikatupa ndoano zake kwa kiungo wa Borussia Dortmund na Ubelgiji Alex Witsel, 32, katika dirisha la usajili la Januari. (Bild, via 90 Min)
Rais wa Napoli Aurelio de Laurentiis amesema uamuzi uko kwa mshambuliaji wa Italia Lorenzo Insigne kama ataamua kusalia kwenye klabu hiyo ya Serie A ama la, huku mkataba wa nyota huyo mwenye umri wa miaka 30 ukielekea ukingoni mwishoni mwa msimu ujao. (Calciomercato)